GODBLESS LEMA AMKWIDA SHATI KIGOGO WA CCM NDANI YA KITUO CHA POLISI...

Godbless Lema akiongozwa na wafuasi wake.
Wakati uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata ya Sombetini katika Jiji la Arusha, ukitarajiwa kufanyika kesho, hali imeanza kuwa tete baada ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wa Wilaya ya Arusha, Elisante Kimaro na Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema kukunjana mashati katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Arusha jana.
Wakati hayo yakifanyika, usiku wa kuamkia jana mashina matatu ya jumuiya ya vijana wa CCM (UVCCM) yaliyozinduliwa na Mjumbe  wa NEC katika wilaya ya Arusha, God Mwalusamba katika kata ya Sombetini Jijini Arusha yameng’olewa na bendera zake kuchomwa moto na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa  Chadema.
Akizungumzia tukio la kukunjana mashati, Katibu wa CCM wa wilaya ya Arusha, Elisante Kimaro alisema Mbunge Lema alitaka kulazimisha kufungua shina la vijana wa chama chake sehemu ya Sombetini shuleni, mahali ambapo CCM imezindua siku mbili zilizopita, kitu ambacho vijana wa UVCCM hawakukikubali.
Kimaro alisema kutokana na kutokuelewana ndipo Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha, Giles Mroto alipoitwa katika eneo la tukio na alilazimika kuwataka viongozi wote kwenda katika kituo kikuu cha polisi kwa mahojiano zaidi.
Alisema walipofika polisi alishangaa kuona Mbunge Lema akiwa mbogo na kutaka kumpiga kwa kufikia hatua ya kumshika shati lakini na yeye hakukubali na kuamua kumshika shati na tukio hilo lilitokea mbele ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Arusha.
"Tulikunjana mashati mbele ya OCD Mroto tukiwa kaunta ya polisi kituo kikuu, na polisi waliamua kutuamulia na kutakiwa kwenda ofisini kwa OCD kwa majadiliano zaidi,’’alisema.
Katibu huyo alisema, “OCD alitusihi kuacha vurugu kama viongozi na kuwa mfano bora kwa wafuasi wa vyama vyetu na tuliruhusiwa kuondoka polisi na kuendelea na kampeni na Lema alizuiliwa kufungua shina mahali ambapo CCM imefungua na kulizindua”.
Alisema cha kushangaza usiku wa kuamkia jana mashina yote matatu yaliyozinduliwa na Mwalusamba yameng’olewa na bendera zake kuchomwa moto, kitu ambacho alidai kimefanywa na Lema na wafuasi wake.
Kimaro aliyataja mashina yaliyong’olewa na bendera zake kuchomwa moto ni pamoja na Godauni, Nguselo na Sombetini shuleni Kona.
Katibu huyo alisema amewaita vijana wa UVCCM na kuwasihi kuacha kulipiza kisasi kwani Chadema wanataka vurugu na umwagaji damu ili uchaguzi huo uahirishwe kwani kwa sasa hali yao sio nzuri.
“Tunajua njama zao na sisi kama chama na jumuiya zake tumeamua kutolipiza kisasi na kuwasihi vijana kuendelea na kampeni zenye ustaarabu ili kesho upigaji kura uwe na amani bila ya vurugu na tuna uhakika wa kuwapiga katika kinyang’anyiro hizo,’’alisema Kimaro.
Mwandishi alipomtafuta Lema kupitia simu yake ya mkononi iliita bila majibu na hadi tunakwenda mitamboni simu hiyo haikupokelewa.
Wakati hayo yakijiri, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema kata ya Sombetini, Iddy Mdava siku moja kabla ya uchaguzi wa kata hiyo yeye na kamati nzima ya siasa ya kata hiyo imehamia CCM juzi na kuleta hofu kwa chama hicho katika uchaguzi wa kesho kama itashinda.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Madava alisema ni kutokana na baadhi ya viongozi wa juu wa Chadema kulazimisha Ally Bananga kugombea udiwani katika kata hiyo bila ya kufuata demokrasia.
Madava alisema Banga sio chaguo la Chadema wa kata ya Sombetini bali ni shinikizo la viongozi wa juu wa Chadema kwa ushawishi wa Lema, kitu ambacho ni hatari ndani ya chama hicho chenye upendeleo wa hali ya juu.
“Chaguo la wana-Chadema Sombetini ni Gody na mimi Madava na sio Bananga lakini kwa kuwa demokrasia ndani ya Chadema hakuna tunalazimishwa kwa nguvu na viongozi wa juu wa chama hicho,” alisema Madava.
Madava alisema kuna wanachama wengi wa Chadema na viongozi wa kata wako njiani kukihama chama hicho kutokana na chama hicho kuendeshwa kibabe na upiundishwaji mkubwa wa demokrasi, kitu ambacho kinawakatisha tamaa. 
Alisema kwa sasa Chadema imekosa mwelekeo na iko siku hayo yote yatakuwa hadharani kwani baadhi ya wana-Chadema na viongozi wanayaficha bila ya sababu za msingi wakati hali ni mbaya.
Akizungumzia hilo, Katibu wa CCM wa wilaya ya Arusha, Elisante Kimaro alisema kuwa chama kimempokea na kinamkabidhi Madava kwa uongozi wa tawi aliko ili chama kiweze kumchunguza mienendo yake isije ikawa Chadema imeleta pandikizi.
Kimaro alisema kamati ya siasa ya tawi ndio wenye jukumu la kujua kama kweli amerudi kwa dhati ama kwa kutaka kuchunguza na baada ya kujiridhisha chama kitampokea rasmi kwa mkutano mkubwa na kumkaribisha rasmi CCM kwa mikono miwili.
Uchaguzi wa Kata ya Sombetini unatarajia kufanyika kesho na mchuano mkali uko kwa wagombea watatu wa vyama vya CCM, Chadema na CUF.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas amewataka viongozi wa vyama vyote na wafuasi wao kuwa watulivu katika muda huu wa dakika za mwisho na siku ya upigaji kura na yeyote atayedhubutu kuleta vurugu polisi haitasita kumchukulia hatua.
“Hatutaangalia mtu katika vurugu kwani yeyote mwenye kuleta vurugu dola iko na itamchukulia hatua bila ya woga kwani hakuna mtu yuko juu ya sheria na polisi hailifumbii macho hilo,’’ alisema.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva amesema kuwa hali ya  kisiasa Jijini Arusha na kata 26 nchini zinazotarajia kufanya uchaguzi kesho ni safi  kwani vyombo vya dola vimejipanga kuhakikisha  wananchi wa kata zote wanapiga kura na kutimiza wajibu wao.
Aidha amesema kuwa serikali imetoa  Sh bilioni 279 kwa ajili ya uboreshwaji wa  Daftari la Kudumu la Wapigakura na hivi sasa hatua za awali zinaendelea kufanyika kwa kupitia vituo vya kupigia kura ili visogezwe maeneo jirani na mahali wanapoishi wananchi.
Jaji Lubuva aliyasema hayo jana Jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na viongozi mbalimbali vya vyama vya siasa juu ya hatua mbalimbali za Tume walizoziona katika chaguzi za udiwani zinazotarajia kufanyika nchi nzima kesho.
Alisema  ingawa kasoro za hapa na pale zilijitokeza wakati wa kampeni za kila vyama lakini anaamini polisi waliweza kuzishughulikia pamoja na wasimamizi wa Tume ya Maadili lakini malalamiko mengi ya tume ya maadili waliyokuwa wakiyapata ni kutoka vyama viwili vya upinzani yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambapo kulikuwa na majibizano ya hapa na pale.
"Tume haijafurahishwa na matokeo ya vurugu wakati wa kampeni za udiwani yaliyotokea katika kata mbalimbali za uchaguzi, lakini nasema ni vyema wahusika wa vyama vya siasa kunadi sera na si kupigana lakini na hao waliofanya vurugu polisi wakidhibitisha watachukuliwa hatua za kisheria pia daftari la wapigakura litaboreshwa kwani serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya kuboresha daftari hilo na hivi sasa kazi imeanza, jitokezeni wananchi mkapige kura''.
Alisema vituo vipo zaidi ya 62  vya kupigia kura huku wasimamizi wa uchaguzi wakiwa 86 ikiwemo wasimamizi wa vituo 62, wasimamizi wasaidizi 62, makarani waongozaji 62 ,wasimamizi wa akiba 4 na kutoa rai kwa wananchi kujitokeza kupiga kura siku hiyo.

No comments: