MVAMIZI KIWANJA CHA MWALIMU NYERERE AMPUUZA MKUU WA WILAYA...

Ukuta uliojengwa kwa siku mbili kwenye kiwanja cha Nyerere.
Ni wazi sasa kuwa mvamizi katika kiwanja cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ana kiburi na jeuri kwa kuwa ameamuru ujenzi kuendelea kinyume cha agizo la Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana.
Rugimbana alimwambia mwandishi kuwa ameshazuia ujenzi kuendelea katika kiwanja hicho, ili kupisha mazungumzo kati ya warithi ambao ni familia ya Mwalimu Nyerere na mfanyabiashara anayedai kununua eneo hilo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa zilizotufikia jana, mfanyabiashara huyo ameanza kuendelea na ujenzi katika kiwanja hicho kwa kutumia utaratibu ule ule wa ulinzi wa watu wa miraba minne.
“Sasa kuna wavamizi wawili; huyu wa pili ni rafiki wa familia ya Mwalimu Nyerere na alipoambiwa kuwa taarifa ipo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni juu ya mgogoro huo, alisema Mkuu huyo wa Wilaya kwake ni mdogo hawezi kumheshimu ni bora kuheshimu familia ya Mwalimu Nyerere.
"Tunajiuliza kama ameweza kujenga ukuta kwa muda wa siku mbili, tena ukuta mkubwa. Sasa kama Serikali itaamua kukaa kimya kwa mwezi, si watajenga ghorofa tano pale?" Alihoji mtoa habari wetu.
Akizungumza na mwandishi jana, mtoa habari huyo kutoka katika familia hiyo, alibainisha kuwa mara tu ujenzi huo ulipoanza, kuliibuka kutokuelewana kati ya wafanyabiashara wawili (majina tumeyahifadhi), uliosababisha wawekane ndani.
Akielezea kisa cha wafanyabiashara hao kufikishana Polisi, mtoa habari huyo alisema mvamizi wa kwanza alimkuta mvamizi wa pili akiwa katika kiwanja hicho pamoja na mafundi, akiwapa maelekezo ya kuendelea na ujenzi.
"Baada ya kuona yule yuko na mafundi akiwaelekeza waanze ujenzi, huyu mvamizi wa kwanza aliondoka na baada ya muda akarudi na magari mawili ya Polisi wakamkamata mvamizi aliyekuwa na mafundi wakaondoka naye," alisema mwanafamilia huyo.
Alisema mvamizi huyo anayejenga, alikaa kituoni kwa muda wa  saa nne siku ya Jumatano iliyopita na alipotoka siku iliyofuata ya Alhamisi, alienda na Polisi na kumkamata mfanyabiashara wa kwanza na kumweka ndani kwa siku nzima.
"Huyu mvamizi wa kwanza alipotoka akashangaa kukuta tayari ukuta umefikia nusu, jambo ambalo hata sisi tunashangaa huyu mvamizi wa pili nguvu hizi anatoa wapi," alidai.
Mvamizi wa pili anayejenga, kwa mujibu wa mtoa habari wetu, anadai ameuziwa kiwanja hicho mwezi uliopita, wakati akijua wazi kuwa kiwanja hicho ni cha familia ya Mwalimu Nyerere na kina mgogoro kutokana na yeye kuwa karibu na familia hiyo.
Mtoa habari huyo alidai kuwa baada ya kusikia kuwa mvamizi huyo wa pili, naye ameamua kuingia katika kiwanja hicho chenye mgogoro, kwa kuwa  amekuwa  akifahamiana na familia ya Mwalimu, walimuita na kumhoji vizuri kwa nini ameamua kufanya hivyo, akawajibu kuwa angekuja lakini hakufanya hivyo.
"Huwezi kuamini hata huyu kaamua kuungana na waporaji na sasa wanagombana wakati anaifahamu vizuri sana familia na alikuwa anakuja nyumbani,” aliongeza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alipopigiwa simu ili kujua kama kweli watu hao walifikishwa kituoni, alisema hakuna suala kama hilo la uvamizi wa kiwanja cha Mwalimu Nyerere na yeye hafahamu lolote.
"Unapotaja jina la Nyerere unamaanisha Baba wa Taifa hili, kwa hiyo linakuwa ni jambo lingine kabisa, hapa hakuna kitu kama hicho," alisema Kamanda Wambura.
Akizungumza kwa njia ya simu mwanafamilia mwingine alisema, wakati ujenzi ukiendelea, alimuona mtoto mmoja wa  mfanyabiashara maarufu nchini (jina limehifadhiwa), akifika katika eneo hilo kukagua ujenzi, jambo lililomfanya  aamini anahusika moja kwa moja.
"Hii itakuwa ni kweli kabisa anahusika kwa sababu tumeambiwa nyumba yake imepakana na kiwanja hiki. Hii jeuri wanaitoa wapi?" Alihoji.
Akiendelea kuzungumzia suala hilo, mtoa habari wa kwanza aliendelea kusema kuwa kwa sasa eneo hilo linaendelezwa kwa ujenzi, ambao unasimamiwa na watu wa miraba minne.
Mwandishi alifika eneo hilo kushuhudia na kukuta ujenzi wa ukuta ukiendelea huku watu hao wa miraba minne wakilinda.
"Kuna zuio la kuendelea kwa ujenzi lakini huwezi kuamini ukuta mkubwa umejengwa ndani ya siku mbili usiku na mchana. Sasa tunaona kama Serikali ilituzuia ili wale waendelee na ujenzi," alidai mtoa habari wa kwanza.

No comments: