Helikopta ya Chadema ikiwa angani. |
Mratibu wa Kampeni za CCM katika jimbo hilo, Miraji Mtaturo, aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kutoa msimamo kuhusu tangazo la Chadema kuwa watatumia helikopta siku ya kupiga kura.
"Mwenyekiti, wenzetu Chadema wametangaza kwamba siku ya uchaguzi, wataleta watu zaidi ya 1,000 wakiwemo wabunge wao kulinda kura, lakini pia wamesema watatumia helikopta yao kufanya doria, hiyo haiwezi kuwa doria itakuwa ni kampeni," alisema.
Mtaturo alisema matumizi ya helikopta hiyo ni kinyume na Sheria ya Uchaguzi inayokataza vyama kufanya kampeni siku ya uchaguzi, na pia akataka kujua kama vyama vya siasa vinaruhusiwa kuweka vikundi vyake vya ulinzi karibu na vituo vya kupigia kura.
Akijibu hoja hiyo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema ni muhimu kwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huo vikazingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.
Jaji Lubuva alisema hayo katika mkutano wa NEC na viongozi wa vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi huo, uliofanyika jana katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, mjini hapa.
Hata hivyo, hakufafanua kama ni makosa au la kutumia helikopta siku ya uchaguzi.
Chombo hicho ni cha usafiri kama ilivyo gari, pikipiki au baiskeli, ambavyo havizuiwi na sheria kutumia siku ya kupiga kura.
Kwa kawaida, hata magari yaliyokuwa yakitumika wakati wa kampeni, siku ya uchaguzi yanaruhusiwa kutumika lakini bila vipeperushi au alama yoyote ya mgombea.
Hata hivyo, pamoja na kuwa helikopta imekuwa ikitumika kama nyenzo ya usafiri, katika siasa za Tanzania imekuwa ikitumika kama nyenzo ya kukusanya vijana na wasikilizaji katika mikutano ya kampeni.
Hilo linadhihirisha na matumizi ya helkopta za kisiasa kupaa kutoka katika kiwanja kimoja kwenda katika kiwanja kingine kilicho umbali usiozidi kilometa moja, kusindikiza maandamano na hata kuvutia watazamaji kwa kusimama angani.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limeahidi kuwakamata na kuwafungulia mashitaka walinzi wa vyama vya siasa watakaonekana kuzagaa karibu na vituo vya kupigia kura.
"Kazi ya Polisi ni pamoja na kuhakikisha amani inakuwepo wakati wa upigaji kura na utangazaji wa matokeo; sitaki kusikia habari ya vikundi vya ulinzi vya CCM Green Guard na Chadema Red Brigade," alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi.
Uchaguzi huo utakaofanyika Jumapili Machi 16, mwaka huu unahusisha vyama vitatu vya siasa; CCM ambayo imemsimamisha Godfrey Mgimwa, Chadema Grace Tendega na Chausta Richard Minja.
Pia Lubuva aliwataka wananchi kuondoka katika vituo vya kupigia kura mara baada ya kupiga kura kwani kazi ya kulinda na kuhesabu kura itafanywa na mawakala wa vyama pamoja na maofisa wa Tume.
No comments:
Post a Comment