SASA MARUFUKU KUUZA KEMIKALI KWA WASIO NA LESENI...

Aina mbalimbali za kemikali.
Wakala wa maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imepiga marufuku uuzaji wa kemikali kwa mtu yeyote asiye na leseni kutoka kwake.

Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali nchini, Sebanito Mtega alisema hatua hiyo inatokana na kukamilika kwa kazi ya kusajili wauzaji na watumiaji wa kemikali nchini, kazi iliyokamilika Novemba 30 mwaka jana.
“ Kwa sasa ni marufuku kwa mtu asiyekuwa na leseni ya matumizi ya kemikali kuuziwa kemikali, na hii imetusaidia sana kuwafanya watu kuja ofisini kujisajili na wengi wao wakiwa ni watengeneza sabuni majumbani,” alisema.
Serikali ilitoa miezi mitatu kuanzia Agosti 16 hadi Novemba 30 mwaka jana kuhakikisha wauzaji wakubwa na warejareja na watumiaji wa kemikali kuhakikisha waagizaji, wasambazaji na watumiaji wa kemikali nchini wanajisajili na kupewa leseni. Lengo  ni kuhakikisha kunakuwa na matumizi salama ya kemikali kwa afya na mazingira.
Hatua hiyo ilitokana na kuongezeka kwa vitendo vya umwagiliaji tindikali kwa watu mbalimbali nchini.
Aidha, Mtega alisema wamekamilisha mapitio ya kanuni na sheria za kemikali za mwaka 2012, kilichosalia ni mapitio hayo kuwekwa sawa na wataalamu wa sheria kabla haijaidhinishwa kwa ajili ya kutumiwa, kudhibiti ajali zitokanazo na kemikali.
Alisema pamoja na mambo mengine, wamependekeza kuwe na adhabu kali zaidi dhidi ya watakaothibitika kutumia kemikali, ikiwemo tindikali kujeruhi wengine na kwamba sheria ya kemikali Na. 3 ya 2003 inayotoa adhabu ya faini kati ya Sh 50,000 kwa mtu hadi Sh milioni 50 kwa kampuni kutegemeana na kosa lililotendwa, ni ndogo ikilinganishwa na athari zinazowapata waathiriwa.
Sheria na kanuni hizi pia zimeangalia wasafirishaji na waingizaji wa kemikali, watumiaji wa viwandani na maabara, wasambazaji, usajili wa maghara na usajili, uteketezaji wa kemikali zilizokwisha muda wake na udhibiti wa kemikali taka zenye madhara.

No comments: