FOLENI SUGU YA KIMARA KUANZA KUPUNGUA WIKI HII...

Ujenzi ukiendelea Barabara ya Morogoro.
Kampuni ya Strabag   inayoendelea na ujenzi wa barabara chini ya mradi wa mabasi yaendayo haraka, imeruhusu upande mmoja wa barabara uliokamilika, kutumika kupunguza foleni  ya magari yatokayo Kimara kwenda katikati ya jiji.  
Mhandisi wa Wakala wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart), John Shauri alitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari  mwishoni mwa wiki.
Licha ya kuruhusu upande mmoja wa barabara, kampuni imeruhusu pia vituo vitano vitumike kwa kugeuzia magari kwa muda wa miezi sita mpaka maeneo matatu ya kudumu yatakapokamilika katika kipindi hicho.
“Kuruhusu upande mmoja kutumika na pia maeneo ya kugeukia magari kumesaidia sana kupunguza foleni kwa magari yanayotoka Kimara kwenda Ubungo na yale yanayotoka Ubungo kwenda Kimara,” alisema Shauri.
Mhandisi huyo ametaka madereva kuwa waangalifu na mwendo kwani wastani wa mwendo unaotakiwa ni kilometa 50 kwa saa na si vinginevyo kwani mwendo kasi utasababisha ajali zisizo za lazima.
“Mwendo wa kawaida utasaidia sana maeneo ambayo yameruhusiwa magari kugeuka na kuelekea sehemu husika bila kusababisha ajali,” alisema.
Shauri ambaye alifuatana na Mshauri Mkuu wa Ufundi wa Mradi huo, Dieter Schelling, alitaja vituo hivyo vitano vya kugeuzia kuwa ni Kimara Kona, Kimara Baruti, katikati ya Kimara Bucha, Kimara Kwa Thomas, Kimara Resort na Kimara Mwisho.
“Kwa sasa magari katika barabara hii ya Morogoro  yanapita pasipo msongamano mkubwa kama ilivyokuwa awali na kurahisisha watu kutoka Mbezi, Kibamba kuwahi kwa wakati katika shughuli zao,” alisisitiza.
Alisema wakati ujenzi ukiwa unaendelea ni vyema daladala zikaendelea kutumia barabara za pembeni badala ya kutumia barabara kubwa kwani itapunguza msongamano.
“Katika kipindi hiki usimamizi wa zoezi hili unahitaji kuungwa mkono na askari wa barabarani kuwadhibiti madereva wote wanaotembea kwa mwendo kasi ili kupunguza ajali ambazo zinaweza kuepukika.
Kwa mujibu wa mhandisi huyo, vituo vya kudumu vya kugeuzia vitajengwa Kimara Baruti, Kimara Bucha  na Kimara Mwisho.
Mradi huo mkubwa wa ujenzi unasimamiwa na Wakala wa Usimamizi wa Barabara nchini (Tanroads). DART iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Hivi karibuni, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya  mradi wa mabasi yaendayo haraka, na kueleza kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi unaofanywa na kampuni ya Strabag kutoka Ujerumani.

No comments: