BARABARA YA MOROGORO-DODOMA SAFI, MKULIMA AKWAMA JUU YA MTI KWA SAA SABA...

Magari ya mizigo kutoka pande zote barabara ya Morogoro- Dodoma, yakipita kwenye daraja la Mkundi - Magole, wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro, baada ya jana asubuhi kukamilishwa na kuruhusiwa kupita kwa zamu kila upande.
Magari yaliyokuwa yamekwama kwa siku tatu kuanzia Januari 22, kwenye barabara kuu ya Morogoro - Dodoma, baada ya daraja la Mkundi eneo la Magole, wilayani hapa kuharibiwa na mafuriko, yalianza kupita jana asubuhi baada ya matengenezo ya muda kukamilika.

Mbali na malori, pia mabasi yaliyokuwa yakitoka Dodoma nayo yalipita eneo hilo, baada ya gari la kwanza kuruhusiwa saa 4:30 asubuhi, siku mbili baada ya kuanza matengenezo yaliyopangwa kuchukua siku nne hadi kesho, kazi iliyozinduliwa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana eneo la Magole, Mkuu wa Mkoa  wa Morogoro, Joel Bendera alimpongeza Waziri Magufuli kwa kusimamia kazi hiyo usiku na mchana hadi kukamilika ndani ya siku mbili tofauti na makadirio ya awali ya siku nne.
Mkuu wa Mkoa pia alishukuru wahandisi wa Kichina kutoka kampuni ya ujenzi ya CCECC kwa kutoa msaada wa magari ya kusomba mawe na kujaza eneo la meta 40 la tuta lililobomolewa na mafuriko kwa upande wa Morogoro na meta 10 upande wa Dodoma wa daraja hilo, hali iliyosababisha kukwama kwa usafiri hasa wa malori.
Mkulima mkazi wa kijiji cha Magole, wilayani hapa, amenusurika kifo  baada ya kusombwa na mafuriko umbali wa meta 225 akiwa shambani  eneo la Feri Magole na kunasa kwenye  mti wa myegeya na kuning'inia kwa saa saba. 
Khatib Bakari (30), ambaye mara nyingi hushinda shambani akilima na kulinda mazao yake hasa mahindi mabichi na minazi, siku hiyo alilala kibandani kwenye mashamba ya ndugu zake na kukutwa na majanga hayo usiku wa manane wa kuamkia Januari 22.
Baada ya kubainika amesombwa na mafuriko na kunasa kwenye mti na kujiokoa alfajiri, mamia ya wananchi wa kijiji cha Magole, walifika eneo hilo kumshuhudia mwenzao huyo akiwa mtini bila nguo  ambazo maji ya mafuriko yalimchojoa.
Hata hivyo, baada ya kuona umati wa watu ukimwangalia alijificha kwenye matawi ili kujisitiri ingawa alikuwa umbali mrefu kutoka barabara ya Magole - Turiani.
Mwandishi wa habari hizi na viongozi wa serikali ya wilaya ya Kilosa na Mkoa wa Morogoro, akiwamo  Mkuu wa Mkoa, Joel Bendera, na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, walimwona mtu huyo akiwa mtini huku chini maji yakipita kwa kasi.
Hata hivyo, viongozi hao akiwamo Mkuu wa Mkoa, walitoa ushauri wa kutafuta namna ya kumwokoa   baada ya kukaa mtini kwa saa nyingi.
Kutokana na mwito huo, watu 18 walijitokeza na kamba na madumu matupu ya plastiki, kwenda kumwokoa ambapo walipiga mbizi na kumfikia na kufanikiwa kumwokoa majira ya saa 9 alasiri baada ya saa mbili za kazi.
Akizungumza baada ya kuokolewa, Bakari alimshukuru Mungu kwa kumlinda, pia wanakijiji wenzake waliojitokeza kumwokoa juu ya mti katikati ya mafuriko.
"Maji yalifika eneo la kibanda changu saa saba usiku nimelala, nilishituka maji yamejaa na kukosa sehemu ya kupita, nikasombwa umbali wa ekari tatu za shamba, Mungu ni mkubwa, nilinasa kwenye mizizi ya mti wa myegeya, nikapanda juu bila nguo - zilichojolewa na maji," alisema kwa masikitiko.
Bakari ambaye hana mke wala mtoto, alisema anaishi na ndugu zake kijijini hapo na shughuli zake ni  kilimo, hivyo mara zote hushinda shambani.
Juzi baada ya maji kupungua, wananchi walikuwa katika hekaheka za kusafisha na kutoa mabaki  ya maji na taka kwenye nyumba zao, na wengine kwenye nyumba za ibada ukiwamo Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Magole.

No comments: