IKULU YAWAJIA JUU WANAOBEZA UTEUZI WA BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI...

Salva Rweyemamu.
Mjadala kuhusu uteuzi wa Baraza la Mawaziri jipya lililotangazwa karibuni hauna maana na ni kupoteza muda, imeelezwa.

Ofisi ya Ikulu imesema mamlaka ya uteuzi wa Baraza la Mawaziri ni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kikatiba ambaye ameifanya kazi hiyo.
Baraza la Mawaziri jipya lilitangazwa Januari 10, na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni  Sefue katika mkutano na waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam.
Akizungumza na mwandishi jana kuhusu mjadala huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema Baraza la Mawaziri ni la ushauri kwa Rais na yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuteua nani anafaa kumshauri na wakati gani.
Alisema maneno yote ambayo yamekuwa yakisemwa kuhusu Baraza hilo, ikiwa ni pamoja na jitihada za kuponda uteuzi wa Rais ni upotezaji muda usiokuwa na nafasi katika nchi inayokabiliwa na changamoto na matatizo mengi ya kimaendeleo kama Tanzania.
Aliongeza kuwa badala ya wananchi na hasa viongozi kupoteza muda kujadili, kuponda na kukejeli uteuzi huo mzuri ambao ulifanywa kwa misingi kamili ya kikatiba, muda huo ungetumika kukabiliana na changamoto na matatizo ya maendeleo yanayoendelea kuikabili nchi.
Rweyemamu alisema wajibu wa Watanzania, na hasa viongozi wakati huu, ni kuunga mkono uteuzi huo na kuwapa nguvu mawaziri wapya ili watoe mchango wao kwa maendeleo ya nchi kupitia ushauri wao kwa Rais pamoja na uamuzi wao mwingine kuhusu masuala mbali mbali.
“Si haki kumhukumu mtu kabla ya kumpa nafasi ya kuonesha uwezo wake ama ukosefu wa uwezo wake.
Kitendo cha kuwashutumu, kuwabeza binafsi na kuwakejeli baadhi ya wateule hao wa Rais ni kitendo cha ubinafsi kwa sababu hakuna mtu yeyote, isipokuwa Rais, anayejua kwa nini ameteua watu hao,” alisema Rweyemamu na kuongeza: “Wakati mwingine unasikiliza mtu anayeshutumu, unaangalia rekodi yake mwenyewe katika uongozi ama ushauri, unaangalia sifa zake na unashangaa kwamba mtu huyo anaweza hata kuwa na ujasiri wa kutoa shutuma za namna hiyo.”
Miongoni mwa viongozi waliokaririwa wakishutumu uteuzi huo ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye alifikia hatua ya kusema Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya hana elimu ya kutosha kushika nafasi hiyo.
Mwingine aliyeshambuliwa na watu mbalimbali wakiwamo baadhi ya wanahabari ni Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia wakidai pia kuwa hana uwezo na kwamba yupo kukandamiza vyombo vya habari.
Hata hivyo, mawaziri hao kwa nyakati tofauti walijibu tuhuma hizo ambapo Mkuya alithibitisha kuwa na elimu ya kutosha, huku Nkamia akiapa kuwa hajateuliwa kukandamiza vyombo vya habari na kamwe hatafanya hivyo.

No comments: