MAMIA YA WAOMBOLEZAJI WASHIRIKI MAZIKO YA JAJI LIUNDI...

Jeneza lenye mwili wa Jaji George Liundi likiingizwa kaburini.
Mke wa marehemu akiweka shada la maua kwenye kaburi la mumewe Jaji Liundi.
Mtoto mkubwa wa marehemu, Taji Liundi na mkewe wakiweka shada la maua kwenye kaburi la baba yao.
Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza mamia ya waombolezaji katika kuuaga na maziko ya Msajili wa Kwanza wa Vyama vya siasa, George Liundi aliyeelezewa kuwa msingi wa Demokrasia nchini.

Aidha, baadhi ya wanasiasa wamemwelezea Liundi kuwa  muasisi wa Demokrasia, ambaye misingi yake haiwezi kuvunjika, ambaye wakati akiwa  Msajili alifuata sheria na taratibu bila kuyumbishwa.
Shughuli za maziko zilizofanyika katika Viwanja vya Karimjee na baadaye maziko katika Makaburi ya Chang'ombe,  zilihudhuriwa Pia na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Kwanza Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na mawaziri wakuu wastaafu, Jaji Joseph Warioba na Salim Ahmed Salim.
Pia, alikuwepo Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, Pius Msekwa, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana  na viongozi wa vyama vya siasa.
Ibada ya maziko iliongozwa na Kateksita, Lebaratus Nyawa wa Kanisa Katoliki Parokia ya ChangÕombe, aliyetaka viongozi kuishi maisha ya kumcha Mungu ili kufanya kazi kwa uadilifu.
Alisema anafurahi anaposikia  viongozi wa nchi wakiwa kanisani au katika misikiti, kwani wanaonesha uadilifu wao. Alitaka kila mmoja kwa nafasi yake, kumtafuta Mungu kila kukicha wakishika amri za Mungu.
Akizungumza kwa niaba ya vyama vya siasa , Mwenyekiti wa chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema alipokuwa msajili alikuwa makini kwa kufuata sheria, kwani hata watu wakubwa waliotaka kusajili vyama bila kufuata taratibu aliwakatalia.
Makaidi alisema alipokuwa Msajili ofisi yake ilikuwa ndogo, licha ya kuwa na cheo kikubwa, lakini alikuwa wa kawaida.
Aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa baada ya Liundi, John Tendwa alisema Liundi aliweka misingi ya demokrasia nchini ambayo haiwezi kuvunjika bali inaboreshwa tu.
Kutokana na misingi hiyo aliifanya nchi kuwa kinara cha demokrasia nje ya nchi hasa zile za SADC na kutaka kufuata nyayo zake hasa katika misingi aliyoiacha.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge,Wiliam Lukuvi alisema Liundi ameitumikia Serikali kwa miaka zaidi ya 60.
Alisema ndiye alikuwa Mtanzania  wa Kwanza Mwandishi wa Sheria na Muasisi wa Mfumo wa vyama vingi vya siasa aliyeanzisha bila kujifunza popote ambapo misingi yake inatumika hadi sasa.
Mjukuu wa Liundi,  Upile Taji Liundi (18) akisoma wasifu wa babu yake alisema alizaliwa mwaka 1938 katika Kijiji cha Chitowe Masasi Mkoa wa Mtwara na kusoma katika Shule ya Msingi Lukuledi mwaka 1953 hadi 1954.
Alisema mwaka 1955 hadi 1956 alisoma Shule ya Hubeya na mwaka 1957 hadi 1962 alimaliza kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Francis kwa sasa Pugu.
Alisema mwaka 1963 hadi 1966 alimaliza shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, kwa sasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
Akielezea kazi alizowahi kufanya alisema alikuwa Wakili wa Serikali mwaka 1968 mkoani Mwanza na baadaye Mwandishi wa Sheria wakati akiwa Naibu Mwanasheria wa Serikali na kushiriki kuandika Katiba ya Muungano ya mwaka 1977 inayotumika hadi sasa.
"Pia alishiriki kuandika Katiba ya nchi za Zimbabwe na Namibia zinazotumika  mpaka sasa," alisema.
Upile alisema  alifunga ndoa na mkewe Agness na kubahatika kupata watoto saba ambapo kati yao, wanne walifariki dunia na kubaki watoto watatu.
Alifariki kwa ugonjwa wa  Shinikizo la Damu uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.

No comments: