Moja ya matukio ya ghasia kati ya wafuasi wa Chadema na wale wa CCM. |
Hata hivyo, uongozi wa CCM mkoani Mara kupitia kwa Mwenyekiti wa Mkoa, Christopher Sanya umekanusha wafuasi na walinzi wao kuwashambulia watu hao, akiwemo mwandishi huyo wa habari wa gazeti la Mwananchi.
“Wakati unaodaiwa kufanyika vurugu hizo sisi hatukuwepo hata hatujui mwandishi huyo alipigwa na nani na kwa kosa gani,” alisema kiongozi huyo wa CCM mkoani Mara.
Watu waliojeruhiwa ni Emma Malibwa (36) mkazi wa mjini Bunda na Jonathan Matiku (50), mkazi wa Bunda Stoo, ambao wote ni makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Habari kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa baada ya mkutano wa hadhara wa CCM kuisha wafuasi wa Chadema waliokuwa karibu na eneo hilo, waliinua picha za mgombea wao na kuzomea msafara wa CCM.
Hali hiyo iliamsha hasira kwa wafuasi na walinzi wa CCM maarufu kama Green Guards na kuwashambulia makada wa Chadema, na kumjeruhi Malibwa.
Wakati wanawashambulia makada wa Chadema, mwandishi huyo wa habari kutoka gazeti la Mwananchi aliyekuwemo kwenye gari la wanaCCM hao, alishuka na kupiga picha ndipo baadhi ya wanaCCM bila kumtambua kama ni mwandishi na kudhani naye ni kada wa Chadema walimpiga na kumnyang’anya kamera yake.
Hata hivyo, mwandishi anayetuhumiwa kuchukua kamera ya mwanahabari huyo alipohojiwa na gazeti hili alisema aliichukua kwa nia nzuri ili isiharibiwe na watu hao na kwamba ameihifadhi na atampatia.
Mwandishi huyo Christopher Maregesi (40), mkazi wa mjini Bunda, amedai kuwa ameshambuliwa na wafuasi hao wa CCM wakati akitekeleza majukumu yake ya kupiga picha na kuandika habari katika eneo la ofisi ya CCM ya wilaya.
Malibwa na Maregesi walidai kuwa baada ya kushambuliwa walikamatwa na kufungiwa ndani ya ofisi ya CCM kwa muda na kisha kupelekwa polisi na kufunguliwa kesi za kufanya vurugu.
Aidha, juzi jioni viongozi wa Chadema pamoja na baadhi ya waandishi wa habari walifuatilia polisi kwa ajili ya kuwapa dhamana, lakini watu hao waliohojiwa na polisi kwa zaidi ya saa tatu na kisha kupewa dhamana, walipelekwa katika hospitali teule ya wilaya ya Bunda kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo Maregesi jana asubuhi aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo baada ya kupata nafuu.
Vurugu hizo zilianza kutokea jioni, baada ya mkutano wa kampeni wa CCM uliokuwa unahutubiwa na Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye kumalizika katika eneo la Senta ya Nyasura mjini Bunda.
Wakisimulia mkasa huo, majeruhi hao walisema kuwa walitekwa na wafuasi wa CCM na kupigwa na kisha kufungiwa katika ofisi ya chama hicho kwa zaidi ya dakika 40 na kisha kupelekwa polisi, wakishitakiwa kuwa wamewafanyia fujo huku mwandishi huyo akituhumiwa kupiga picha katika eneo la ofisi ya CCM.
Naye Matiku alisema kuwa alishambuliwa na kikundi cha watu hao wanaodhaniwa kuwa ni wa CCM na kukatwa panga kichwani wakati akitoka polisi kuona waliojeruhiwa na kuwapa dhamana.
“Wakati nikitoka polisi saa 3:30 usiku nilivamiwa na watu hao na kunikata mapanga kichwani, lakini nimewatambua karibu wote,” alisema.
Baada ya kukamatwa watu hao, viongozi wa Chadema wakiwa na wafuasi wengine wa chama hicho walifika katika kituo cha polisi na kutaka kuwawekea dhamana.
Diwani wa kata ya Balili, Georges Miyawa (Chadema) alionekana mbogo katika kituo hicho na kudai kuwa iwapo watu hao hawataachiwa lolote laweza kufanyika.
Watuhumiwa wote walipewa dhamana na kuandikiwa fomu ya polisi kwa ajili ya kwenda kutibiwa hospitalini, ambapo wote akiwemo mwandishi wa habari, Maregesi waliwekewa dhamana na Diwani huyo wa Chadema.
Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Ferdinand Mtui, alithibitisha kuwepo kwa matukio hayo na kwamba upelelezi bado unaendelea.
Mtui alisema kuwa watawakamata wote waliohusika na kuwafikisha kwenye sheria.
Alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kusema kuwa jeshi hilo limejipanga vilivyo ili kuhakikisha uvunjifu wa amani hautokei katika uchaguzi huo mdogo wa udiwani kata ya Nyasura.
Msimamizi mkuu wa uchaguzi katika wilaya ya Bunda, Simon Mayeye jana hakupatikana kuzungumzia tukio hilo.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia aliyekuwa diwani wa kata hiyo kupitia tiketi ya Chadema kufariki dunia mwaka jana.
Uchaguzi huo mdogo wa udiwani utafanyika leo katika kata 28 kwa nchi nzima, ili kuziba mapengo hayo ambapo kwa mkoa wa Mara ni kata ya Nyasura pekee, ambapo vyama vya CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD, vimesimamisha wagombea wao.
Akihutubia katika mkutano huo, Nape aliwaomba wananchi wa kata ya Nyasura kuchagua mgombea wa CCM na akafananisha vyama vya upinzani sawa na jogoo ambaye hata kama akiwika kutoka kwake nje mpaka mwenye mji afungue mlango hata kama ni saa 6:00 mchana.
Alisema kuwa ili kata hiyo kuharakishiwa maendeleo ni vema wananchi wakachagua mgombea wa CCM, Alexander Mwikwabe, kwani chama kilichoko kwenye madaraka ndio chama chake na maendeleo yataletwa kutokana na mipango.
No comments:
Post a Comment