Dk Titus Kamani. |
Dk Kamani ambaye ni Waziri mpya pekee ambaye hakuwahi kuwa Waziri kabla, na katika uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwezi uliopita alitoka kuwa Mbunge mpaka Waziri, amesema hali ya ranchi hizo zenye ukubwa wa zaidi ya hekta 400,000 hairidhishi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo ranchi ndogo zipo 124 zenye ukubwa wa hekta 286,235 na uwezo wa kutunza ng’ombe bora 120,000, lakini hadi sasa zina ng’ombe 53,416 pekee.
Pia zipo ranchi za mfano 10 zenye eneo la ukubwa wa hekta 235,768 na uwezo wa kutunza ng’ombe bora 90,000 hadi 100,000 lakini chakusikitisha hadi sasa zina ng’ombe 14,371 tu.
Akizungumza na wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Narco jana Dar es Salaam, Dk Kamani aliagiza Bodi hiyo kuanza na ukaguzi wa wawekezaji wazawa waliomilikishwa ranchi za ufugaji na kuhakiki kama wanazingatia mikataba yao, watakaokutwa wamekiuka mikataba, ifutwe na kunyang’anywa ranchi hizo mara moja.
Alifafanua kuwa ametoa agizo hilo kwa kuwa ranchi hizo hazifanyi vizuri, hivyo ni vema Bodi ikague wote waliomilikishwa maeneo hayo, ili ijiridhishe wanavyoendesha ufugaji wao na kupeleka kwake taarifa za waliokiuka utaratibu, mkataba ufutwe na kunyang’anywa maeneo.
“Wamiliki wote waliokabidhiwa ranchi ndogo, wanatakiwa kufuga kisasa na kuweka miundombinu muhimu kwa ajili ya mifugo, kama walivyoainisha katika mpango wa biashara waliowasilisha wakati wa kuomba kumilikishwa maeneo hayo.
“Kutokufanya hivyo ni kinyume cha mkataba na Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali wote watakaoenda kinyume. Kila mwekezaji anatakiwa kuwa na fikra za kibiashara na juhudi za kupata mitaji mikubwa katika taasisi za fedha ili kufanikiwa kufuga kibiashara,” alisema Dk Kamani.
Dk Kamani alisema maeneo waliyopewa wawekezaji hao, hawakuuziwa bali walimilikishwa ili Serikali kupitia Narco, iyasimamie kwa karibu na Bodi hiyo inapaswa kujenga mifumo na utaratibu mzuri kuhakikisha malengo yanafikiwa na yanakuwa endelevu kupitia sekta binafsi ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi.
Katika hatua nyingine, Dk Kamani ametaka Bodi hiyo kuzingatia nidhamu katika matumizi ya rasilimali hasa fedha, kwa kuepuka kujiwekea posho kubwa hasa wakitambua kuwa wamepewa dhamana katika kipindi chenye changamoto kubwa katika sekta ya mifugo na uvuvi na sekta nyingine ya kilimo.
“Naomba Bodi na kampuni nzima ya Narco mbadilishe sura hii mbaya huko nje, sekta haifanyi vizuri, mkumbuke Rais Jakaya Kikwete mwaka 2009 na 2011 aliagiza ujenzi wa ranchi Ruvu ukamilike na ranchi zote zifufuliwe, kama kuna mtu, kanuni au sheria ni kikwazo, zibainishwe tushughulikie,” alisema Dk Kamani.
Dk Kamani aliiambia Bodi kuwa dhamana yao kuhakikisha sekta ya ufugaji inastawi, haipaswi kuzuiwa na mtu yeyote kwani kwa muda mrefu kumekuwa na migogoro baina ya wakulima na wafugaji, iliyosababisha watu kuchinjana kama wanyama na mifugo kuuawa.
Wakati Dk Kamani akitoa maelekezo hayo kwa Bodi, alisisitiza pia utekelezaji wa agizo hilo la Rais Kikwete la 2009 na 2011 kwa Wizara hiyo, ambapo pamoja na mambo mengine aliagiza Wizara kuweka mazingira ya kumaliza migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
Katika hilo, aliagiza Wizara kupima maeneo ya ranchi na kuandaa mpango wa uwekezaji kibiashara kwa kila ranchi, kubaini na kuainisha fursa zilizopo kama vivutio katika kutafuta wabia.
Dk Kamani alisema maagizo hayo pamoja na lile la kuendelea kunenepesha mifugo katika ranchi na kuingia mkataba wa wenye ranchi ndogo katika unenepeshaji huo, zitachangia kuzalisha nyama bora.
Hata hivyo alisema ikiwa ufugaji utaendelea kuwa holela na duni na wenye migogoro kila kukicha, agizo la Rais litakwama na yeye hayupo tayari kuiangusha Serikali.
Kutokana na upungufu uliopo wa maeneo ya malisho ya mifugo, uliochangia kuwepo kwa migogoro, tayari Wizara kwa kushirikiana na halmashauri na wilaya kote nchini, inafanya tathmini ya maeneo yenye nafasi, ili kupanga wafugaji wasigombee maeneo na kuwezesha ranchi zilizopo kuzalisha zaidi.
Dk Kamani alisema hatua ya kwanza ya tathmini hiyo inafanyika kwa kuwabaini wafugaji kote nchini.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Salum Shamte alimhakikishia Waziri na wananchi kuwa, watafanya kazi kwa ufanisi, ubunifu na ushirikiano baina yao, sekta binafsi na Serikali na katika muda mfupi, Watanzania wategemee mabadiliko makubwa.
Narco inahitaji Sh bilioni 17.1 ili ijiendeshe ikiwa ni pamoja na ukarabati wa miundombinu na mifugo ya kutosha na Dk Kamani alisema Wizara itatafuta vyanzo zaidi vya mapato kuiimarisha kampuni hiyo.
No comments:
Post a Comment