ASKARI POLISI ADAIWA KUMTOROSHA MFUNGWA MKOANI KIGOMA...

Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limekumbwa na kashfa baada ya askari wake kukutwa na tuhuma za kutorosha mfungwa.

Habari za uhakika ambazo mwandishi amezipata zilieleza kuwa baadhi ya askari wa Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa walikula njama na kumtorosha Bakila Hassan aliyehukumiwa na Mahakama ya Mwanzo Mwandiga kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la wizi wa kuaminika.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Fraisser Kashai amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema tayari maofisa wawili wa Jeshi hilo ambao wanasimamia makabidhiano ya zamu katika kituo hicho, wamefikishwa Mahakama ya kijeshi kujibu tuhuma hizo.
Kamanda Kashai alisema sambamba na kufikishwa mahakamani kwa maofisa hao pia Jeshi hilo linafanya uchunguzi kujua askari zaidi waliohusika na sakata hilo ili liweze kuchukua hatua.
Aidha, Kamanda alisema pamoja na kuchukuliwa hatua kwa watendaji wake, pia ameagiza kuundwa kwa timu itakayopeleleza mahali aliko mfungwa huyo na kumkamata.
Hata hivyo, Kamanda Kashai alikanusha madai ya kuwapo njama ya kutoroshwa mfungwa huyo badala yake akasema ulikuwa uzembe wa watendaji wake uliotoa mwanya kwa mfungwa kutoroka.
Desemba 10 mwaka jana, Hassan alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela na Mahakama hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kuiba kwa kuaminika.
Hakimu Mfawidhi Fred Shayo alitoa hukumu hiyo baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka ulioongozwa na Mara Mashaka. 
Baada ya hukumu, askari waliokuwa na gari la kusafirisha wafungwa na mahabusu walimchukua Hassan na kumpeleka kituo cha Polisi mjini hapa badala ya Gereza la Bangwe ili aanze kutumikia adhabu yake.
Alipofikishwa kituoni askari hao walikula njama za kumtorosha ambapo Desemba 12   aliachiwa na kutoroka.
Baadhi ya watu waliomwona na kumtambua walidai kuwa Desemba 13 alionekana kwenye kituo kikuu cha mabasi ya kwenda mikoani cha Masanga akiwa kwenye basi liendalo Dar es Salaam.

No comments: