KANISA LA PENTEKOSTE LAMTAKA KIKWETE AWAKUMBUKE BUNGE LA KATIBA...

Rais Jakaya Kikwete.
Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (PCT) limemwomba Rais Jakaya Kikwete awafikirie  kuwapa  nafasi  za uwakilishi katika Bunge Maalumu la Katiba litakaloanza siku saba zijazo.
Aidha, limeomba viongozi wa madhehebu mengine ya Kikristo wasiwatenge katika masuala yanayohusu dini na taifa, kwa kuwa nao ni sehemu ya jamii inayostahili kuhusishwa na mambo mbalimbali yanayoendelea nchini.
Wamesema licha ya kupendekeza majina tisa kwa ajili ya uteuzi, wamesahauliwa kwenye bunge hilo hivyo wanaomba wapatiwe angalau nafasi mbili.
Askofu Mkuu wa PCT, David Batenzi alisema Rais ana uwezo wa kufanya jambo jema la kuwapa nafasi ya uwakilishi, hivyo awafikirie kwa kuwa bado bunge hilo halijaanza.
"Tumeona wenzetu wa madhehebu mengine ya Kikristo wamepata uwakilishi wa nafasi tano hadi 10 hivyo, tunamwomba Rais Kikwete atupe na sisi angalau nafasi mbili, tuweze kuwasilisha mawazo yetu" alisema.
Askofu Batenzi aliendelea kusema, “Jamii haina budi kutuelewa kwa sababu kutopata nafasi hiyo kwetu ni kama kutengwa, kwa hiyo tusingependa jambo hili litawale vichwa vya Wapentekoste kuwa tunatengwa na Serikali yetu sikivu ndio maana tunamwomba Rais afanye linalowezekana keki hiyo tuile wote.”
Akionesha kutambua busara za Rais Kikwete, Batenzi alisema kuwa anaamini pengine uamuzi wake wa kuacha kuwajumuisha kwenye orodha ya wajumbe wa bunge hilo kumetokana na kuamini kuwa imani yao (Wapentekoste) ni sawa na imani ya Wakristo wengine, ilhali ipo tofauti kubwa.
Alitupia lawama  viongozi wa madhehebu mengine ya Kikristo akisema wamekuwa kimya wakati wote Wapentekoste wanapotengwa katika shughuli za kitaifa na kidini, hivyo kuwa sawa na watu wengine wanaowatenga. 
Walifafanua kwamba uwepo wa baadhi ya viongozi wa Kipentekoste kama vile  Mchungaji Christopher Mtikila, haukutokana na kuteuliwa kuwakilisha madhehebu hayo isipokuwa ameteuliwa kuwakilisha nafasi ya kisiasa.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Fellowship, Zacharia Kakobe alitoa ufafanuzi kuhusu tofauti ya Wapentekoste na Wakristo wengine kuwa ni pamoja na asili ya kunena kwa lugha, pamoja na kuwa waumini kwa kuchagua wenyewe, na si kwa sababu ya kufuata imani ya wazazi wao.
"Watanzania wanapaswa kutambua kuwa walokole yaani Wapentekoste hawafanani kiimani na Wakristo wengine ingawa  sisi sote ni Wakristo. Kutokana na ukweli huo na kama madhehebu halali yaliyosajiliwa kisheria, tunapaswa kuwa na uwakilishi wetu kwenye masuala kama haya ya katiba vinginevyo tunakuwa tumeporwa haki yetu", alisema Kakobe .
Katika hatua nyingine, baraza hilo lilisema kuwa, huenda likafanya mkutano wa wapentekoste wote nchini kuzungumzia suala hilo, endapo hapatakuwa na jitihada zozote za kulitafutia ufumbuzi.
Wakati huo huo  visiwani Zanzibar, jamii ya Masingasinga wameeleza kusikitishwa na uteuzi wa wajumbe wa bunge hilo la katiba wakisema haukuzingatia nafasi ya waumini wa dini nyingine zenye idadi ndogo ya wafuasi.
Kwa upande wa jamii ya Masingasinga Zanzibar,  aliyewahi kuwa mbunge wa  jimbo la Kikwajuni, Parmukhi Hoogan Sigh, alimwambia mwandishi kwamba katika kundi la viongozi wa dini, nafasi 20 zimetolewa lakini kwa upande wa Zanzibar ni wawakilishi wa dini mbili; za Kikristo na Kiislamu  walioteuliwa kuingia katika bunge hilo.
Alisema kitendo hicho kitafanya katiba mpya kukosa uwakilishi wa makundi mengine ya waumini wa dini mbali mbali.
“Sisi wafuasi wa dini zenye waumini wachache hapa Zanzibar Masingasinga,Wahindu pamoja na Maparisi tumesikitishwa sana kuenguliwa na kushindwa kupewa kipaumbele katika ushiriki na uteuzi wa viongozi wa dini,” alisema .
Parmukhi ambaye alikuwa mbunge Kikwajuni kwa tiketi ya CCM tangu  2000 hadi 2010 alisema mchango wa waumini wa dini ndogo zenye wafuasi wachache Zanzibar ni mkubwa tangu enzi za kupigania uhuru.
Alisema kitendo cha kutoshirikishwa  katika mchakato wa katiba, kitawanyima fursa mbali mbali muhimu katika jamii ikiwemo sikukuu za kidini kama ilivyo kwa Waislamu na Wakristo.
“Sisi ni wachache lakini tunahitaji kupewa kipaumbele cha kwanza kwa sababu ni sawa na makundi yenye mahitaji maalumu kama ilivyo walemavu,” alisema.
Wajumbe 20 wa Bunge Maalumu la Katiba waliteuliwa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa upande wa bara, wajumbe ni 13 ambao ni  Tamrina Manzi , Olive Luwena,  Shamim Khan,  Mchungaji  Ernest Kadiva, Shehe Hamid Jongo na Askofu Mkuu (Mstaafu) Donald Mtetemela.
Wengine ni Magdalena Songora, Hamisi Togwa, Askofu Amos  Muhagachi , Easter Msambazi,  Mussa Kundecha, Respa Miguma na Profesa Costa Mahalu.
Wajumbe kutoka Zanzibar ni Shehe Thabit Nouman Jongo, Suzana Peter Kunambi, Shehe  Nassoro Mohammed Ibrahimu, Fatma Mohammed Hassan, Louis Majaliwa, Yasmin Yusufali na  Thuwein Issa Thuwein.
Wanaharakati  wa masuala ya Kijinsia, haki za binadamu, demokrasia na utawala bora wanadai kumekosekana ushiriki mpana wa uwakilishi wa makundi halisi yaliyoko pembezoni.
Wanadai yamechomekwa  majina ya watu wasiostahili kwenye nafasi za makundi mengine jambo walilodai litasababisha upungufu mkubwa wa uwakilishi.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Lilian Liundi, inadai yameingizwa majina ya wanasiasa kwenye  kundi la NGO na kuwaacha wawakilishi wa asasi za kiraia wakati wanasiasa walikuwa na uwakilishi mkubwa kwenye kundi lao la watu 40.
“Aidha kundi la watu wenye mlengo unaofanana  nalo hatukupewa tafsiri  halisi kuwa ni watu kutoka kundi gani au ni kina nani badala yake wameingia wanasiasa na kulifanya Bunge hili la katiba kuwa na wanasiasa wengi  zaidi ya makundi mengine,” alisema Lilian.
Aliendelea kusema, “Wanaharakati tunahoji nini ilikuwa tafsiri ya watu wenye malengo yanayofanana? Baada ya wanasiasa kuteuliwa kupitia kundi lao la wajumbe 40 hawakutakiwa kuingia tena kupitia kundi hili la pili badala yake wangezingatia  makundi yaliyokuwa yamebaki.”
“Tunajiuliza kwa hali hii ya kujaza wanasiasa kwenye haya makundi ya wananchi tutapata katiba mpya tunayostahili kuwa nayo? Tunadai uwakilishi zaidi wa makundi mengine kwenye hili Bunge,” alisema.
Kwa mujibu wake, wabunge wa sasa hawakuchaguliwa kwa kuzingatia uwiano wa kijinsia na makundi yaliyoko pembezoni. Wanaharakati hao wanadai pia wabunge wamechaguliwa kwa kuzingatia mfumo na ushawishi na itikadi za vyama  vya siasa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye akijibu maswali ya waandishi wa habari jana Dar es Salaam, aliviijia juu  baadhi ya vyama na taasisi zinazolalamikia uteuzi wa wajumbe wa bunge  maalumu la katiba walioteuliwa na Rais Kikwete.
Alisema madai yanayotolewa kuwa bunge hilo limejaa wanachama wengi wa CCM ni ya kupuuzwa. Alisema kwa vyovyote,  hilo lingetokea kutokana na mtaji wa wanachama zaidi ya milioni sita ilio nao.
Alisema hata bunge la kawaida lina wabunge wengi wa CCM hivyo hoja ya kwamba wajumbe wengi wanatoka chama hicho, haina mashiko.
Wiki iliyopita, Rais Jakaya Kikwete alitangaza majina ya wajumbe 201 wa Bunge la Katiba, watakaoshirikiana na wajumbe wengine  ambao ni wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wapatao 357, wajumbe wa Baraza la wawakilishi Zanzibar wapatao 81 na kufanya jumla yote kuwa wajumbe 639.
Kwa mujibu wa sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka namba 81 ya 2013, rais amepewa mamlaka ya kuteua  wajumbe wa Bunge hili kwa kushauriana na rais wa Zanzibar baada ya kupelekewa  mapendekezo ya majina kutoka kwa makundi yote ya wananchi kwa mujibu wa sheria na ndivyo alivyofanya.

No comments: