PINDA ARIDHISHWA NA KAZI YA UTANDAZAJI WA BOMBA LA GESI...

Mafundi na wataalamu wa kigeni wakiendelea na kazi ya utandazaji bomba la gesi.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema kazi ya kutandaza mabomba ya gesi itokayo Mtwara kwenda Dar es Salaam itakamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Pinda, ambaye jana alikagua ujenzi wa bomba hilo unaofanywa na Kampuni ya Mafuta ya China (CNPC) alisema wataalamu wamemhakikishia kuwa ujenzi utakamilika kwa muda uliopangwa wa miezi 18.
Alisema asilimia 81 ya mabomba yameshawasili eneo la mradi kutoka China. Idadi ya mabomba inayohitajika ni 440, hali ambayo alisema inamfariji kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati.
Aliongeza kuwa mabomba zaidi ya nusu (kilometa 265 ) yameshaunganishwa kati ya kilometa 542 ambazo ndio umbali wa Mtwara hadi Dar es Salaam.
Mtaro ambao umechimbwa hadi sasa ni kilometa 114 kazi ambayo Pinda alisema inaendelea vizuri na inasimamiwa na wataalamu wazuri kutoka Afrika Kusini na nchini.
Kuhusu ubora wa mabomba, Pinda alihakikishiwa na mtaalamu mwelekezi anayesimamia mradi huo kuwa yana ubora wa hali ya juu.
"Hili la ubora linatuhakikishia tusiwe na wasiwasi, kwani hawa wataalamu wamekwenda hadi China, kukagua utengenezaji wa mabomba haya na kuridhika na ubora wao," alisema Pinda.
Aliongeza kuwa uhai wa mabomba hayo chini ya ardhi ni miaka 30, na yakifanyiwa matengenezo yana uwezo wa kudumu miaka 50 hadi 70. Jambo ambalo linaonesha mradi utadumu kwa miaka mingi.
Awali akimpa maelezo Waziri Mkuu, Mhandisi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Baltazar Mroso alisema kati ya kazi zinazofanywa ni kuweka zege kwenye mabomba yatakayotandazwa baharini umbali wa kilometa 25.
Alisema asilimia 85 ya kazi ya kutandaza mabomba inafanywa na Watanzania, hivyo mradi umesaidia kuongeza ajira nchini.
Pinda alikagua kiwanda cha kusiliba mabomba baharini na ya maeneo ya ardhi oevu kwa saruji, alitembelea maeneo wanayochimba mtaro wa mabomba, alikagua eneo linapoibukia bomba la baharini litokalo Songosongo na sehemu mabomba yanakopindwa.

No comments: