MJI WA BAGAMOYO KUWA JIJI LA VIWANDA NA BIASHARA...

Moja ya mitaa ya mji wa Bagamoyo.
Uendelezaji wa maeneo maalumu ya uwekezaji katika mji wa Bagamoyo ukikamilika, utasaidia mji huo kuwa Jiji kubwa la viwanda na biashara na kuchangia katika shughuli za maendeleo ya nchi.

Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Huduma wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu ya Uwekezaji (EPZA), Zawadia Nanyaro, alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na ujumbe wa wafanyabiashara  kutoka mji wa Vallejo uliopo Jimbo la California nchini Marekani.
Wafanyabiashara hao, walifanya ziara kwenda kujionea fursa mbalimbali za kibiashara katika eneo hilo ambalo linatarajiwa   kuwa wa viwanda na biashara.
“Serikali imetenga eneo la hekari 22,000 sawa na hekta 9,000 katika eneo hili maalumu la uwekezaji hapa Bagamoyo, na tunahamasisha wawekezaji wakiwemo wa mji wa Vallejo kuja kuwekeza hapa,” alielezea ujumbe huo ambao umeongozwa na Meya wa Vallejo, Osby Davis.
Zawadia alisema kwa sasa Serikali inayo mipango ya kujenga miundombinu mbalimbali kwa kushirikiana na sekta binafsi, hivyo wafanyabiashara hawanabudi kuchangamkia fursa hiyo kwa kuanzisha viwanda na biashara na huduma mbalimbali.
“ Mji wa Bagamoyo kutokana na kuwa eneo maalumu la uwekezaji, kutajengwa Bandari kubwa ya kisasa kupita zote nchini ili kuunganisha na maeneo mengine ya nchi na nje ya nchi,” alisema Mkurugenzi huyo na kuongeza kuwa Bagamoyo itakuwa  kiungo kikubwa kwa biashara nchini.
Mbali na bandari, Zawadia alisema kuna mradi  mwingine  wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa na reli itakayounganishwa na Reli ya Kati na Tazara na miundombinu yote hiyo, inalenga kuweka mazingira bora ya kibiashara na uwekezaji.
Ugeni huo wa wafanyabiashara hao kutoka mji wa Vallejo, walitembelea maeneo hayo ya uwekezaji, likiwemo eneo la hekta 300 la Kamal Industrial Estate, linalomilikiwa na mtu binafsi.
“ Ujumbe wa wafanyabiashara hawa wengi wao wamefurahishwa na Serikali ya Tanzania kutenga maeneo  hayo kwa ajili ya viwanda na biashara,” aliongeza mkurugenzi huyo na kuongeza kuwa  wako tayari kuja nchini kuitumia fursa waliyoiona Bagamoyo kwa ajili ya maendeleo ya nchi hizi mbili.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Weusi wa Mji wa Vallejo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Carl Davis Jr  alisema wao wanahitaji kufanya biashara  katika mji  wa Bagamoyo kwa faida ya miji hiyo miwili.

No comments: