Kikao cha madiwani Shinyanga. |
Jana madiwani wawili wa Chadema katika Manispaa ya Shinyanga; Sebastian Peter wa kata ya Ngokolo na Zacharia Mfuko wa Masekelo, walitangaza kujiuzulu nafasi hizo na kuacha kata mbili wazi.
Madiwani hao walikabidhi barua zao za kujiuzulu katika ofisi za Manispaa hiyo huku wakimweleza Kaimu Mkurugenzi, Mwanamsiu Dossi, sababu za uamuzi huo.
Pia walimtaka Dossi awaombee radhi kama kuna sehemu walikwaruzana na watendaji waliokuwa wakifanya nao kazi na kutaka wananchi wa kata hizo kuona kuwa kitendo walichofanya si kwa nia mbaya bali nia ni kujenga Taifa makini.
Kutokana na uamuzi huo, Chadema imebakiwa na madiwani sita huku CCM ikiendelea kuongoza Manispaa ikiwa na madiwani 14 na kuacha kata mbili bila uwakilishi.
Sababu ya uamuzi wao, ilitajwa kuwa ni mgogoro huo wakidai ya uongozi ngazi ya Taifa, umeendelea kusikiliza majungu, kudhalilisha baadhi ya viongozi pamoja na kuwaita wahaini au wasaliti katika chama bila kuchambua ukweli.
Wakizungumza mbele ya waandishi wa habari jana katika Ofisi ya Naibu Meya wa Manispaa, madiwani hao walidai kuwa mbali na mgogoro huo, uamuzi wao pia umesukumwa na ahadi hewa za viongozi wa Taifa wa chama hicho.
Waliita hatua hiyo ya kujiuzulu, kuwa ni kuwajibika kutokana na makosa yaliyofanywa na viongozi wa kitaifa kwa nyakati tofauti.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, baada ya kupata taarifa hizo akiwa kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Kalenga, aliwajibu.
Alisema Chadema iko tayari kubaki na watu wachache, lakini safi wenye dhamira na nia ya dhati ya kuendeleza mapambano ya kumpigania Mtanzania, kuliko kundi kubwa la watu wasio tayari kuuza wajibu waliokabidhiwa na Watanzania kwa maslahi binafsi.
"Tayari (madiwani hao) walikuwa na tuhuma wiki tatu zilizopita kuwa wamehongwa Sh milioni 20 kila mmoja, ili wapokewe na CCM. CCM inahonga madiwani ili waondoke kwa sababu wanazosema na kupokewa majukwaani," alidai Dk Slaa.
Pamoja na majibu hayo ya Dk Slaa, Peter ambaye pia alijiuzulu nafasi yake ya Katibu wa Mbunge wa Viti Maalumu, Rachel Mashishanga, alidai kuwa Novemba mwaka jana kikundi cha ulinzi cha Red Brigade, kiliandika barua kwa Dk Slaa na kudhalilisha viongozi.
Katika barua hiyo, viongozi hao akiwamo Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Shinyanga, Nyangaki Shilungusheila na Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Shinyanga, Siri Yasini, walidaiwa kuhongwa Sh milioni 90.
"Tuhuma hii ninaamini ni ya uongo iliyolenga kudhalilisha viongozi ambao kimsingi ndio waliotufikisha hapa tulipo.
"Katibu Mkuu wa Chama alipokea barua hiyo na kushindwa kuifanyia kazi na kusababisha viongozi hawa wafungiwe hata kwenye mkutano mkuu wa wilaya.
"Jambo hili limenifanya niamini kuwa nyuma ya Red Brigade kuna viongozi wa kitaifa wanaowaagiza kufanya hayo," alidai Peter.
Peter aliendelea kudai kuwa sababu nyingine ya kuchukua uamuzi huo, ni kutotekelezwa kwa ahadi za Mwenyekiti, Freeman Mbowe, kwamba chama kitamalizia kujenga nyumba ya marehemu Shelembi Magadula, aliyekuwa mgombea ubunge Shinyanga Mjini na Diwani wa Masekelo.
Alidai kuwa Mbowe alitoa ahadi hiyo kwenye maziko ya kiongozi huyo katika viwanja vya Shycom, lakini katika kikao kingine alichokuwa akikiongoza, alipinga ujenzi wa nyumba hiyo.
Jambo la tatu lililowasukuma kujiuzulu kwa mujibu wa Peter, ni tabia iliyozuka ndani ya chama ya kudhalilisha baadhi ya wanachama na viongozi kwa kuwabatiza majina ya wasaliti au wahaini.
Kwa mujibu wa madai ya Peter, waasisi wa kauli hizo ni viongozi wa kitaifa kitendo kilichomfanya aamini kuwa ni uongo ambao hauna tija katika chama.
"Mimi ni miongoni mwa wanachama nitakaokuwa wa mwisho kuamini kama kweli Zitto Kabwe, Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba na wengine ni wasaliti ndani ya chama hiki.
"Binafsi najiuliza kama kweli Zitto ni msaliti wa chama na kwa mujibu wa taarifa ya chama, kwamba mwaka 2008 na 2009 aligundulika kutumiwa na CCM, mwaka 2010 walimruhusu kugombea ubunge Kigoma Kaskazini kwa nini?"Alihoji Peter.
Alidai kwa hiari yake kulingana na hayo aliyopima ndani ya kichwa chake, kuna umuhimu wa kujiuzulu udiwani na ukatibu wa Mbunge ikiwa ni njia ya kuwafundisha viongozi namna bora ya kuwajibika.
Alidai asingeweza kujionesha mbele ya wananchi kwa mavazi ya kondoo, wakati ndani ya nyoyo ni mbwa mwitu na kuongeza kuwa hana mpango wa kujiunga na chama chochote, atabaki Chadema.
Zacharia aliunga mkono madai ya Peter, na kuongeza kuwa uamuzi wake ulitokana na ubabaishaji ndani ya chama.
Alidai kuwa aliripoti kwenye uongozi juu ya kashfa ya uongozi wa mtaa wa Masekelo, unaoongozwa na CCM kugawa kiwanja bila kushirikisha Kamati ya Ugawaji Viwanja ya Mtaa.
Baada ya kuripoti, alidai aliahidiwa kuwa chama kingeshughulikia, lakini hakuna kinachoendelea na uongozi wa chama uko kimya kinyume na sera ya Chadema ya kutetea wanyonge.
No comments:
Post a Comment