MILIONI 10/- ZAKWAMISHA SHEKHE KWENDA INDIA KWA MATIBABU...

Shekhe wa Mkoa wa Mara, Athuman Magee, amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa takribani wiki moja sasa akisumbuliwa na matatizo ya pingili za uti wa mgongo huku shilingi takriban milioni 10 zikikosekana ili kumpeleka India kwa matibabu.

Kwa mujibu wa ndugu wa karibu wa Shekhe huyo ambaye amekuwa akiongoza mkoa wa Mara tangu mwanzoni mwa miaka ya sabini. Shekhe Magee anatakiwa kwenda kutibiwa India kutokana na maelekezo ya madaktari.
Ndugu ambaye hakutaka jina lake litajwe alimwambia mwandishi kwamba tangu Shekhe huyo aanze kuugua, hawajapata msaada wa maana kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) licha ya kuwapa taarifa.
Alisema mpaka sasa michango inayotokana na ndugu imefikia Sh milioni 6 wakati kiasi kinachotakiwa ili kumpeleka India si chini ya Sh milioni 16.
"Bakwata Mkoa wa Mara wametupa Sh 175,000 ingawa waliahidi kuchangia Sh milioni tano. Hata hivyo tunawashukuru kwa hilo. Tunawashukuru pia Answar Sunna mkoa wa Mara ambao walichangia Sh 400,000 licha ya kuwajulisha kwa muda mfupi wakati tukimleta Shekhe Muhimbili," alisema ndugu huyo.
Ndugu huyo alisema juzi walikwenda Bakwata  makao makuu kuwaeleza tatizo la Shekhe Magee, lakini hawakupewa ahadi yoyote 'inayoeleweka'.
"Lakini tunashukuru juzi hiyo hiyo walikuja hapa kumwombea dua, kisha wakaondoka," anasema.
Alisema mbunge wa mkoa wa Mara aliahidi kuchangia gharama za kumpeleka Shekhe Magee India, lakini kwa sasa inaonekana kama alinukuliwa vibaya.
"Yaani hapa tumechanganyikiwa. Hatujui tufanyeje."
Msemaji wa Bakwata, Ustaadh Shabani Simba alipopigiwa simu na mwandishi, alisema yuko likizo akaomba apigiwe Katibu Mkuu wa Bakwata, Suleiman Lolila.
Naye Lolila alipopigiwa simu, mazungumzo yalikuwa ifuatavyo baada ya salamu:
Mwandishi: Ninaulizia mustakabali wa Shekhe Athumani Magee, Shekhe wa Mkoa wa Mara. Je, mna habari zake sahihi?
Lolila: Kwani wewe kama mwandishi anakuhusu nini?
Mwandishi: Nisikilize kwanza utajua kwa nini ninakuuliza. Ni kwamba, kwa mujibu wa ndugu zake anatakiwa akatibiwe India na hivyo kuna suala zima la....
Lolila: (akimkatisha mwandishi) Kwani wewe ni daktari na ndiye unayeamua kwamba akatibiwe India?
Mwandishi: Naomba unisikilize kwanza nimalize...
Lolilila: Mimi ninaingia msikitini. Nipigie baadaye.
Lolila alipopigiwa baadaye, kwa simu ya mezani alidai hasikii vema, na alipopigiwa muda huo zaidi ya mara nne kwa simu ya mkononi hakupokea.

No comments: