WABUNGE WAPINGA KIINGEREZA KUTUMIKA KUFUNDISHIA MASHULENI...

Wabunge ndani ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.
Mjadala kuhusu lugha ya kutumia kufundishia shuleni umepamba moto, ambapo baadhi ya wabunge wamejitokeza kupinga Kiingereza kutumika kufundishia shule za msingi mpaka vyuo vikuu.
Wakati wabunge hao wakiwa na msimamo huo, jana Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, alisema Serikali haijafikia uamuzi wa kuruhusu Kiingereza kutumkika kuanzia shule za msingi, na hivi sasa inashughulikia changamoto kubwa zaidi.
“Haya yote yanaweza kutatuliwa iwapo sekta hii tutaibadili na kuwa ya kisasa zaidi, katika eneo la vitabu kila mwanafunzi akiwa na kompyuta yake ni rahisi kitabu kuwekwa kwenye CD na wanafunzi wote wakakisoma kupitia kompyuta zao,” alisema Profesa Mchome alipozungumza na gazeti hili.
Mbunge wa Kibiti, Abdul Malombwa  akizungumza jana katika ofisi ndogo za Bunge alipinga matumizi ya Kiingereza badala ya Kiswahili shuleni na kusisitiza kuwa kitendo hicho si tu kitaua Kiswahili bali pia kitaondoa uwezo wa mwanafunzi kuelewa.
“Kwenye ripoti yetu tumeweka wazi kuhusu hili, tunataka lugha ya Kiswahili itumike kufundishia hadi vyuoni, na tumetoa mapendekezo yetu ya namna ya kutekeleza mfumo huu, ikiwamo kuboresha Kiswahili chenyewe ili kiendane na masomo,” alisema Malombwa ambaye pia ni mjumbe wa Jukwaa la Taasisi na Mamlaka za Udhibiti wa Ubora wa Elimu nchini.
Aliongeza kuwa walipendekeza kila mkoa angalau uwe na shule moja ya sekondari ambayo itafanya majaribio ya kufundisha kwa Kiswahili masomo yote na kuona kama itafaa au la.
Mbunge wa Mgogoni, Kombo Khamis Kombo, alisema anasikitishwa na namna Kiswahili kinavyonyimwa kipaumbele katika elimu, kiasi cha nchi jirani ya Kenya kubeba sifa ya ujuzi wa lugha hiyo kimataifa.
“Hii ni lugha yetu lazima tuipe kipaumbele tuijenge, lakini leo nashangaa eti Wakenya ndio wanaonekana wanaijua vizuri na wanapewa kazi za kufundisha mataifa mengine, hatukubali hili lazima libadilike,” alisisitiza.
“Jukwaa la Taasisi na Mamlaka za Udhibiti wa Ubora wa Elimu nchini limetoa maoni yake kwa Waziri Mkuu juu ya suala hili la matumizi ya lugha ya Kiswahili shuleni, tunasubiri kwanza tuone namna ya kufanya,” alisema Profesa Mchome.
Aliongeza kuwa Serikali inatambua changamoto zote zinazoikabili sekta ya elimu na ndiyo maana ina mikakati ya kuboresha sekta hiyo, ili kukabiliana na changamoto zilizopo.
Alisema kwa sasa moja ya changamoto katika sekta hiyo ni pamoja na uhaba wa walimu na vifaa. 
Alifafanua kuwa tayari katika nchi zilizoendelea, sekta ya elimu imekua, kiasi cha matatizo kama walimu kuwa historia kwani mwalimu mmoja haijalishi yuko wapi, anaweza kufundisha darasa kokote aliko kwa kutumia mitandao inayomwezesha  kuonana ana kwa ana na wanafunzi kupitia kompyuta kubwa.
Kwa muda mrefu tangu uhuru, shule zote za msingi za Serikali zilikuwa zikitumia Kiswahili kufundishia masomo yote isipokuwa somo la Kiingereza.
Baada ya kumaliza shule ya msingi, mwanafunzi akiingia sekondari alikuwa akibadilisha mfumo ghafla na kuanza kufundishwa masomo yote kwa Kiingereza isipokuwa somo la Kiswahili.
Shule za msingi za Serikali ambazo zilikuwa zikitumia Kiingereza kufundisha masomo yote ni shule za msingi za Olympio na Diamond za Dar es Salaam na ya Arusha, jijini Arusha.
Lakini mwaka huu tayari shule ya Oysterbay  ya Dar es Salaam, imeanza mchakato wa kuhama kutoka Kiswahili kufundishia masomo yote na Kiingereza kuwa somo la kawaida, mpaka kufundisha masomo yote kwa Kiingereza na Kiswahili kuwa somo la kawaida.
Mbali na shule hiyo, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf Mwenda, alisema zipo shule zingine Kinondoni, zimeshapeleka maombi kutaka kuhamia mfumo wa kufundisha masomo yote kwa Kiingereza.

No comments: