SERIKALI KUILIPA KNCU SHILINGI MILIONI 255 KUFIDIA HASARA...

Ofisi za KNCU.
Serikali imekubali kulipa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU) 1984, Sh milioni 255. 1, kusaidia chama hicho kufidia hasara iliyotokana na mdororo wa uchumi duniani.

Meneja Mkuu wa KNCU 1984, Honest Temba, ameeleza hayo katika taarifa yake aliyotuma kwa vyombo vya habari jana, na kufafanua taarifa zilizochapishwa katika kitabu cha Mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema.
Mrema katika kitabu hicho anadaiwa kudai kuwa KNCU imeidanganya Serikali kwamba wakati wa mdororo wa uchumi duniani, ilipata faida ya Sh bilioni mbili na sio hasara.
Akifafanua madai hayo, Temba alisema KNCU iliiandikia Serikali kufafanua hasara waliyopata ya Sh milioni 255. 1 ambazo zilithibitishwa na Shirika la Ukaguzi wa Mahesabu ya Vyama vya Ushirika (Coasco), na Serikali ilikubali na kuahidi kulipa.
Mbali na madai hayo, Mrema katika kitabu hicho pia anadaiwa kusema kuwa KNCU imekuwa ikiwakopa wakulima, jambo ambalo Temba amekanusha kuwa haliwezi kutokea.
Kwa mujibu wa Temba KNCU, hainunui kahawa, bali inakusanya mazao ya mkulima na kwenda kuyatafutia soko na baada ya kuuza, inarejesha malipo kwa mkulima na kuhoji chama kinawezaje kukopa wakati hakinunui?
Alisema hoja inatakiwa kuwa kuchelewesha malipo badala ya mkopo, na kufafanua kuwa malalamiko hayo, yalitokea baada ya kuanzishwa kwa soko huria, ambapo ushirika ulipambanishwa na kampuni binafsi zilizokuwa zikinunua hapohapo.
“Kelele za kucheleweshwa fedha za makopesho zimeibuka kwa kasi baada ya  kuanzishwa kwa soko huria kwani ushirika umeingia katika mfumo huo kwa kushtukizwa na hauna nguvu za fedha za wanunuzi binafsi.
“Japokuwa fedha zinachelewa lakini hakuna mkulima anayedai  zaidi ya wiki mbili au tatu,” alisema Temba na kumtaka Mrema kufika ofisini kwao apewe ufafanuzi.

No comments: