MEMBE ATAKA MGOMBEA URAIS CCM 2015 ATANGAZWE DESEMBA MWAKA HUU...

Bernard Membe.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ametema cheche akitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuruhusu mgombea wa urais mwakani, kujulikana ifikapo Desemba, lakini akawashushia lawama waandishi wa habari nchini.

Alitoa kauli hizo na nyingine wakati akihojiwa na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya CCM, White House mjini hapa, mara tu baada ya kutoka kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ya chama hicho tawala, akihusishwa na mbio za urais za mwaka 2015.
Membe na wenzake watano wanatuhumiwa kuanza mapema kampeni za kusaka urais kupitia chama hicho, kinyume cha taratibu na mwongozo wa chama hicho tawala nchini.
Wengine waliohojiwa kuanzia Jumatano wiki hii ni pamoja na mawaziri wakuu wastaafu Edward Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Frederick Sumaye; aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Wamo pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ambao wote wanatajwa kuwa katika mbio za urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Membe aliyefika White House saa 3.15 na kwenda moja kwa moja kwenye ukumbi wa mahojiano, tofauti na wenzake, alikiri kwamba aliitwa na Kamati ya Maadili na kuhojiwa kuhusu mbio za urais 2015.
"Nazungumza nanyi kwa sababu mbili; moja katika wiki moja iliyopita nimepata meseji nyingi sana na watu wakiuliza kulikoni kuitwa Dodoma. Pili, ni kweli ninatoka kuhojiwa katika Kamati ya Maadili, wote tuliitwa kuhojiwa," Membe aliwaambia waandishi wa habari, huku akionekana mwenye furaha.
Alisema Kamati ya Maadili inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, imefanya kazi nzuri sana na kwamba ameulizwa maswali mazito na magumu yanayohusu uvunjaji wa maadili ya chama hicho.
"Kamati yetu ya Maadili imejipanga vizuri sana, na msidanganyike, wanauliza maswali mazito, maswali magumu ama unayoyafanya wewe au mashabiki. Lakini yote yanalenga katika kukiimarisha chama, katika kuimarisha ushindi kwa mwaka 2015 na kuimarisha maadili. Yale ni mambo mazito," alisema Membe na kuongeza:
"Makubwa matatu ambayo Kamati ya Maadili inayauliza, kubwa kabisa ni uzukaji ghafla wa makundi makubwa ambayo yanazaliwa kila watu wanapodhani fulani anafaa kuwa kiongozi. Tunafanyaje kukifanya chama chetu kiwe na kundi moja litakalokwenda mwakani kwenye ushindi.
"Lakini la pili pia ni suala zima la fedha kama msingi wa ushindi. Inatokeaje watu wanatumia mamilioni, mabilioni ya pesa katika kujinufaisha na kujiandaa kwenda kwenye uchaguzi.
"Lakini tatu ni media, ninyi waandishi wa habari, mnalishwa vitu gani, mmemeza nini vichwani mwenu mpaka muone kinachosemwa na fulani ni cha maana hadi kitoke katika magazeti na kingine kikisemwa na fulani, hata kikiwa cha maana kisitoke kwenye magazeti, mmemeza mdudu gani," alihoji Membe.
Membe alisema kutokana na hayo, majibu yake yalikuwa ni kwamba Kamati ya Maadili iendelee kufanya kazi hiyo, na bado kuna watu wataitwa, lengo likiwa ni kuwa na chama imara, kitakachokwenda mwakani kuvishinda vyama vingine, ambavyo alidai baadhi vimeanza kufa.
"Lakini la pili, nadhani sasa itafika mahala kwamba chama sasa itabidi kichague kiongozi au nani wanafaa kuwa viongozi, ili kufanyike midahalo kwa mfano, ili wananchi wajue tunapokwenda mwaka 2015, candidate wa Chama Cha Mapinduzi ni nani? Lazima tufike hapo.
"Tukiacha kila mwanachama aombe, kila binadamu anayejiona anavaa nguo ya kijani na ana hela aombe, tutakiangusha chama chetu. Na kwa hiyo mwelekeo ni wa kushauri, nadhani mwelekeo sasa ni wa kushauri.
"Na watu kama sisi tunashauri, ni vizuri sasa chama kikajipanga na kiwe na candidate, yaani kiwe na watu ambao haraka haraka wapitishwe ili inapofika kwa mfano Desemba mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi kinajua nani anachukua bendera ya chama chetu mwakani. Ili chama chetu kiwe kimoja, kisimegukemeguke," alisema Membe.
