MAMALISHE 'WAWAOKOA' WAJUMBE BUNGE LA KATIBA DODOMA...

Mamalishe akiwa kazini mjini Dodoma.
Wakati wabunge wakisubiri nyongeza ya posho kwa madai maisha Dodoma ni ghali, huduma ya chakula cha bei nafuu, imesogezwa karibu nao.

Hivi sasa vibanda vya mama na baba lishe, vimejengwa pembeni mwa barabara kwa ajili ya kuhudumia wajumbe na wafanyakazi wanaohudumia Bunge hilo mjini hapa.
Vibanda vipatavyo 10 vimejengwa katika eneo la wazi, linaloangaliana na lango kuu la Bunge, pembeni mwa barabara iendayo Dar es Salaam.
Baadhi ya vibanda vilianza kutoa huduma ya chakula na vinywaji tangu jana, huku wamiliki na wahudumu wakisema wateja wengi wameeleza kuvutiwa navyo, kutokana na chakula kinachoendana na mazingira ya kitanzania.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Mwenyekiti wa Mama Lishe Mkoa wa Dodoma ambaye pia anamiliki kibanda kimojawapo, Ester Mwansasu alisema bei yao inaanzia Sh 3,000 hadi Sh 4,000 kwa sahani kwa kuzingatia kitoweo.
Mwansasu alisema chakula chochote; hususan wali, ugali na ndizi, kinachoendana na kitoweo cha kuku wa kienyeji (robo), bei ni Sh 4,000.
Kwa sahani ya chakula chenye kitoweo cha nyama ya ng'ombe, bei ni Sh 3,000 na upande wa samaki ni Sh 3,500 na kinatolewa kikiwa na mboga za majani, tunda na maharage.
Chipsi mayai ni Sh 2,000, chai ya rangi ni Sh 300 kikombe na ya maziwa ni Sh 500. Supu ya kuku ni Sh 3,000, ya nyama ya ng'ombe Sh 2,000 na supu ya kongoro Sh 1,500. Wanauza pia vinywaji baridi na vikali. Bia inauzwa Sh 2,000, soda Sh 1,000 na maji.
"Wakati wa Bunge la kawaida, kulikuwa na banda moja lakini sasa tumeona waheshimiwa wengi wa kawaida, ambao hawajazoea hoteli kubwa zenye bei kubwa wanafika hapa kupata huduma zetu," alisema.
Aidha, alisema: "Kuna baadhi ya waheshimiwa wanapenda vyakula vya kinyumbani kama vile mlenda, kisamvu na jana baadhi walikuja leo (jana) wamekuja wachache hasa madereva, kwa sababu hakuna kikao."
Mwansasu alisema waliomba kibali Halmashauri ya Manispaa cha kuendesha shughuli hiyo karibu na Bunge wakakubaliwa.
Ingawa hadi jana kazi ya ujenzi wa vibanda ilikuwa ikiendelea, Mwansasu alisema Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), iliamuru waondoe vibanda hivyo.
Hata hivyo, alisema walikuwa kwenye mazungumzo na uongozi wa Sekondari ya Dodoma inayomiliki eneo hilo, ili kuomba kuendesha biashara  katika eneo hilo linalotumiwa pia kama sehemu ya maegesho kwa wajumbe na watumishi wengine ndani ya Bunge.
"Tunaendelea na mazungumzo na Kamati ya Shule pamoja na uongozi. Hata kama tumekubaliwa na Manispaa, lakini shule ndiye mmiliki," alisema kiongozi huyo wa mama lishe.
Kiongozi huyo wa mama lishe alisema katika Bunge la kawaida, kulikuwa na banda lililokuwa likitumika zaidi kuandaa chakula kwa ajili ya madereva tofauti na sasa ambako mabanda ni mengi.
Pia alisema Bunge Maalumu lilipoanza, wapo wengine walikwenda kujenga mabanda katika eneo la nyumba za NHC ambako wamekodishwa Sh 10,000 kwa siku.
"NHC kuna wapishi wanalipa Sh 10,000 kwa siku... sisi tumeshindwa hiyo bei," alisema.
Akieleza namna wateja walivyoitika, mama huyo alisema ingawa juzi kikao kiliahirishwa mapema, aliuza chakula chote ndani banda lake lenye uwezo wa kuchukua watu zaidi ya 20 kwa pamoja.
Vivyo hivyo kwa upande wa vinywaji, alisema waliuza kwa kiwango kikubwa. Mwandishi wa habari hizi, alishuhudia baadhi ya wajumbe wakipata mlo katika maeneo hayo, huku Mwansasu akisisitiza: "Tunashukuru mwitikio ni mzuri. Tuna
imani kesho hali itakuwa nzuri zaidi".
Wakati mama na baba lishe hao wakitumia fursa ya Bunge Maalumu kujiongeza kipato, kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu malalamiko ya baadhi ya wajumbe kwamba posho ya Sh 300,000 kwa siku haitoshelezi matumizi mjini hapa.
Wajumbe hao akiwamo Richard Ndassa wa Sumve, waliomba Rais aongeze posho, wakishikilia kwamba gharama mjini hapa, zikiwamo za chakula, ziko juu kiasi cha kutotoshelezwa na Sh 80,000 za kujikimu na Sh 220,000 za posho maalumu.
Hatma ya maombi hayo ya nyongeza ya posho, iko mikononi mwa Rais Jakaya Kikwete aliyefikishiwa kilio hicho na Kamati iliyoundwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho kushughulikia suala hilo.
Wajumbe wa Kamati hiyo ni William Lukuvi, Freeman Mbowe, Paul Kimiti, Jenista Mhagama, Mohamed Aboud Mohamed, Asha Bakari Makame na Kificho mwenyewe.

No comments: