Sipora Liana. |
Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo amegonga mwamba baada ya Liana kupuuza agizo lake alilotaka litekelezwe ndani ya siku sita.
Mulongo mwishoni mwa Desemba, alimtaka Liana aombe radhi kwake, kwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela na Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo kwa madai ya kuwadharau, lakini hadi jana hajafanya hivyo.
Mulongo alisema katika kikao hicho cha kutathimini miradi inayotekelezwa chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, kuwa Liana asipoomba radhi atakuwa tayari kumpisha mkoa.
Wakati Mulongo akisubiri kauli ya Liana kuomba radhi, jana Mkurugenzi huyo alionesha nguvu, alipoamuru wakuu wa idara na watendaji wa Halmashauri, wasuse kikao cha Baraza la Madiwani.
Kabla ya kuamuru watendaji kususa Baraza, Liana akiwa katika kikao hicho, Diwani Cyprian Tarimo aliomba kikao kibadilike kuwa Kamati ili kujadili tuhuma zinazomkabili Mkurugenzi huyo kutoka kwa madiwani.
Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji, Prosper Msofe, alitoa fursa kwa madiwani kupiga kura ya kukubali au kukataa hoja hiyo, ndipo madiwani wakaafiki Mkurugenzi ajadiliwe.
Baada ya maafikiano hayo, Liana alisimama na kuamuru wakuu wa idara na watendaji wote wa Halmashauri watoke nje ya kikao hicho.
Akizungumzia hali hiyo, Msofe alisema walibadilisha Baraza kuwa Kamati kwa kufuata kanuni ya 13(a) na kanuni ya 2 ambazo zinaruhusu kama madiwani wana jambo la kulishughulikia wafanye hivyo.
"Sisi tumefuata kanuni na sheria, lakini hatukufanikiwa kuendelea na kamati kwa sababu Katibu kisheria ni Mkurugenzi ambaye amezira kwa sababu zake, ila tulichofanya tumeandika malalamiko yetu na kupeleka kwa Mkuu wa Mkoa," alisema Msofe.
Alisema wakiwa katika Kamati hiyo, walituma wenyeviti wa kamati mbili ya Mipango Miji na Uchumi, Elimu na Afya wakamwite Mkurugenzi aje kusikiliza kero za madiwani, akatoa jibu kwa maandishi kuwa hawawezi kumjadili na kimsingi kikao hicho ni batili.
"Sasa kama sisi tumejibiwa hivyo, basi tumeandika malalamiko yetu na yatakwenda kwa Mkuu wa Mkoa kama sheria inavyosema," alisema Msofe.
Meya Lyimo, alisema Baraza lilipoanza alikuwa akiaga mwili wa kijana aliyefariki dunia Mererani ambaye ni jirani yake na alimruhusu Naibu Meya kuendelea na kikao.
Alisema alipomaliza kuaga, alikwenda kwenye Baraza hilo na kukuta limebadilika kuwa kamati.
"Sasa kama kimsingi Mkurugenzi alitakiwa kujibu hoja za madiwani na yeye akakimbia, basi sisi tumeorodhesha kero zetu na tutapeleka kwa Mkuu wa Mkoa ambaye ana mamlaka ya kuitisha kikao cha dharura cha Baraza na hapo mtasikia yote," alisema Lyimo.
Aliongeza kuswa Mkuu wa Mkoa yupo kwa niaba ya Rais na hivyo wanatarajia yote yafanyike, ili watendaji wote wawekane sawa.
"Mnajua hapa hatuwezi kufanya kitu chochote na hatuwezi kuitisha tena kikao chochote bila Mkuu wa Mkoa kufanya hivyo, kwa sababu hapa viongozi tuna tofauti za kiutendaji na ni tatizo," alisema Lyimo.
Kuhusu kutoelewana kwake na Mkurugenzi wa Jiji, Lyimo alisema hana ugomvi ila ana tofauti za kiutendaji na wangependa wawekwe sawa ili wafanye kazi.
Diwani wa Sokoni One, Michael Kivuyo, alisema Mkurugenzi amedharau madiwani kiasi cha kuwaandikia barua kuwa hawawezi kumjadili, wakati uwezo wa kumjadili wanao, ila uamuzi utatolewa na mamlaka zingine.
"Sisi tuna uwezo wa kumjadili na leo tumejadili kero zake kwetu ila kuna mamlaka za kutoa uamuzi," alisema Kivuyo.
Waandishi walipojaribu kwenda kwenye ofisi za Mkurugenzi kusikiliza upande wake, hakutaka kuonana nao na badala yake alituma mjumbe aliyedai kuwa hahitaji kuzungumza na yeyote na hana cha kusema.
No comments:
Post a Comment