Membe alisema jingine ni kwamba iwe ni mwiko kwa mtu yeyote ndani ya chama kutumia fedha kama nguzo ya ushindi wake, akisema uongozi wa Taifa hauwezi kununuliwa na fedha.
"Na mimi nawaambia waandishi wa habari, chezeni mtaona, hatuwezi kuruhusu uongozi wa nchi hii au kiongozi wa juu anunue kama biashara ya njugu dukani. Mkiacha hilo linaendelea, ninyi waandishi wa habari ni sehemu ya kulaumiwa duniani.
"Hamuwezi kuwa na kiongozi anayenunua uongozi kwa njia yoyote ile, iwe ya fedha au jambo jingine lolote lile. Na hili ndio Kamati ya Maadili inakemea na mimi najiunga nao, lazima kukemea. Huwezi kununua uongozi wa Taifa kwa namna nyingine yoyote ile. Na tutakuwa watu wa ajabu Watanzania kama tutaanza kufanya biashara ya uongozi wa kitaifa," alieleza Membe.
Alilitaja suala la tatu alilolitolea ushauri ni uongozi wa CCM kwamba ndio chama kinachotegemewa duniani, akitaka kuwapo kwa mwongozo unapofika wakati wa uchaguzi.
"La tatu na la mwisho nililotolea ushauri, na ambalo nataka niwaambie na waandishi wa habari, ni uongozi. Uongozi wa chama chetu, cha Mapinduzi, ndio uongozi unaotegemewa duniani, chama hiki kimefanya mambo mengi mno, na kwa hiyo lazima kuwe na mwongozo.
"Mwongozo rasmi unaotakiwa kufuatwa na wanaCCM kuanzia ngazi ya matawi kuja mpaka huku juu kwamba unapofika wakati wa uongozi, utumie hatua zipi, uzingatie nini ili usivunje na kukiuka maadili. Mashabiki nao wafanye nini ili wasikiuke maadili, ili tuweze kwenda pamoja.
"Kwa hiyo ni Kamati ya Maadili inayouliza maswali magumu sana, sana sana, kwa watu wanaosemwa kwamba wanaweza kuwa viongozi, lakini Kamati ya Maadili inayosikiliza ushauri, lakini ni Kamati ya Maadili inayotaka chama hiki kiende katika uchaguzi mwakani kikiwa strong yaani cha nguvu, united yaani chama kimoja na kikiwa na uhakika wa ushindi.
"Na mimi nasema wazi kwa vyovyote vile tukizingatia hayo, Chama Cha Mapinduzi kitapeta miaka 60 ijayo, hakuna atakayeingia hapo."
Aliwageukia tena waandishi wa habari, akisema lazima wapime, waandike ya wote wote, na wasibague.
"Lakini narudia, waandishi wa habari lazima muwe objective, waandishi wa habari lazima mpime, waandishi wa habari ndio mnaoweza kuamua direction ziende wapi, lazima muandike ya watu wote wanaozungumza bila kuchagua mambo fulani ya fulani tuyaandike yote, na mwingine akisema hata akisema nini tusiandike yote, mtaiua nchi, mtajiua ninyi wenyewe, objectivity ya vyombo vya habari ni kuandika habari taarifa zote au habari zote kwa manufaa ya Watanzania wote, msiwanyime Watanzania nafasi ya kuyazungumza.
"Kwa mfano haya niliyoyazungumza, kuna watu mtakwenda kuyachuja, Membe kazungumza hiki, tusiseme kwa sababu tutamuudhi fulani, hiki kisiandikwe tutamuudhi fulani. Halafu zitabaki tv tu," alisema Membe na kukataa kuulizwa maswali kwani alikwishaulizwa ndani.
Baada ya kuhojiwa na Kamati hiyo ya Maadili, Lowassa alisema: "Sijibu lawama, kwa vile hakikuwa kikao cha lawama, kilikuwa cha mazungumzo na ndani ya kikao,
hakukuzungumzwa makundi."
Sumaye kwa upande wake alitania akisema alikuwa amekwenda kunywa chai, lakini akawataka waandishi wasubiri wakubwa (uongozi wa CCM) wawape taarifa.
Ngeleja alisema kwamba hajatangaza nia ya kugombea urais, lakini akaongeza: "CCM ni chama chenye Katiba na kanuni zake na wakati wa kutangaza nia ndani ya CCM bado haujafika."
January kwa upande wake, alisema aliitwa katika kikao hicho kwa maoni na ushauri, lakini akaongeza kuwa kuna faida kubwa ya kujulikana mapema (wagombea urais) kuliko mwishoni kwani watu wanapata fursa ya kukujadili na kutoa mawazo yao kama unafaa kuwa kiongozi au la.
Mwanasiasa mkongwe, Wassira alisema hajawahi kutangaza nia ya kugombea urais, lakini si dhambi mtu kutamani kuwa Rais wa Nchi.
"Sio dhambi kutamani kuwa Rais, kwani nafasi ni moja kwa Watanzania wote na kila mtu anayo haki ya kuomba nafasi hiyo, ila utaratibu ufuatwe," alisema mbunge huyo wa Bunda mkoani Mara.

No comments: