WAFANYABIASHARA WAIHENYESHA TRA, BADO WAGOMEA MASHINE ZA EFDs...

Baadhi ya maduka Kariakoo, Dar es Salaam yakiwa yamefungwa kuunga mkono mgomo huo.
Mgomo wa wafanyabiashara dhidi ya mashine za kielektroniki (EFDs) umetafsiriwa kuwa na ajenda ya siri kutokana na ushawishi unaodaiwa kufanyika nchi nzima huku katika maeneo mengine, ukiungwa mkono na wachuuzi wasiohusika na mashine hizo.
Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani Dodoma  kimeeleza kushangazwa na wafanyabiashara  kugomea mashine za kielektroniki za kukusanyia kodi (EFDs) wakati suala hilo likijadiliwa na ofisi ya  Rais.
Katika kile kinacholeta maswali juu ya mantiki ya migomo hiyo, ni hali iliyobainika mkoani Kigoma ambako  umetafsiriwa kuwa na ajenda ya vurugu baada ya wafanyabiashara ndogo wakiwemo wa nyanya na mahindi,  wasiohusika na mashine hizo, pia kugoma kufungua biashara. 
Mkoani Mwanza ambako pia wafanyabiashara waligoma leo,  serikali imeagiza Polisi  kutoa ulinzi kwa wafanyabiashara walio tayari kufungua maduka yao na kuendelea na biashara.
Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Dodoma, Faustine Mwakalinga alikanusha  kuwepo mgomo wa mkoa mzima. Hata hivyo alisema wanaogoma kushinikiza serikali kuondoa mashine hizo, ni sawa na kijiko cha sukari katika bahari kwa kuwa hakiwezi kubadilisha ladha.
Alisema ni vyema wakaendelea na biashara zao wakisubiri matokeo ya mazungumzo kati ya wawakilishi wa wafanyabiashara na serikali kuhusu mashine hizo. Hata hivyo Mwakalinga alikanusha kuwepo kwa mgomo wa kimkoa , badala yake, alisema waliogoma ni wa Kata ya Madukani katika Manispaa ya Dodoma.
"Matatizo yapo ila wafanyabiashara wanapogoma kwa ngazi ya mkoa ni kama kuweka kijiko cha sukari kwenye bahari," alisema na kuongeza kwamba wafanyabiashara hao wanagoma wakati suala hilo likiwa kwenye majadiliano Ofisi ya Rais.
"Wanatakiwa kusubiri kuona matokeo ya majadiliano ya mezani na si kugoma bila kupata matokeo hayo," alisema. Alisema ingawa mashine hizo zinauzwa kwa bei kubwa, elimu kwa wafanyabiashara haitoshi.
Kwa upande wa mkoani Mwanza, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo alisema suala la matumizi ya mashine hizo, ni maelekezo ya serikali ambayo yeye hawezi kwenda kinyume.
Kutokana na mgomo huo, leo saa  5.30 asubuhi gari la matangazo lilipita na kutangazia wafanyabiashara kufungua maduka yao na kuendelea na biashara zao. Hata hivyo hakukuwa na mabadiliko kwani maduka yaliendelea kufungwa huku wenye maduka wakiwa nje.
Ndikilo alisema suala la biashara ni la mtu binafsi kwani baadhi wako tayari kufungua lakini wanashawishiwa  na wengine kwa vitisho, jambo linalowatia hofu kufungua.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa,  wanaoshawishi wamesambaza vipeperushi vinavyotaka  kufunga maduka yao kuanzia sasa kwa muda usiojulikana ili kuungana na wenzao nchi nzima hadi hapo Rais atakapotoa tamko juu ya madai na malalamiko dhidi ya mashine hizo.
 “Tayari nimemwagiza Kamanda wa polisi mkoa kufuatilia wanaosambaza vikaratasi hivyo na mahali vilipochapishwa na walio tayari kufanya biashara jeshi litasimamia usalama wao,” alisema Ndikilo.
Alisema mwezi uliopita,  alikutana na wawakilishi wa wafanyabiashara na viongozi wa TCCIA na kupeana maelekezo kwamba TRA waendelee kutoa elimu. Alieleza kushangazwa na hatua yao ya kufunga maduka.
Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa jijini hapa wanaotumia mashine hizo, wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema wako tayari kufungua maduka  lakini wanahofia usalama wao kutoka kwa baadhi ya wenzao wanaoongoza mgomo huo.
Kutoka Kigoma, taarifa zinasema pia wafanyabiashara wameanza mgomo waliodai hauna muda wa ukomo ikiwa ni hatua ya kuunga mkono wenzao wa mikoa mingine.
Mwandishi wa habari hii alitembelea masoko ya Mwanga na soko kuu la mjini Kigoma ambapo alishuhudia maduka ya ndani na nje  ya masoko hayo yakiwa yamefungwa huku wafanyabiashara wakiwa kwenye vikundi wakijadili.
Katika hali ya kushangaza, mwandishi alishuhudia pia wafanyabiashara wadogo ambao hawahusiki na mashine hizo, wakiwemo wauza mahindi, wauza nyanya na matunda, pia wakiwa wamefunga biashara zao na kujiunga na mgomo.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Kigoma, Augustino Mukandara alisema ni jambo la kushangaza kuona wafanyabiashara wakubwa wakigoma kutumia mashine hizo wakati wakifahamu walishazungumza na mamlaka na kukubali.
Mukandara alieleza pia kushangazwa na wafanyabiashara ndogo kufunga biashara wakati hawako katika matumizi ya mashine hizo.
Kwa mujibu wa meneja huyo wa TRA, wafanyabiashara wanaopaswa kununua na kutumia mashine hizo, ni wenye mitaji inayoanzia Sh milioni 14. 
"Baadhi ya wafanyabiashara wameingia kwenye mkumbo usio  wao, mashine zinawahusu wafanyabiashara wa kiwango cha kati ambao mauzo yao yanafikia Sh milioni 14, sasa hata wale wenye mitaji midogo nao wanagoma hiyo ni vurugu tu hakuna kingine hapo," alisema Mukandara.
Wafanyabiashara katika mikoa kadhaa wanadaiwa kushawishiana kugoma kufungua maduka yao wakishinikiza serikali kuondoa mashine hizo. Mikoa mingine ambayo wafanyabiashara wamegoma ni  Ruvuma, Iringa, Mbeya na maeneo kadhaa ya mkoa wa Dar es Salaam hususani Kariakoo.

No comments: