MDUNGUAJI AUA MWANAJESHI NA WATU WENGINE WANANE TARIME...

Mdunguaji akiwa mawindoni.
Jeshi la Polisi limeanzisha operesheni maalumu ya kumsaka mtu anayedaiwa kuwa jambazi, ambaye anaendelea kufanya mauaji wilayani Tarime.

Jambazi huyo ambaye amefanya mauaji katika vijiji vya Mogabiri na Nkende, wilayani Rorya Tarime, imeelezwa mpaka sasa ameshaua watu  tisa na kujeruhi wengine wawili, ambapo anatembea na bunduki aina ya SMG.
Akizungumza na waandishi wa habari  jana Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi nchini, Paul Chagonja alisema, mwuaji huyo amekuwa akiua watu wasio na hatia, pia inasadikiwa kuwa si mkazi wa eneo hilo bali ni mgeni.
Alisema sababu ya mtu huyo kufanya mauaji hayo haijulikani kwani anapofanya mauaji hachukui mali isipokuwa ndogo, ambapo alisema anachukua simu, mikate, biskuti na soda.
“Januari 26, saa 12 asubuhi katika kijiji cha Mogabiri katika Mkoa wa kipolisi Tarime Rorya,   alimwua kwa risasi Zakaria Marwa (28) na Erick Lucas (24) baada ya kukutana nao njiani,” alisema Chagonja.
Alisema siku hiyo hiyo saa 4 usiku katika kijiji hicho alimwua Robert Kisiri (45) baada ya kuvamia baa inayomilikiwa na Chacha Ryoba na kumjeruhi mtu mwingine.
Aliongeza kuwa siku iliyofuata saa 11.30 alfajiri alifanya mauaji mengine katika kijiji hicho  kwa kumpiga risasi David Matiko (39) na kumpora simu aina ya Nokia.
Katika tukio hilo alimjeruhi Machungu Nyamahemba (19) ambaye bado amelazwa Hospitali ya Tarime kwa matibabu. Chagonja aliongeza kuwa   siku hiyo  saa 2 usiku katika kijiji cha Nkende alimwua Juma Nyaitara (30)  na baada ya mauaji hayo alipora simu za mkononi za Chacha Magige na Masero Marigiri.
“Usiku wa kuamkia Januari 28,   aliua watu wengine watatu ambao bado majina yao hayajafahamika. Mmoja alipigwa risasi wakati akiendesha pikipiki katika kijiji cha Nkende, wengine wawili waliuawa baada ya kukutwa wakitengeneza gari lililokuwa limewaharibikia katika kijiji cha Mogabiri,” aliiongeza.
Mpaka sasa juhudi za kumsaka mtu huyo bado zinaendelea, pia wanashirikiana na vyombo vingine vya usalama ili kufanikisha kukamatwa kwa mtu huyo.
Alisema Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu ametuma timu maalumu kutoka makao makuu ya Polisi inayohusisha Kamisheni ya Operesheni, Upelelezi na Intelijensia kwenda kuongeza nguvu katika juhudi zinazofanywa na ngazi ya mkoa, kuhakikisha mtu huyo anakamatwa haraka iwezekanavyo ili kuwaondoa hofu wananchi.
“Anaua watu wasio na hatia na sababu  ya kufanya mauaji hayo haijulikani kwa sababu hakuna mali anazochukua, lakini tutahakikisha jambazi huyu anapatikana ili wananchi waendelee kuishi kwa amani,” alisema.
Chagonja alisema wanatoa mwito kwa wananchi wote kutoa ushirikiano ili mtu huyo aweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria haraka, alitaka kwa yeyote atakayekuwa na taarifa atumie namba maalumu ambazo ni 0754 785 557.
Taarifa zilizopatikana mapema, zilisema watu waliopoteza maisha walitambuliwa kuwa ni askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Koplo Zakaria Mwita ambaye ni mtoto wa marehemu Meja Jenerali Mwita Marwa na aliyekuwa Mhandisi Ujenzi wa Wilaya ya Rorya na Mkandarasi, David Misiwa ambaye pia alikuwa akimiliki kampuni binafsi ya Yomani.
Waliouawa wengine katika mashambulizi tofauti ya siku tatu kuanzia Januari 26 hadi juzi, ni aliyekuwa mfanyabiashara wa magari ya kusafirisha abiria, Samwel Mohenga na mwendesha bodaboda mkazi wa kijiji cha Nkende, Juma Nyaitara.
Wengine ni Erick Makanya ambaye ni mjukuu wa Meja Jenerali Marwa na mfanyabiashara wa duka la nyama mkazi wa kijiji cha Rebu, Juma Mroni na mkazi wa Kenyamanyori, Robert Kisiri.
Kutokana na hali hiyo, jana kati ya saa 4 na 5 asubuhi mtu aliyekuwa amevaa koti refu alinusurika kushambuliwa na wananchi akidhaniwa ndiye muuaji anayesakwa, lakini aliokolewa na polisi waliolazimika kufyatua risasi angani na kutawanya wananchi hao na kisha kumpeleka kituoni. Ilibainika hakuwa anayesakwa.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele wakishirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime, jana walitembelea maeneo ya  mauaji hayo.
Mkazi  wa kijiji cha Kisa, tarafa ya Kipeta, bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga , Josephat  Chinga ‘Bonge’ (32)  anadaiwa  kumwua  hawara  wake  kikatili  kwa  kumchinja  kisha  kuhifadhi  kichwa chake ndani ya  sufuria.
Pia anatuhumiwa kukata  viganja  vya mwanamke  huyo  na kutokomea  navyo  kwa imani  za kishirikiana.
Inadaiwa  Chinga  alikodisha  watu  wanne  kumwua  mpenzi wake  huyo kwa  ahadi ya malipo  ya Sh  milioni 1.6 - ambapo kila mmoja  angelipwa Sh 400,000 -  baada ya mauaji  hayo.
Taarifa kutoka  eneo la  tukio ambazo  zilithibitishwa na Polisi zilidai kuwa  Chinga  alihitaji  viganja  vya  mpenzi  wake  huyo,  kwa kuwa vina  alama  ya ‘M’  ambayo  ni imani kuwa alama  hiyo  inahitajika kutengeneza  dawa  ya kutajirisha  mtu.
Mtoa taarifa kutoka eneo la  tukio,  alidai  kuwa  baada ya Chinga  kushindwa  kutimiza  ahadi  yake  ya uwalipa kiasi  hicho cha  fedha,  watuhumiwa  hao  waliokodishwa  walimwibia  kichwa  alichokuwa  amehifadhi kwenye  sufuria  na kukitelekeza  kwenye  uwanja wa michezo  wa shule ya msingi ya Kisa. 
Inadaiwa  watuhumiwa  hao  waliandika  barua na kueleza mkasa mzima  kisha  kuipachika pembeni  mwa sufuria lenye kichwa cha marehemu.
Akithibitisha  kutokea  kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi  wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda  alibanisha kuwa  watuhumiwa  hao  walikamatwa  mwanzoni  mwa  wiki  hii,  baada ya kichwa  hicho kugundulika kwenye uwanja wa michezo.  
Mwaruanda  aliongeza kuwa  mwanamke huyo, Ritha Malecela (35) alipotea  katika mazingira ya kutatanisha  Desemba  mwaka  jana  hadi  mwanzoni  mwa wiki  hii. 
Uchunguzi  wa awali  kwa mujibu  wa Mwaruanda  ulibainisha kuwa Desemba 10, mwaka  jana  Ritha ambaye alikuwa  akiishi  kinyumba na Chinga baada  ya kutoroka kwa mumewe  na kupotea  katika mazingira ya kutatanisha.
"Polisi  kwa  kushirikiana na wananchi  tuliendesha msako  bila  mafanikio wakati  uchunguzi  ukiendelea  kuhusu kupotea kwake, Januari  23 kichwa  cha mwanamke  kilikutwa katika uwanja  wa  michezo kwenye sufuria," alibainisha.
Mwaruanda alibainisha kuwa  pembeni  mwa  sufuria   hilo kulikuwa  na barua  inayosadikiwa kuandikwa na  mmoja  wa watuhumiwa  hao,  akimtaja  Chinga  aliyekuwa  hawara wa marehemu  ndiye aliyewakodisha  kumwua Ritha.
Kwa mujibu  wa  Kamanda Mwaruanda  baada ya kufanya mauaji  hayo  walitupa  ndani ya Ziwa  Rukwa  huku kichwa chake kilichukuliwa na hawara  yake  ambaye aliwaahidi  ujira  wa Sh 400,000 - kila  mmoja aliyeshiriki  kumwua mwanamke  huyo .
Inadaiwa kuwa  baada  ya  Chinga  kushindwa  kutimiza  ahadi  yake  ya kuwalipa 'wauaji '  hao  mmoja wao  aliamua  kutoboa  siri  hiyo hadharani.
Kamanda  Mwaruanda  akifafanua  alidai kuwa  watuhumiwa  wanne walikamatwa  ambao  ni pamoja na  'hawara'  ya marehemu , wengine  ni Joseph Milumba (31) , Geofrey  Ndenje (27)  na  Grace Sindani (40)  ambaye  inasemekana alimrubuni na  kumtorosha Ritha  kutoka kwa mumewe  na  kumpeleka  kwa Chinga kwa  lengo  la  kumwua.
Inadaiwa  mtuhumiwa  mwingine  ambaye jina lake  halikuweza kupatikana mara  moja  anatafutwa na Polisi  baada  ya  kutoroka na kujificha kusikojulikana  mara  baada ya kufanyika mauaji  hayo .
Kamanda Mwaruanda  alidai  kuwa  bado  jitihada  za kukitafuta kiwiliwili  cha  marehemu  katika Ziwa  Rukwa  zinaendelea  ambapo watuhumiwa  hao wanaendelea  kuhojiwa  na watafikishwa  mahakamani  baada ya  uchunguzi  wa awali wa  shauri lao kukamilika.A

No comments: