Mwalimu akifundisha moja ya masomo kwa Kiswahili. |
Kwa muda mrefu tangu Uhuru, shule karibu zote za msingi za Serikali zilikuwa zikitumia Kiswahili kufundishia masomo yote isipokuwa somo la Kiingereza.
Baada ya kumaliza shule ya msingi, mwanafunzi alikuwa akibadilisha mfumo ghafla na kuanza kufundishwa masomo yote kwa Kiingereza isipokuwa somo la Kiswahili.
Shule za msingi za Serikali ambazo zilikuwa zikitumia Kiingereza kufundisha masomo yote ni shule za Msingi Olympio na Diamond za jijini Dar es Salaam na Shule ya Msingi ya Arusha, jijini Arusha.
Lakini mwaka huu tayari Shule ya Msingi ya Oysterbay jijini Dar es Salaam, imeanza mchakato wa kuhama kutoka kutumia Kiswahili kufundishia masomo yote na Kiingereza kuwa somo la kawaida, mpaka kufundisha masomo yote kwa Kiingereza, na Kiswahili kuwa somo la kawaida.
Mbali na shule hiyo, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf Mwenda, alisema ziko shule zingine katika Manispaa ya Kinondoni, zimeshapeleka maombi kutaka kuhamia mfumo wa kufundisha masomo yote kwa Kiingereza.
Akizungumza na mwandishi mwishoni mwa wiki, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Oysterbay, Victoria Majesa, alisema wamefuata utaratibu kabla ya kufikia uamuzi huo na wanacho kibali cha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Kwa mujibu wa Majesa, kuna mahitaji makubwa ya shule zinazofundisha kwa Kiingereza na hatua yao, inalenga kupunguza msongamano katika shule zinazotumia Kiingereza jijini Dar es Salaam.
Alisema katika Manispaa ya Kinondoni hakuna shule
ya Serikali iliyo katika mfumo wa Kiingereza kama ilivyo kwa shule za Diamond na Olympio ambazo zote ziko katika Manispaa ya Ilala.
Kutokuwa na shule za aina hiyo katika Manispaa hiyo, kumesababisha wanafunzi wengi kutoka Manispaa hiyo kutafuta nafasi katika shule hizo za Ilala na kusababisha msongamano mkubwa.
Alisema wameanza kwa darasa la kwanza mwaka huu na wataendelea kuondoa mfumo wa kufundisha kwa Kiswahili kila mwaka kadri watakavyokuwa wakisajili wanafunzi wapya.
“Kwa mwaka huu tumeanza na wanafunzi 88 wa darasa la kwanza na lengo lilikuwa ni wanafunzi 100 na kila mwaka mfumo (wa kuondoa matumizi ya Kiswahili) utakuwa ukiendelea kwa kadri tutakavyokuwa tukiandikisha wanafunzi wapya na baada ya miaka sita ijayo, shule itakuwa imebadilika kuwa katika mfumo huo kwa shule yote,” alisema.
Kuhusu utaratibu uliofuatwa, Mwalimu Majesa alisema uongozi wa shule hiyo ulikutana na wazazi pamoja na viongozi wa Manispaa na kujadili mabadiliko hayo.
Baada ya maridhiano, Baraza la Madiwani Kinondoni, lilituma maombi Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambayo kwa mujibu wa Mwalimu Majesa, walipata kibali cha kuanza mfumo huo.
Meya Mwenda alithibitisha kuwa maombi ya mabadiliko ya shule hiyo yalipelekwa mwaka jana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, iliwaletea barua ya kuridhia.
Mwenda alisema kila mzazi anayehitaji nafasi katika shule hiyo, atawajibika kutuma maombi Manispaa ambayo itaangalia uwezo uliopo na kuwapatia nafasi.
Alisema mtoto yeyote wa Dar es Salaam anaruhusiwa kusoma katika shule hiyo, ingawa kipaumbele ni kwa wanafunzi wa Kinondoni.
Kutokana na msongamano huo, alisema Manispaa inaendelea kuombea shule nyingine nyingi zaidi zipewe kibali kama Shule ya Msingi Oysterbay, ili kutoa nafasi kubwa kwa wanafunzi wengi kupata masomo kwa mfumo huo.
Hatua hiyo inapingana na maoni ya Jukwaa la Taasisi na Mamlaka za Udhibiti wa Ubora wa Elimu nchini, ambalo kupitia Mwenyekiti wake, Profesa Sifuni Mchome, lilipendekeza Kiswahili kitumike mpaka vyuo vikuu.
Jukwaa hilo linaundwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), Taasisi ya Elimu Tanzania, Baraza za Mitihani la Taifa (Necta), Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte).
Profesa Mchome, ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, akiwakilisha jukwaa hilo kutoa mapendekezo kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alikaririwa akisema kwamba wamependekeza Kiswahili kitumike kufundishia kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu, ili kukuza kiwango cha elimu nchini.
Alipendekeza kabla ya kuanza kutumika kuwa lugha ya kufundishia, lugha hiyo iandaliwe kitaalamu ili iguse ngazi zote za masomo ambayo yatafundishwa katika taasisi za elimu.
“Tumetaka lugha ya Kiswahili itumike kuwa lugha ya kufundishia kuanzia shule ya msingi hadi sekondari ili kuhakikisha tunakuza lugha yetu.
“Tunataka Katiba mpya itamke kwamba kutakuwa na mipango sahihi kabla ya kuanza kutumika kwa lugha hiyo ya kufundishia ili kuhakikisha inagusa maeneo yote,” alisema Profesa Mchome.
No comments:
Post a Comment