BUNGE LA KATIBA KUANZA NA MASWALI YA HAKI ZA RAIA WA TANGANYIKA...

Mwalimu Nyerere akisherehekea na wananchi wengine Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.
Wakati wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakijikusanya mjini Dodoma leo, kuanza safari ya siku 70 mpaka 90 ya kuwapatia Watanzania Katiba mpya, wasomi zaidi ya 100 wanakutana Dar es Salaam, kujibu maswali magumu yanayotakiwa kupatiwa ufumbuzi wa mwisho na Bunge hilo.

Taasisi ya Utafiti ya Umoja wa Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki na Kusini (ESAURP), imekusanya wasomi hao kutoka nchi mbalimbali duniani na vyuo karibu 36 nchini kwa siku mbili, kutafuta ipi inapaswa kuwa Katiba bora kwa Watanzania.
Mkutano huo wa wasomi, utaongozwa na maswali ambayo majibu yake yanatarajiwa kutoa misingi ya hoja, zitakazojadiliwa na zitahusu pamoja na mambo mengine haki za raia, zinazotajwa kutishia uwepo wa Muungano.
Akitumia rasimu ya pili ya Katiba mpya kama muongozo,  kuchokoza kitakachojadiliwa leo, mmoja wa watoa mada, Profesa Bonaventura Rutinwa wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alionya jana kuwa haki za Watanganyika, zitawabagua Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara.
Alifafanua kuwa ingawa Rasimu ya Pili ya Katiba mpya, katika Sura ya Tano inazungumzia haki za raia wa Jamhuri ya Muungano, lakini suala hilo litaamsha kero kubwa zaidi ya zilizopo zinazoweza kuvunja Muungano.
Kwa mujibu wa Profesa Rutinwa, aliyezungumza katika ofisi za Esaurp,  jijini Dar es Salaam jana, kosa la kwanza lililopo katika Rasimu ya Pili ya Katiba mpya, ni kutojipa nafasi ya kuwa Katiba Kuu kuliko Katiba ya Zanzibar na itakayokuwa Katiba ya Tanganyika.
"Sasa kwa kuwa Zanzibar tayari ina Katiba yake, inayotoa na kulinda haki za kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa Wazanzibari, huhitaji nguvu za kinabii kubashiri kuwa Katiba ya Tanganyika ikija itatoa na kulinda haki za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa Watanganyika.
"Hii ikitokea, itasababisha wananchi kutoka Tanganyika wanaoishi Zanzibar na Wazanzibari wanaoishi Tanganyika kushindwa kudai haki zao za uraia kisheria," alionya Profesa Rutinwa.
Alihitimisha kuwa katika mazingira hayo, mfumo unaopendekezwa wa serikali tatu, utafifisha mshikamano wa Watanzania na serikali za nchi washirika, na katika hali mbaya zaidi, utazalisha kero mpya za Muungano zitakazokuwa na nguvu ya kuvunja Muungano.
"Kunahitajika umakini katika hili, la sivyo historia imeshaonesha kuwa ni rahisi kuvunja Taifa kuliko kulikusanya na kulijenga upya," alionya Profesa Rutinwa, ambaye leo atatoa hoja yake na kujadiliwa na wasomi wenzake.
Katika sehemu ya ushauri wake, Profesa Rutinwa alipendekeza pamoja na mambo mengine, utatuzi wa kero za Muungano, ufanyike pamoja na kulitazama wazo la kuwa na serikali moja, ambayo kwa mujibu wa ushauri huo, serikali hiyo ndiyo lengo la siku nyingi la Muungano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Hata hivyo, mmoja wa watoa mada wa leo, Hugh Mason ambaye ni Kaimu Meya wa Mji wa Portsmouth, Scotland, akizungumza jana alisema hashangai Zanzibar kutaka uhuru zaidi au kujitoa katika Muungano.
Kwa mujibu wa Mason, Zanzibar ni eneo ambalo lina historia yake tofauti na eneo lingine ndani ya Tanzania na wakazi wake wanajisikia vizuri kwa historia yao na utamaduni wao, hivyo ni vyema hilo liheshimiwe katika Katiba mpya.
Alisema hata Uingereza, eneo la Scotland lina utawala wake unaojitegemea kama ilivyo Zanzibar, ambayo ina utawala wake unaojitegemea ndani ya Tanzania.
Mason ambaye ni Mscotishi na anajivunia kuwa Mscotishi, anasema tayari Scotland inatarajiwa kupiga kura ya kujitoa Uingereza na kuwa na uhuru kamili mwaka huu, hivyo hashangai hoja za Zanzibar kujikita katika Muungano wakati huu Tanzania inapotafuta Katiba mpya.  
"Jambo muhimu ni namna gani Zanzibar ambayo ni tofauti na eneo lingine Tanzania itatambulika katika Katiba mpya.
"Zanzibar haiwezi kujitofautisha kiuchumi na Tanzania; uchumi wake wa utalii umeungana kwa sehemu kubwa na wa Tanzania na uchumi wa bidhaa za viungo, hautabiriki. Zanzibar pia haiwezi kujitenga na Tanzania katika lugha," alisema Mason, ambaye anaamini Scotland haitajitoa katika Muungano wake wa Uingereza.
Mscotishi huyo anaamini namna Zanzibar itakavyotambulika katika Katiba ya Tanzania, itakuwa tofauti na katika nchi nyingine, lakini anasema haiondoi umuhimu wa kujifunza namna maeneo kama Zanzibar yanavyotambulika katika nchi nyingine duniani.
Mason alitoa mfano wa Iraki, ambako watu wa kabila la Kurdi, ambalo ni la watu wachache, lakini kama ilivyo kwa Wazanzibari, wana historia na utamaduni tofauti na watu wengine wa nchi hiyo.
Kutokana na tofauti hizo, maeneo ya Wakurdi yamekuwa yakitambuliwa kwa kiasi fulani Iraki.
Lakini, Uturuki maeneo ya watu hao hayatambuliwi, licha ya kuwa na historia na utamaduni tofauti na Waturuki wengine.
Alisema utofauti huo umekuwa ukisababisha hali ya kutoridhika kwa Wakurdi katika nchi hizo.
Kwa mujibu wa Mason, mwaka 1997 nchini Uingereza eneo la Scotland lenye mfumo unaojitegemea wa sheria, elimu na kwa kiasi mfumo wa fedha, lilitambuliwa ndani ya Serikali moja.
Utambulisho huo kwa mujibu wa Mason, ulifanyika kwa wabunge wa Bunge la Uingereza wanaotoka Scotland, kuruhusiwa kuunda Kamati yao ambayo hukutana na kutunga sheria katika mambo yanayohusu Scotland.
"Kinadharia maoni ya Kamati hiyo kuhusu sheria za mambo yanayohusu Scotland, yangeweza kukataliwa na Bunge lenye wabunge wengi kutoka maeneo mengine ya Uingereza, lakini hali hiyo haijatokea," alisema Mason.
Mfano mwingine wa eneo lenye historia na utawala tofauti ndani ya nchi moja ni visiwa vya Faroe, ambavyo ni sehemu ya Denmark.
Kwa mujibu wa Mason, watu wa visiwa hivyo wana utawala unaojitegemea katika mambo ya visiwa hivyo na wana wabunge katika Bunge la Denmark.
Mscotishi huyo alitoa mfano pia wa Hong Kong na Macau nchini China, ambako kuna utawala na mipaka inayojitegemea, isipokuwa kwa masuala yanayohusu Mambo ya Nje na Ulinzi
Maeneo hayo na China yana utawala unaojitegemea kama ilivyo Zanzibar ndani ya Tanzania, lakini tofauti yao hayana mbunge katika Bunge la China.
Kwa mujibu Mason, kama Katiba itakuwa ya serikali tatu, mamlaka ya Bunge lazima yapunguzwe, lakini lazima  kutatokea mgongano kati ya kiongozi wa Muungano na viongozi wa serikali za nchi washirika.
"Katika mazingira ya Tanzania, ambako kuna nchi mshirika mmoja ana ukubwa, madaraka ya kiongozi wa Bara, yatakuwa yakiashiria hatari ya wazi kwa kiongozi wa shirikisho," alisema Mason ambaye leo atatoa hoja na kujadiliwa na wasomi.

No comments: