SHAHIDI AKIRI MAHAKAMANI KUSHIRIKI KUPAKIA TWIGA KWENYE NDEGE...

Shahidi wa 20 katika kesi ya utoroshaji wa wanyama hai aina ya twiga kwenda Arabuni, amedai kushuhudia wanyama hao wakipakiwa katika ndege saa nane usiku.

Shahidi huyo, Robert Nyanda alitoa madai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini hapa, na kuongeza kuwa alimwona mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Kamran Ahmed, siku ya kusafirisha wanyama hao.
Nyanda alidai kuwa mshitakiwa huyo alifuatana na watu wengine ambao kwa pamoja walikwenda na gari dogo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Evetha Mushi mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Simon Kobelo, shahidi huyo ambaye ni mtumishi wa kampuni ya Swissport katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam alisisitiza kumwona mshitakiwa huyo uwanjani hapo.
Aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa huyo akiwa na wenzake, walikuja na gari dogo huku lingine lori aina ya Fuso likiwa na wanyama hao pamoja na timu kubwa ya watu wa kusaidia upakiaji wa wanyama hao kwenye ndege la Shirika la Qatar.
"Nilikuwa Ofisa wa Kampuni ya Swissport na jukumu langu lilikuwa kusimamia, kupakia na kupakua mizigo kutoka kwenye ndege.
"Niliagizwa na bosi wangu, Rosemary Israel kuandaa vifaa vya aina tatu vya kubebea vitu vizito vilivyokuwa katika magari likiwamo lori la Fuso," alidai.
Aliendelea kudai kwamba siku ya tukio, pia alimwona Msimamizi wa Kitengo cha Wanyama uwanjani hapo, bila kumtaja jina, lakini hakutilia shaka kwa kuwa alijua yuko kazini.
"Upakiaji mizigo kwenye ndege ya Qatar ulifanyika saa nane usiku, sisi hatukuwa na jukumu la kukagua, kwa vile ndege haikuwa yetu, tulichotakiwa kufanya ni kusaidia upakiaji mizigo tu, masuala mengine yalikuwa chini ya kampuni ya Equity Aviation," alidai.
Akijibu maswali ya wakili wa utetezi, Edmund Ngemela, aliyetaka kufahamu alipo bosi wa shahidi huyo, Rosemary, shahidi huyo alidai hiyo haikuwa kazi yake.
Aidha, wakili alitaka kufahamu sababu za shahidi huyo, kutokagua nyaraka za mzigo uliokuwa ukipakiwa katika ndege hiyo, shahidi huyo alisisitiza lilikuwa jukumu la kampuni ya Equity, kwani wao waliombwa kutoa vifaa vya kunyanyua vitu vizito tu.
Shahidi wa 21 katika kesi hiyo, Rewald Amani aliyekuwa Meneja Mwongozaji wa Ndege KIA, alithibitisha kutua kwa ndege hiyo Novemba 24, 2010  katika uwanja huo na kuondoka Novemba 26, 2010 ikiwa salama kwenda Doha, Qatar.
Alidai kuwa awali ndege hiyo ilitakiwa kutua uwanjani hapo Novemba 7, 2010, lakini haikufika, kutokana na sababu ambazo hakuzijua hadi  ilipotua Novemba 24 bila   tatizo lolote la kiusalama au kiufundi.
Kesi hiyo imepangwa kuendelea leo, ambapo upande wa mashitaka utaendelea kuleta mashahidi, ambapo washitakiwa ni raia wa Pakistani, Ahmed; Hawa Mang'unyuka, Martin Kimathi na Michael Mrutu, na wote wako nje kwa dhamana.

No comments: