Mita za kusomea umeme. |
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Kijamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo alisema jana kuwa kupanda kwa gharama za umeme ni moja ya sababu ambazo zimechangia kuwepo kwa ongezeko la mfumuko wa bei.
Mwezi jana, NBS ilitangaza kushuka kwa mfumuko wa bei kutoka asilimia 6.2 ya Novemba hadi kufikia asilimia 5.6 Desemba 2013. Kushuka huko kulichangiwa na kupungua kwa bei za bidhaa za vyakula hasa mchele na bidhaa zisizo za vyakula hasa vifaa vya kielektroniki.
Lakini hali imebadilika, baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) kuruhusu Shirika la Umeme (Tanesco) kupandisha bei ya umeme kuanzia Januari mosi mwaka huu, wananchi wameanza kuonja machungu hayo kutokana na bidhaa zingine nazo sasa kupanda bei.
Kwesigabo alisema jana kuwa kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa Januari 2014 kunaamisha kuwa kuna kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa Januari ikilinganishwa na kasi ya kupanda kwa bei kwa Desemba mwaka jana.
"Kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwezi Januari kumechangiwa hasa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa bidhaa zisizo vya vyakula," alisema mkurugenzi huyo.
Bidhaa hizo ambazo sio za vyakula zimetajwa kuwa ni ankara za umeme kwa matumizi ya nyumbani na gesi ambazo bei zake kuanzia Januari zilipanda na kulalamikiwa zaidi na wananchi.
Alitaja bidhaa zingine zisizo za vyakula zilizosababisha kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa Januari mwaka huu ni pamoja na karo za shule binafsi za msingi na sekondari, sare za shule na kodi za nyumba za makazi binafsi.
Kuanzia Januari Tanesco ilipandisha bei ya umeme wa majumbani kutoka Sh 221 hadi Sh 306 kwa uniti moja, ongezeko la bei kwa uniti moja ni Sh 85.
Licha ya bei ya uniti moja kupandishwa, lakini pia tozo la kutoa huduma kwa mteja iliongezwa kutoka Sh 3,841 hadi Sh 5,520.
Bei hiyo mpya imelalamikiwa na wananchi kwani mteja anayetoa Sh 10,000 kununua umeme, anaambulia kupata uniti nane za umeme, hivyo kufanya gharama za umeme kuwa anasa kwa baadhi ya familia.
Kwa wananchi wa vijijini ambao matumizi yao sio zaidi ya uniti 75, wao wananunua umeme kwa Sh 100 badala ya Sh 60. Ila mtumiaji ambaye anavuka matumizi ya uniti 75 atanunua umeme kwa Sh 350 badala ya Sh 275.
Bei ya gesi inayotumika kupikia majumbani nayo ilipanda kwa mtungi wa kilo 15 kutoka Sh 54,000 hadi Sh 63,000. Bidhaa zote hizo NBS imethibitisha kuwa imechangia kuwepo kwa ongezeko la mfumuko wa bei.
Katika mchanganuo wa bei hizo, umeme umeongoza kuongeza bei kwa asilimia 42.6, gesi ya kupikia asilimia 10.2, karo ya shule za msingi binafsi asilimia 10.2, sare za shule za msingi asilimia 5.1, karo za shule binafsi sekondari asilimia 8.1 na bima za magari binafsi kwa asilimia 1.4.
Kwesigabo alisema umeme unategemewa na kila sehemu, hivyo kupanda kwake ndio mwanzo wa kufanya mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali nchini nazo kupanda.
"Itategemea Serikali imejipanga vipi kudhibiti hali hii, lakini ukweli ni kwamba madhara yake yameanza pole pole na pia bei inaweza kushuka kutegemeana na Serikali ilivyojipanga," alisema mkurugenzi huyo.
Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani umebaki kuwa asilimia 6.6 Januari, 2014 kama ilivyokuwa Desemba. Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula kasi ya ongezeko la bei imeongezeka hadi asilimia 6.7 kwa Januari kutoka asilimia 5.5 ya Desemba 2013.
Akizungumzia mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi, nako alisema umeongezeka kwa asilimia 1.8 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 1.3 kama ilivyokuwa Desemba mwaka 2013.
Alisema baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa bei ni mchele asilimia 2.0, mahindi asilimia 2.8, nyama asilimia 1.7, samaki wabichi asilimia 3.7, matunda asilimia 4.7 na mboga asilimia 6.7.
Kuhusu thamani ya Shilingi ya Tanzania, Kwesigabo alisema uwezo wa Sh 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma kwa Januari 2014 umefikia Sh 68 na senti 21.
No comments:
Post a Comment