HATIMAYE 'MDUNGUAJI' WA TARIME ATIWA MBARONI TANGA...

Mtuhumiwa wa mauaji ya watu tisa wilayani hapa, ametiwa mbaroni huku mwenzake akiuawa katika majibizano ya risasi na polisi.
Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya kwa kushirikiana na raia wema na Polisi wa Mkoa wa Tanga ndio waliofanikisha ukamataji wa mtu huyo. 
Mauaji ya watu hao tisa yalianza kutekelezwa Januari 25-27 na mtu anayedaiwa kuwa ni Charles Range Msongo au Josephat Chacha Kichune (38) mkazi wa kijiji cha Kenyamanyori.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, mtu aliyeuawa alitambuliwa kwa majina ya Marwa Keryoba (42)  mkazi wa  kijiji cha Kebeyo ambaye inadaiwa alikuwa mhifadhi wa silaha iliyotumika kwa mauaji hayo.
Kamanda Kamugisha alisema wakati Kichune akikamatwa  Februari 6 mkoani Tanga, Keryoba aliuawa mjini Musoma mkoani Mara katika majibizano ya kurushiana risasi na polisi.
Alisema Kichune alikimbilia Tanga baada ya msako mkali kuendeshwa mkoani Mara ukishirikisha polisi na raia wema, ambapo ufuatiliaji wa Polisi ulibaini kuwa mtuhumiwa alitoroka kwa pikipiki kutoka Kenyamanyori hadi Musoma.
Inadaiwa alipofika Musoma alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa Keryoba eneo la Nyabisare kata ya Bweri na kuhifadhi bunduki aliyokuwa akiitumia kufanya mauaji.
“Baada ya kuhifadhi silaha hiyo alipanda basi na kwenda Tanga akipitia Arusha akitumia jina la Josephat Chacha kwenye tiketi yake … tulitoa taarifa kwa askari wa Tanga ambao walifanikisha ukamataji,” alisema Kamanda Kamugisha.
Aliongeza kuwa mtuhumiwa alipohojiwa na Polisi alikiri kufanya mauaji ya watu wilayani Tarime hususan katika kata za Turwa, Binagi na Kitare katika tarafa ya Inchage.
“Tulipomwuliza alikohifadhi silaha akasema ameihifadhi kwa Keryoba ambaye alihamia Bweri mwishoni mwa mwaka jana,” alisema na kuongeza kuwa walimchukua mtuhumiwa akawaoneshe alikokuwa akiishi mshirika wake na walipofika Keryoba alijaribu kutoroka akiwa na silaha.
“Alifyatua risasi akiwaelekeza askari ambao walijibu mapigo na kumjeruhi, lakini akafa akiwa njiani kukimbizwa katika hospitali ya mkoa mjini Musoma … tulichukua bunduki hiyo ya SMG iliyokatwa kitako, ikiwa na magazini yenye risasi tisa huku moja ikiwa tayari imekokiwa,” alisema Kamanda.
Upekuzi uliofanywa katika chumba alimokuwa akiishi Keryoba, ulibaini kuwamo deki moja, tochi mbili, pea ya viatu vya buti, simu mbili za mkononi, CD za picha mbalimbali, bidhaa za dukani na mpira wa baiskeli.
Polisi ilipongeza wananchi hususan raia wema kwa kujitolea kutoa taarifa na kuwaomba waendeleze moyo wa kushiriki mapambano dhidi ya uhalifu. 
Alisema Polisi itatoa zawadi ya Sh milioni moja kwa mtu atakayetoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa silaha ya moto au watuhumiwa wa ujambazi.
Mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote msako wa kukamata watuhumiwa wengine wa tukio hilo utakapokamilika.
Hivi karibuni, Kamanda Kamugisha alitangaza kukamatwa kwa watu 10 kutokana na mauaji hayo huku akikataa kutaja majina yao akihofia kuvuruga upelelezi na kusema mtuhumiwa inaonekana alikuwa akitumia silaha aina ya SMG au SAR kutokana na maganda ya risasi yaliyokutwa maeneo ya mauaji.
Januari 26, saa 12 asubuhi katika kijiji cha Mogabiri,   inadaiwa alimwua kwa risasi Zakaria Marwa (28) na Erick Lucas (24) baada ya kukutana nao njiani, kwa mujibu wa Polisi.
Siku hiyo hiyo saa 4 usiku katika kijiji hicho alidaiwa kumwua Robert Kisiri (45) baada ya kuvamia baa inayomilikiwa na Chacha Ryoba na kumjeruhi mtu mwingine.
Siku iliyofuata saa 11.30 alfajiri inadaiwa alifanya mauaji mengine katika kijiji hicho  kwa kumpiga risasi David Matiko (39) na kumpora simu aina ya Nokia.
Katika tukio hilo, alimjeruhi Machungu Nyamahemba (19) ambaye alilazwa katika hospitali ya Tarime kwa matibabu.  Siku hiyo  saa 2 usiku katika kijiji cha Nkende anadaiwa kumwua Juma Nyaitara (30)  na baada ya mauaji akapora simu za mkononi za Chacha Magige na Masero Marigiri.

No comments: