MBUNGE WA CHADEMA ATANGAZA KUWANIA URAIS 2015, MUMEWE PIA ATAJWA KUGOMBEA...

Rose Kamili na Dk Willibrod Slaa.
Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Manyara kupitia Chadema, Rose Kamili ametangaza kugombea urais katika uchaguzi mkuu mwakani.

Alitangaza kuwania nafasi hiyo jana mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii iliyokuwa ikitembelea shughuli za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, mjini hapa.
Wakiwa katika chuo cha maendeleo ya jamii Ruaha kilichoko Ipogolo mjini hapa, Kamili alisema: "Naitwa Rose Kamili, mimi ni mbunge wa viti maalumu wa mkoa wa Manyara kupitia Chadema na napenda kutumia fursa hii kutangaza rasmi, kwamba nitawania urais katika Uchaguzi Mkuu mwakani."
Baadhi wabunge wenzake wa Kamati hiyo walipiga makofi huku wageni wengine waalikwa katika ziara ya wabunge hao chuoni hapo wakicheka.
Baadaya kutangaza azma hiyo aliketi huku akisema anataka kudhihirisha usemi kuwa 'wanawake wanaweza'.
Katika hali ya utani, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Said Mtanda (CCM) alisema: "Hata kama ukikosa, huenda ukawa 'first lady (mke wa Rais)' endapo mumeo, Dk Wilbrod Slaa, atapata nafasi hiyo."  Kauli iliyosababisha kicheko kutoka kwa wajumbe wengine.
Akipongeza uamuzi wa Kamili, Mbunge wa Mtera,  Livingstone Lusinde (CCM), alisema Rose Kamili ameonesha ujasiri mkubwa kutangaza nia hiyo.
"Ni ujasiri hasa katika kipindi hiki ambacho ndugu zetu Chadema wamemvua uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wao, Zitto Kabwe wakimtuhumu kwa makosa mbalimbali," alisema.
Alitaja moja ya sababu za Zitto kupata adhabu hiyo ni kutangaza kugombea urais kupitia chama hicho, wakati kuna kila dalili inayoonesha kwamba Dk Slaa atagombea urais kwa mara nyingine katika uchaguzi ujao.
"Najua amefanya ujasiri kutangaza mbele ya wajumbe wa Kamati, wanachuo na watumishi wachuo hiki, lakini nina wasiwasi kama yaliyompata Zitto yanaweza yasimkute," alisema.
Akitaka kunukuliwa kama Mbunge wa Kondoa Kusini, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia alisema ameshitushwa na uamuzi wa Kamili.
"Nachoweza kusema hiyo ni demokrasia, lakini kama mbunge mwenzake imenishitusha sana, kwa sababu katika mazingira ya kawaida, inahitaji ujasiri ndani ya Chadema kutangaza kugombea urais," alisema.
"Kila mtu anajua kwamba Kamili amekuwa na uhusiano ya mume na mke na Dk Slaa; anavyotangaza kuwania nafasi ambayo kuna kila dalili kwamba mumewe ataiwania haogopi kufukuzwa chama?" Alihoji Nkamia.
Julai mwaka juzi, Kamili anayejulikana kuwa mke wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Slaa, alifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akiiomba isimamishe ndoa ya kiongozi huyo na mchumba wake Josephine Mushumbusi iliyokuwa ifungwe Julai 21, mwaka juzi.
Katika kesi hiyo, Kamili aliiomba Mahakama imwamuru pia Dk Slaa amlipe Sh milioni 50 za fidia ya matumizi anayofanya pasipo matunzo ya mumewe huyo.
Kwa kupitia wakili wake, Joseph Thadayo, Kamili aliiomba Mahamaka imwamuru Mushumbusi amlipe Sh milioni 500 za fidia ya maumivu aliyopata kutokana na kitendo chake cha kuingilia ndoa yao.
Katika hati hiyo ya madai, Mbunge huyo alidai kuwa ndoa inayotarajiwa kufungwa kati ya Dk Slaa na Mushumbusi ni batili kwa sababu kuna ndoa nyingine halali na inayoendelea kuishi kati ya Dk Slaa na Kamili iliyofungwa mwaka 1985.
Kamili anadaiwa pia kuwasilisha hati hiyo ya mashitaka kwa Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo akimweleza Askofu huyo wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam kuwa moja yaParokia za Dar es Salaam zilikuwa na taarifa ya ndoa hiyo.
Nakala ya madai hayo zimeelezwa kuwasilishwa kwa Msajili wa Mahakama Kuu, Msajili waNdoa na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mbulu.
Oktoba mwaka jana, Mahakama hiyo ilitupilia mbali kwa gharama pingamizi la Dk Slaa lililokuwa likiiomba ifute kesi hiyo ya madai namba 4 ya mwaka 2012 iliyofunguliwa na Kamili.

No comments: