VIBANDA VYA MAMA LISHE BUNGENI DODOMA VYABOMOLEWA...

Bomoabomoa Dodoma.
Siku moja baada ya mama na baba lishe kusogeza chakula cha bei nafuu  karibu na Bunge, vibanda vya huduma hiyo vilivyokuwa vimejengwa pembezoni mwa barabara, vimebomolewa.

Bomoabomoa hiyo inadaiwa kufanywa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) jana alfajiri, kwa kile kilichoelezwa kuwa mama lishe hao hawakuwa na kibali cha ujenzi.
Baada ya kitendo hicho, ambacho baadhi ya mamalishe wanadai kuharibiwa vifaa vilivyokuwemo ndani ya  vibanda, waliandamana hadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ambako kulifanyika kikao.
Akizungumza na mwandishi wetu, mmoja wa waathirika wa bomoabomoa hiyo na Mwenyekiti wa Mama Lishe Mkoa wa Dodoma, Ester Mwansasu alisema katika kikao hicho kilichohusisha Mkuu wa Mkoa, Dk Rehema Nchimbi, Mkuu wa Wilaya na CDA, wameruhusiwa kujenga upya vibanda na kuendelea na huduma.
“Mimi nilifika saa 12 alfajiri nikakuta greda likianza kubomoa. Niliwaomba nitoe vifaa vyangu; lakini kwa wale ambao hawakuwepo, wameharibiwa vifaa mbalimbali zikiwemo sahani,” alisema Mwansasu.
Mwansasu ambaye alikuwa na mafundi, wakianza upya ujenzi wa banda, alisema, “CDA walituambia tuna makosa, lakini sasa wameturuhusu kujenga.”
Awali, kulikuwa na vibanda vipatavyo 10 vilivyojengwa mwishoni mwa wiki katika eneo la wazi, linaloangaliana na lango kuu la Bunge, pembezoni mwa barabara iendayo Dar es Salaam.
Bei ya chakula, hususani wali, ugali na ndizi, kinachoendana na kitoweo cha kuku ambao ni wa kienyeji (robo)  ni Sh 4,000.  Chenye  kitoweo cha nyama ya ng’ombe, bei yake ni Sh 3,000 na upande wa samaki ni Sh 3,500. Kinatolewa kikiwa na mboga za majani, tunda na maharage.
 Chai ya rangi ni Sh 300 na ya maziwa Sh 500. Vile vile wanauza vinywaji baridi na vikali. Bia  inauzwa Sh 2,000, soda Sh 1,000 na maji.
Wamelenga zaidi watumishi, wageni na hata wabunge wa Bunge Maalumu ambao kwa mujibu wa mama lishe hao, wengi wameonesha kupendelea chakula chao ambacho ni cha asili zaidi tofauti na vinavyopatikana kwenye hoteli kubwa za kisasa.

No comments: