Simu za mkononi. |
Hatua hiyo inatokana na uzinduzi wa Mtambo Maalumu wa Usimamizi na Uhakiki wa Mawasiliano ya Simu (TTMS) Dar es Salaam jana.
Mtambo huo baada ya kurekodi kila senti inayoingia katika kampuni hizo, kutokana na mawasiliano yanayofanyika ndani na nje ya nchi, utaiwezesha Serikali kupata mgawo wake wa kodi kupitia sekta ya mawasiliano.
Akizindua mtambo huo, Rais Jakaya Kikwete alisema baada ya kufungwa kwa mtambo huo, Serikali inatarajia angalau kupata takribani Sh bilioni 20 kila mwaka kupitia sekta ya mawasiliano.
“Najua watu wanafahamu hatua kubwa tuliyofikia katika suala zima la kukuza mfumo wa mawasiliano kupitia mikongo hii, lakini maswali mengi ya Watanzania yalikuwa ni kweli Serikali inalipwa inavyostahili na kampuni hizi za simu na zile zinazotoa huduma za mawasiliano?” Alisema Rais Kikwete.
Alikiri kuwa kabla ya kufungwa kwa mtambo huo, Serikali ilikuwa ikipata kodi kwa kutegemea taarifa za kampuni husika, jambo ambalo kwa sasa halitaruhusiwa kwa kuwa mtambo huo utarekodi idadi ya simu zilizopigwa, muda uliotumika na mapato yaliyopatikana kupitia simu hizo.
Alisema kufungwa kwa mtambo huo, kutaleta mafanikio kutoka katika mikongo miwili ya mawasiliano iliyojengwa na Serikali, ambayo imeunganishwa kwenye mtambo mkubwa wa mawasiliano duniani.
“Kama kuna uamuzi mzuri ambao Serikali imewahi kuufanya ni huu wa kufunga mikongo hii ya mawasiliano, na hatua ziko mbioni kuhakikisha kila wilaya katika nchi hii inafikiwa na mkongo huu,” alisema.
Alifafanua, kwamba tangu kufungwa kwa mikongo hiyo, mafanikio makubwa yameanza kuonekana ikiwamo kupungua gharama za simu kwa takribani asimilia 57.
Aidha, gharama za intaneti zimepungua kwa asilimia 75 huku gharama za uwekezaji nazo zikipungua.
Rais Kikwete alisema kabla ya mkongo wa mawasiliano, Tanzania ilikuwa inatumia mfumo wa satelaiti ambao ulikuwa na gharama kubwa kwa mwaka na kusababisha huduma zote za mawasiliano kuwa na gharama kubwa.
“Ili kuthibitisha kuwa sasa mfumo huu wa mawasiliano umeleta unafuu, hata idadi ya watumiaji wa huduma za simu kama laini wameongezeka kutoka milioni 2.3 mwaka 2009 hadi milioni 28 Desemba mwaka jana, kwa lugha nyingine sasa Tanzania ‘tunatesa’ katika mawasiliano,” alisema.
Alisema mkakati wa Serikali ni kuhakikisha mikongo hiyo itakapokamilika nchi nzima, kila ofisi ya Serikali itatumia mfumo wa eletroniki kuhudumia wananchi, hali ambayo pamoja na kurahisisha utoaji huduma, lakini pia itaondoa vitendo vya urasimu, rushwa na ufisadi.
“Tunataka watu wasiende ofisini kupatiwa huduma na mtu, bali watumie njia ya eletroniki kupata huduma hiyo, kila sekta itatumia mfumo wa Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuanzia elimu, afya hadi utalii,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alihamasisha Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kutengeneza Sheria ya Usalama wa Mawasiliano ili kuilinda Tanzania na matumizi mabaya ya mawasiliano.
“Hakuna uhuru usio na mipaka, wapo watu wanadhani uhuru wa habari ni kufanya kila kitu, la hasha, hakuna nchi inayoweka siri zake hadharani… haipo na haitatokea, ndiyo maana hata kwenye nchi zilizoendelea kuna watu wanachukuliwa hatua kwa kuingilia uhuru huo, sasa na sisi tujiandae,” alisisitiza.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma alisema mtambo huo wa TTMS lengo lake ni kuhakikisha mgawanyo wa huduma za mawasiliano unapatikana kwa uhakika, unaweka uwazi na uwajibikaji, kuzuia uwezo wa simu zinazopigwa na kampuni zisizosajiliwa na kupunguza wizi wa simu.
“Kabla ya mtambo huu, Serikali haikuwa na uwezo wa kujua wingi wa dakika za simu zinazopigwa nchini na kubaini wanaotumia mitandao ya wizi ya kimataifa bila leseni na hivyo kuikosesha Serikali fedha na watoa huduma zenye leseni mapato mazuri,” alisema.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, alisema Serikali imeandaa kanuni za matumizi ya mtambo huo, ambazo zinabainisha kuwa kampuni za simu za nje zitalipa kampuni za ndani senti 25 za dola ya Marekani kwa kila dakika moja ya simu inayopigwa, wakati awali zilikuwa zikilipa senti nane tu.
“Sheria pia inatamka kuwa katika mgawanyo huo wa senti 25, Serikali itapata senti saba kwa kila dakika, watoa huduma senti 13 na senti tano zitumike kwa ajili ya kuendesha mitambo. Lakini pia TCRA tayari imeshailipa Sh bilioni 1.6 za Januari na Februari,” alisema.
No comments:
Post a Comment