Amatus Liyumba. |
Liyumba alikuwa anakabiliwa na kesi ya kukutwa na simu wakati alipokuwa gerezani kutumikia kifungo chake cha miaka miwili baada ya kupatikana na hatia ya kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma.
Hakimu Mkazi Augustina Mmbando alimwachia Liyumba kwa kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya mshitakiwa bila kuacha shaka.
Alisema mshitakiwa anaachiwa huru kutokana na upelelezi kuwa dhaifu na uzembe wa Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda wa kutowasilisha kielelezo cha simu mahakamani, ambacho ndiyo msingi wa kesi hiyo.
Hakimu Mmbando alisema Shahidi Warder Patrick alivyofika mahakamani kutoa ushahidi, aliitambua simu ambayo alidai alimkamata nayo mshitakiwa lakini Wakili Kaganda aliomba ipokewe kama utambulisho kwa kuwa alikuwa anaitumia kwa ajili ya kufanya upelelezi lakini hakuiwasilisha mahakamani kama kielelezo.
Alisema simu hiyo haikupaswa kupokewa mahakamani kama utambulisho kwa kuwa aliyetakiwa kuomba ni shahidi na siyo Wakili, mahakama ilipokea simu kama utambulisho, lakini haiwezi kuipa uzito kama sehemu ya ushahidi kwa kuwa ni makosa kisheria kutumia maelezo kama kielelezo.
Aidha, alisema upande wa Jamhuri ulitakiwa kuthibitisha kama kweli hiyo simu ni ya mshitakiwa, lakini pamoja na kudai walifanya uchunguzi hawakuwasilisha mahakamani ripoti ya uchunguzi uliobaini mmiliki wa namba ya simu iliyotumika.
"Inawezekana Liyumba alikamatwa akiwa na simu gerezani lakini kutokana na upelelezi kuwa dhaifu na upande wa Jamhuri kushindwa kuwasilisha kielelezo cha simu kama sehemu ya ushahidi, mahakama inamwachia huru," alisema.
Liyumba alitoka mahakamani na kukwepa waandishi wa habari, wasimpige picha kwa madai wana picha zake nyingi, ingawa walifanikiwa kumpiga picha.
Ilidaiwa kuwa Julai 27 mwaka juzi, Liyumba akiwa mfungwa katika Gereza la Ukonga, alikutwa na simu aina ya Nokia 1280 nyeusi yenye laini namba 0653004662.
Liyumba alisomewa mashitaka hayo wiki mbili kabla ya kumaliza kifungo chake, ambapo Septemba 23 mwaka juzi alitoka gerezani baada ya kumaliza kutumikia adhabu yake ya kifungo cha miaka miwili.
No comments:
Post a Comment