KAGASHEKI AIPONDA RIPOTI YA OPERESHENI TOKOMEZA UJANGILI...

Balozi Khamis Kagasheki akitangaza kujiuzulu wadhifa wake bungeni mjini Dodoma.
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki amekosoa ripoti ya Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira akidai ilikuwa ya upande mmoja kwani haikuonesha mauaji ya  askari waliohusika katika Operesheni Tokomeza Ujangili.

Aidha, ameshangaa walioshangilia kujiuzulu kwake na baadaye uwaziri wake kutenguliwa na Rais Jakaya Kikwete, akisema kujiuzulu ni jambo la kawaida na kwamba angejisikia vibaya kama angeondolewa wizarani kwa sababu za ufisadi au wizi wa mali za umma.
Kagasheki, ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Mjini, alisema hayo juzi katika viwanja vya Mashujaa kwenye mkutano wa hadhara alioutumia kueleza mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uamuzi wake wa kujiuzulu kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii kutokana na matatizo yaliyoibuka wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili, mwaka jana.
Akiizungumzia ripoti hiyo, alisema: "Katika operesheni hiyo maalumu watu waliumizwa, ambapo katika ripoti ya Lembeli (James Lembeli, Mbunge wa Kahama na Mwenyekiti wa Kamati)  ilionesha kuwa watu 10 waliuawa, jambo ambalo lisingempendeza mtu yeyote.
"Lakini katika operesheni hiyo, askari wapatao sita walikufa ila hiyo hatukuisema. Tukumbuke kuwa nao ni binadamu kama sisi, pia katika sakata la kuua tembo, wamo watu wengi wenye uwezo wa kifedha hata baadhi ya wabunge pia wanahusika, kwa hiyo kazi ya kupambana na watu hao inahitaji umakini sana.
"Kutokana na vitendo vya mauaji na unyanyasaji vilivyofanyika katika operesheni hiyo, mimi nikiwa Waziri mwenye dhamana, niliamua kuwajibika kisiasa kwa kujiuzulu, kwani kufanya hivyo ni jambo la kawaida ila nilishangaa kuona baadhi ya watu wanashangilia na kufurahia mimi kuondoka katika wizara hiyo.
"Mungu humpandisha ampendaye na pia humshusha vivyo hivyo kwa mwenye nchi (Rais) humpa uwaziri anayeridhika naye na kumwamini sijaumizwa, labda ningetoka kwa kashfa ya ufisadi au wizi wa mali ya umma, hilo lingeniumiza sana."
Alisema kujiuzulu uongozi ni jambo la kuonesha ukomavu, akitolea mfano kuwa, hata Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alipata kujiuzulu lakini kutokana na uungwana wake, baadaye aliaminiwa na kupewa jukumu la kuiongoza nchi kwa miaka 10.
"Ila tatizo kama hilo limejitokeza tena hivi sasa ambapo tembo wamepungua katika pori hilo kutoka 70,000 na kufikia 13,000, jambo ambalo linatishia kutoweka kabisa kwa wanyama hao," alisema Balozi Kagasheki na kuongeza, kuwa siku zote amekuwa akipigania maendeleo na haki za wananchi, wakiwamo wa jimboni mwake.
Mbali ya Balozi Kagasheki, wengine waliopoteza nafasi zao za uwaziri kutokana na kadhia iliyotokana na Operesheni Tokomeza Ujangili ni aliyekuwa wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo David.
Kwa sasa, nafasi ya Kagasheki imeshikwa na aliyekuwa Naibu wake, Lazaro Nyalandu aliyepandishwa cheo na Rais Kikwete.
Aidha, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe amehamishiwa Mambo ya Ndani ya Nchi kuchukua nafasi ya Dk Nchimbi, huku Dk Hussein Mwinyi aliyekuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii akirejeshwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, alikopata kuongoza kwa vipindi tofauti. Nafasi ya Dk Mathayo imezibwa na Mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani.

No comments: