WANAFUNZI WASIOJUA KUANDIKA WASOMEA GESI VETA...

Chuo cha VETA Lindi.
Wanafunzi 64 waliojiunga katika Chuo cha Mamlaka Ufundi Stadi (Veta) mjini Lindi mkoani humo mwaka jana, baadhi yao wamebainika hawajui kusoma wala kuandika.
Mkuu wa Chuo cha Veta Lindi, Malisa Leonard amesema hayo jana wakati alipozungumza na mwandishi wa habari hizi, ofisini kwake mjini hapa.
Alisema wanafunzi hao waliletwa kupata mafunzo ya gesi, lakini wana matatizo ya kutofahamu lugha ya Kiingereza,  kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Kwa mujibu wa Leornad, wanapata shida kuanza kuwafundisha kwa kuwa kazi zote za gesi na mafuta zinatawaliwa na mawasiliano na hesabu.
Leornad alisema kinachotakiwa wazazi wawekeze kwenye elimu kwa watoto ili wapate vijana ambao wanaweza kufanya kazi na  kampuni hizo za kigeni, mkoani hapa.
Alisema isipofanyika juhudi za makusudi na kuingiza wanafunzi wengine kama hao watapokewa lakini ieleweke matunda yake yatakuwa magumu.
Hivi karibuni, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi alikieleza kikao maalumu cha Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kuhamasisha wazazi
wawasomeshe watoto wao ili kukabiliana na soko la ajira.
"Watoto wetu tuwasomeshe kwani kampuni hizi zinazoletwa zinataka wafanyakazi wenye elimu kulingana na kazi zilizoko hapo," alisema Maswi.
Alisema Wizara hiyo inasomesha vijana karibu 50 wanaotokea mkoani Lindi, lakini kati ya hao Wilaya ya Kilwa ilipata upendeleo kuwapo wengi, kuliko wilaya zingine.

No comments: