HATIMA YA ZITTO KABWE CHADEMA KUJULIKANA HIVI KARIBUNI...

Zitto Kabwe (kushoto) na Dk Willibrod Slaa.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, amesema hawaogopi kuita Baraza Kuu la Chama hicho,  kusikiliza rufaa ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Amesema chama hicho kitaitisha kikao hicho wakati wowote kuanzia sasa, ili kusikiliza utetezi wa
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Akihutubia mamia ya wakazi wa Manispaa ya Iringa na vitongoji vyake katika uwanja wa Mbwetogwa juzi, Dk Slaa alisema Zitto alivuliwa nafasi zake za uongozi ndani ya chama hicho baada ya kubainika amekiuka maadili ya chama.
"Hata ikitokea mimi au Mwenyekiti wangu, Freeman Mbowe au kiongozi au mwanachama yeyote amevunja maadili ya chama, ni lazima atafukuzwa; huu ni utaratibu wa chama na ni lazima usimamiwe," alisema.
Alisema hivi sasa Zitto haruhusiwi kufanya shughuli za kichama kupitia jukwaa la Chadema kwa kuwa si kiongozi tena wa Chadema, rufaa yake haijasikilizwa na kafungua kesi mahakamani.
“Wanachama, wapenzi na wadau wote wa Chadema msimpe ushirikiano wowote Zitto mpaka suala
lake litakapohitimishwa,” alisema.
Alisema Operesheni ya M4C Pamoja Daima, haifanywi na chama hicho kumshughulikia Zitto, inafanywa kama maandalizi ya kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu.
Dk Slaa alitoa kauli hiyo, wakati Zitto kupitia gazeti moja la kila siku, akikaririwa kutangaza kuanza mikutano ya kuzungumza na Watanzania.
“Kama kuna mtu anadhani sitaweza kufanya mkutano wa aina yoyote katika maeneo mbalimbali nchini anajidanganya, nitazunguka kuzungumza na wananchi kwa maslahi ya Taifa hili na ni haki yangu kikatiba,” alikaririwa Zitto.

No comments: