WENGER AFUNGUKA DAKIKA ZA MAJERUHI, KIUNGO WA SWEDEN ATUA RASMI ARSENAL...

Kim Kallstrom.
Klabu ya soka ya Arsenal ya England usiku wa kuamkia leo imefanikiwa kumsajili kiungo wa Sweden, Kim Kallstrom kutoka klabu ya Spartak Moscow ya Urusi.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31 alisafiri hadi London akitokea Abu Dhabi, ambako alikuwa akijifua na klabu yake hiyo ya Urusi wakati wa mapumziko ya majira ya baridi, kukamilisha uhamisho wake wa mkopo hadi mwisho wa msimu, ambao utasaidia kuimarisha kikosi cha Arsenal kilichodhoofika kufuatia kuumia kwa Aaron Ramsey.
Kallstrom alianza safari yake ya soka akiwa na Djurgarden kabla ya kujiunga na klabu ya Rennes ya Ufaransa na kisha kuhamia Lyon mwaka 2006, ambako aliiwezesha kutwaa Ubingwa wa Ligue 1 na Kombe la Ufaransa, mataji yote hayo mara mbili.
Akiwa amecheza kwenye Kombe la Dunia mwaka 2006 na pia Klabu Bingwa ya Ulaya mara tatu, alielekea Spartak katika majira ya joto mwaka 2012 na kucheza mara 10 msimu huu kabla ya mapumziko ya majira ya baridi.
Wakati wa kutangaza kumnyakua kiungo huyo, Arsene Wenger alisema: "Kim Kallstrom ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa mno. Ni kiungo mwenye ubora uliothibitika katika klabu zote na kiwango cha kimataifa. Tunamkaribisha Kim klabuni Arsenal."
Kiungo huyo akielezea furaha yake kwa kujiunga na Arsenal, anasisitiza kwamba atafanya kila awezalo kusaidia kuongeza makali ya risasi za Washika Bunduki hao kuweza kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya England.

No comments: