TICTS YAPIGWA MARUFUKU KULIPISHA WATEJA KWA DOLA...

Shehena ya makontena bandarini Dar es Salaam.
Wizara ya Fedha imeipiga marufuku Kampuni ya Kuhudumia Kontena Bandarini  (TICTS), kulazimisha wateja kulipia huduma kwa dola ya Marekani.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema Dar es Salaam jana kuwa Wizara imeamuru kufutwa kwa masharti yanayolazimisha wateja kulipia huduma kwa fedha za kigeni.
"Tuliamua kuwazuia TICTS kulazimisha wateja walipie huduma kwa dola kwa sababu haikupaswa kufanya hivyo. Hii ni nchi yenye fedha yake, na ndiyo inayopasa kutawala sokoni wakati wote,  kuwalazimisha wananchi watumie fedha ya nchi nyingine  ni kosa," alisema. 
Alifafanua kuwa katika maeneo ya kitalii kama vile kwenye hoteli kubwa zinazotumiwa zaidi na wageni, katika shule za kimataifa na kwenye huduma nyingine ambazo wateja wake wengi si Watanzania, kunaweza kuwa na utaratibu wa kulipia kwa dola lakini si lazima.
"Vinginevyo, kutumika au kutotumika kwa dola ni hiari ya mteja au mtaka huduma. Hata hizo hoteli na shule za kimataifa nazo zinapaswa kupokea shilingi ya Tanzania na kubadili na wala si kukataa kutoa huduma eti kwa sababu kinacholipwa si dola. Watanzania ni lazima watambue thamani ya fedha yao," alisema.
Kauli hiyo ilitolewa wakati TICTS ilishasitisha uamuzi wake wa kulazimisha wateja kulipia huduma kwa dola.
Baadhi ya wateja wa kampuni hiyo, akiwamo Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wakala wa Forodha  na Uondoshaji wa Shehena Tanzania (TAFFA), Edward Urio, alisema tangazo laTICTS la kusitisha malipo kwa dola, lilitolewa kwao kimyakimya.
Hata hivyo, alisema baada ya hatua hiyo, TICTS walipandisha kiwango cha kubadilisha fedha kuzidi kinachotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wakinunua dola kwa Sh 1,658 badala ya Sh 1615.24 za BoT.
Kutokana na hatua hiyo, TAFFA waliazimia kwenda kumwona Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ili aweze kutoa ufumbuzi wa tatizo hilo.

No comments: