Ukumbi wa Bunge la Katiba. |
Shughuli za wiki hii, licha ya mjadala huo, pia wajumbe hao watapigwa msasa na wataalamu wa mambo ya Katiba kutoka nje ya nchi kesho, kabla ya bunge hilo kuhutubiwa na Rais Jakaya Kikwete kesho kutwa.
Kwa shughuli hizo, ni wazi kuwa hii itakuwa ni wiki yenye shughuli nyingi kwa wajumbe hao, ambao licha ya kumaliza mwezi mzima wakiwa mjini Dodoma, wametumia wiki tatu kutunga Kanuni na wiki nyingine kwa ajili ya kuchagua viongozi wa bunge hilo na kula kiapo.
Tayari robo tatu ya wajumbe wameshaapa, wamebaki wachache tu ambao kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta wataapishwa leo asubuhi, kabla ya Jaji Warioba kuwasilisha rasimu ya Katiba jioni.
Katika kipindi cha wiki nne za kuwepo mjini hapa, wajumbe wa Bunge hilo wameonekana dhahiri, kutofautiana kimsimamo, jambo ambalo linafanya mijadala ya siku tatu kabla ya kuanza kugawanyika kwenye kamati kuwa moto.
Bunge hilo ambalo lina wajumbe 629, kati ya hao wanasiasa ni 428 wakati wajumbe ambao wameteuliwa na Rais ni 201. Lakini katika kundi hilo, pia kuna wanasiasa ambao wametokana na vyama vya siasa, lakini pia wengine wamechomokea kutoka katika makundi mengine, ambayo ni miongoni mwa wateule wa Rais.
Hata hivyo, Rais Kikwete aliwahi kuzungumzia suala hilo, akiweka wazi kuwa Katiba ni mchakato wa kisiasa na hata wajumbe kutoka makundi maalumu wakichunguzwa vizuri, watabainika kuwa na vyama.
Ndani ya vyama vya siasa kwenyewe, wabunge wamegawanyika na mgawanyiko huo ndio umekwamisha hata Bunge hadi sasa kushindwa kupata namna ya kufanya uamuzi, kama uwe wa kura ya wazi au ya siri.
Kutokana na Bunge hilo kutawaliwa na wanasiasa wengi, wasiwasi unakuja kwamba maeneo ambayo rasimu ya Katiba inaonesha kwenda kinyume na misimamo ya vyama, yanaweza kupata upinzani mkubwa kutoka kwa wanasiasa hao.
Moja ya maeneo hayo ni Sura ya 6 ya Rasimu ya Katiba, inayozungumzia muundo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo ilitawala mjadala mara tu baada ya kutoka kwa rasimu ya kwanza na ya pili ya Katiba.
Rasimu ya Katiba itakayowasilishwa leo jioni na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, inapendekeza Muungano wa Tanzania wenye serikali tatu kutoka serikali mbili, kwa maelezo kuwa ndio njia pekee ya kudumisha Muungano na kuondokana na kero za Muungano zilizopo kwa sasa.
Muundo huo umekuwa ukitetewa na Tume ya Jaji Warioba kuwa ndio suluhisho la kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kutokana na mwenendo wa siasa za hapa nchini ulivyo.
Lakini mapendekezo hayo, yamepingwa na wadau mbalimbali, wakiwemo wasomi, viongozi wa dini na CCM ambayo inasisitiza kuwa serikali mbili katika sera yake ya kuiongoza Tanzania.
Viongozi walio nje ya CCM wanaopinga serikali tatu ni pamoja na Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo ambaye msimamo wake binafsi ni serikali mbili, akiungwa mkono na wasomi kadhaa.
CCM yenyewe imekuwa na sababu nyingi za kutetea muundo huo wa Muungano na moja ya sababu zake ni kwamba serikali tatu ni gharama kubwa kuziendesha na hali hiyo itaifanya Serikali ya Tanganyika, kubeba mzigo mzito katika kuendesha Serikali ya Muungano wa Tanzania.
Hoja hiyo inatokana na ukweli kwamba nchi washirika, ambazo zinatajwa kwenye rasimu ya Katiba-Tanganyika na Zanzibar, haziko sawa kieneo, kiuchumi na idadi ya watu, jambo ambalo CCM inaona kuwa bado mfumo wa Serikali mbili ni muafaka katika kudumisha Muungano uliopo.
Kwa wale ambao wanataka serikali tatu, wanaamini kuwa Katiba inayoandikwa sio ya wanasiasa, ambao wana maslahi katika miundo ya mfumo wa serikali zinazounda Muungano, bali ni ya wananchi walio wengi ambao wanaamini katika muundo wa serikali tatu.
Jaji Warioba mwenyewe ambaye tume yake ilisheheni wasomi, wanasiasa na wanasheria kutoka pande zote za Muungano, anatetea mfumo huo kuwa uendeshaji wake utakuwa wa gharama ndogo kuliko ilivyo sasa, kutokana na kupunguza mambo yatakayoshughulikiwa na serikali ya Muungano.
Eneo lingine ambalo litaleta mjadala kwa wanasiasa ni eneo la kukataza mawaziri wasiwe wabunge, jambo ambalo linawazuia na kuwaondolewa nguvu wanasiasa ya kuendelea kuziongoza wizara zinazotekekeza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Katiba inawapa haki mawaziri kupata maslahi manono, jambo ambalo limewafanya wasomi wengi kuacha kazi za kuajiriwa na kwenda kwenye siasa wakiamini kuwa wanaweza kuteuliwa kuwa mawaziri.
Rasimu ya katiba inawazuia wabunge wasiwe mawaziri, jambo ambalo wachunguzi wa mambo wanaona kuwa wanasiasa watalipinga kwa nguvu kwenye Bunge hilo.
Wasiwasi mwingine kwa wanasiasa hao, ambao wengi ndani ya Bunge la Katiba ni kwamba wanaweza kupinga ibara inayotaka wabunge kuwa na ukomo ambao ni miaka 15; jambo ambalo litawaondolea wanasiasa wengi kugeuza ubunge kama ajira ya kudumu.
Eneo hilo wanasiasa hao wanaweza kulipinga, kwa hoja kuwa mbunge aondolewe na wananchi wenyewe pale anapoona hawafai tena kuwaongoza uchaguzi mwingine unapofika; lakini kama anawatumikia vizuri wapiga kura wake ni vyema akaendelea na wadhifa wake bila kujali ametumika kwa miaka mingapi.
Pia, kuna eneo ambalo linawapa nguvu wananchi kuwaondoa wabunge wao, pale watakapoona inafaa hata kabla ya muda wa uchaguzi kufika, pale wanapoona kuwa mbunge huyo hawafai. Eneo hilo kwa maslahi ya wanasisa, wanaweza kulipinga na hivyo kuleta mjadala mkubwa ndani ya wiki hii.
No comments:
Post a Comment