USHAHIDI DHAIFU WAWANUSURU ABSALOM KIBANDA NA WENZAKE...

Absalom Kibanda.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia huru aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda na wenzake baada ya kuwaona hawana hatia katika mashitaka ya uchochezi yaliyokuwa yanawakabili.
Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alitoa hukumu hiyo jana akisema upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya washitakiwa hao.
Mbali na Kibanda, washitakiwa wengine walioachiwa huru ni Meneja Uendelezaji Biashara wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Theophil Makunga na mwandishi wa habari Samson Mwigamba.
Washitakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashitaka ya kuandika na kuchapisha makala ya uchochezi iliyokuwa ikishawishi askari wa majeshi yote wasitii Serikali.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Lema alisema upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha makala hayo yaliandikwa na nani zaidi ya mshitakiwa kukiri mwenyewe, pia hawajaeleza Kibanda na Mwigamba walihusika vipi.
"Kwa mtu yeyote mwenye akili timamu hawezi kusema ile ilikuwa makala ya uchochezi, bali  Mwigamba alitumia haki yake kikatiba ya kutoa maoni yake na kulikumbusha Jeshi la Polisi kuhusu utendaji wa kazi," alisema Hakimu Lema.
Alisema kwa mujibu wa sheria, chapisho linatakiwa lioneshe nia ya uchochezi ambayo huthibitishwa na matokeo, liwe la uhasama kwa mamlaka husika, lakini ushahidi haujaonesha kama kulikuwa na chuki wala askari aliyegoma baada ya kusoma makala hayo.
Aliongeza kuwa katika ushahidi hakuna sehemu yoyote iliyomtaja Makunga na Kibanda kuchapisha makala hayo, jambo linaloonesha walishitakiwa kwa hisia, kutokana na maelezo yaliyo kwenye gazeti lakini hisia haziwezi kusimama na kumtia mtu hatiani.
Hakimu Lema alisema upande wa Jamhuri ndio wenye jukumu la kuthibitisha mashitaka, hivyo walitakiwa kuonesha nani aliyeandika na nani aliyehariri, kitu ambacho hawakukifanya.
Akizungumza nje ya Mahakama, Wakili wa Utetezi Nyaronyo Kicheere alisema kesi hiyo ni ushindi kwa waandishi wa habari kuwa wana haki ya kutoa maoni yao, kwa sababu alichofanya Mwigamba ni kutoa maoni jinsi Jeshi linavyotakiwa kufanyakazi na si uchochezi.
Kibanda na Makunga walisema kipindi cha miaka miwili ya kesi kilikuwa cha mateso kwao, kwani  walishindwa kufanya kazi zao za uandishi wa habari vizuri, pia walishindwa kusafiri kwa kuwa hati zao za kusafiria zilizuiwa mahakamani na walipokuwa wakiomba walikataliwa.
Mwigamba na Kibanda walidaiwa kuwa Novemba 30, 2011, kwa nia ya kuvunja sheria, walitenda kosa la uchochezi kwa kuruhusu makala ya uchochezi ichapishwe kwenye gazeti la Tanzania Daima la Novemba 30, 2011.
Makala yaliyoandikwa na Mwigamba yalikuwa na kichwa cha habari kisemacho: “Waraka maalumu kwa askari wote,” ambapo inadaiwa yalikuwa yakishawishi askari wasitii Serikali.
Makunga alishitakiwa kutokana na Kampuni ya Mwananchi, kuchapisha gazeti la Tanzania Daima likiwa na makala hayo yaliyodaiwa kuwa ya uchochezi, wakati akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo.

No comments: