Ndugu na jamaa wakimfariji Paul Mutora hospitalini. |
Wafanyakazi wa mochari ya Hospitali ya Naivasha wakiwa na mshituko walikimbia huku na huko walipoona mwili unajitingisha na kupumua.
Paul Mutora, ambaye alijaribu kujiua kwa kumeza sumu ya kuua wadudu, alithibitishwa kufa Jumatano usiku.
Daktari aliyemhudumia alisema dawa zilizotumika kumtibu zilipunguza mapigo ya moyo, hali inayoweza kuwa imesababisha kosa hilo la kitabibu lililofanyika.
"Hiyo inaweza kuwa imemchanganya daktari, lakini Mutora aliwahiwa kabla hajadungwa sindano ya kuzuia mwili kuharibika," Dk Joseph Mburu, Mganga aliyekuwa zamu katika Hospitali hiyo ya Wilaya ya Naivasha, alikaririwa na gazeti la Standard akisema jana.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, baba wa Mutora na ndugu wengine walifika kwenye mochari Alhamisi asubuhi kuangalia mwili na kurudi nyumbani kuanza maandalizi ya mazishi.
"Lakini mchana tukaarifiwa kuwa yuko hai na tukaondoka kurudi huko kwa mshituko," alisema baba huyo.
Shuhuda aliliambia gazeti la Star kwamba sauti iliposikika ndani ya chumba cha barafu: "Msimamizi wa mochari na mfanyakazi wake walikimbia huku wakipiga mayowe."
Mpigapicha alimpiga picha Mutora akiwa kitandani kwenye wodi ya wanaume katika hospitali hiyo iliyoko mjini humo umbali wa kilometa 90 Kaskazini Magharibi mwa Nairobi.
"Hili ni kosa ambalo lilifanyika tangu awali na naomba radhi kwa baba," alisema mgonjwa huyo.
No comments:
Post a Comment