HIVI NDIVYO NOAH ILIVYOUA WATU 13 SINGIDA NA BASI KUUA WATU 13 LINDI...

Wasamaria wakisaidia kutoa miili ya abiria waliokufa katika ajali hiyo Singida jana.
Watu wamekufa na wengine 26 kujeruhiwa katika ajali mbili tofauti  za barabarani zilizotokea jana, Singida na Lindi.

Ajali ya kwanza iliyoua watu 13 papo hapo na mmoja kujeruhiwa, ilitokea jana asubuhi, baada ya gari dogo la abiria aina ya Toyota Noah walilokuwa wakisafiria, kugongana uso kwa uso na lori la mizigo eneo la Isuna, barabara kuu ya Singida-Dodoma.
Ya pili ni iliyoua watu 13 na kujeruhi wengine 25 baada ya basi la Al Hamdullilah  walilokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Mtwara, kuacha njia na kupinduka mtaroni saa 7.30 mchana.
Waliokufa na kutambuliwa katika ajali ya kwanza ni Haji Mohamed (29), mkazi wa Msisi, Singida; Salma Omar wa Itigi, Manyoni; Mtunku Rashid (68), Swalehe Hamis (28), Nyamumwi Omari (10) na Samir Shaban (20) wote wa Saranda, Manyoni.
Wengine ni Mwareki Nkuwi (35) wa Ikungi, Athman Kalemba (38), Ramadhan Mkanga na Omar Shaban wa Saranda na wengine watatu ambao hawakutambulika mara moja.
Majeruhi ambaye amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya mkoa, jina lake pia halijafahamika. 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alisema mjini hapa jana kuwa ajali hiyo ilitokea saa 2 asubuhi ikihusisha lori namba T 687 AXD aina ya Scania mali ya Mussa Transport ya Dar es Salaam na Noah namba T730 BUX, mali ya Mbua Ndofo wa Ikungi, Singida.
Alieleza kuwa Noah ilikuwa inatoka Itigi kwenda Singida wakati lori likitoka Mwanza kwenda Dar es Salaam likiwa na shehena ya samaki wabichi.
Kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, chanzo cha ajali hiyo kinaweza kuwa ni uzembe na mwendo kasi na baada ya ajali kutokea, dereva wa lori na utingo wake walikimbilia kusikojulikana.
Kuhusu ajali ya pili, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga, alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kuongeza kuwa basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Ali Hamza.
Akisimulia kuhusu ajali hiyo, abiria wa basi hilo aliyepata majeraha mkononi, George Steven alidai kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na mvua iliyokuwa inanyesha iliyosababisha  dereva asione vizuri mbele.
Kabla ya kupinduka, Steven alidai basi hilo liliyumba na kuvamia  mtaro na kupinduka na kuungwa mkono na abiria mwingine Joseph Francis.
Nako huko Mbeya ajali nyingine imehusisha magari zaidi ya matano  ambapo inadaiwa gari moja liligonga magari mengine matano.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Parseko Kone, kutokana na vifo hivyo.
"Nimeshitushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya watu 13 akiwamo mtoto wa miezi minne vilivyotokea katika eneo la ajali, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Itigi kwenda Singida kugongana uso kwa uso na lori eneo la Isuna," alisema Rais Kikwete katika taarifa ya Ikulu iliyotumwa jana. 
Rais alisema inatia simanzi kuona ajali zikiendelea kutokea na kupoteza maisha ya watu wasio na hatia hususan mtoto mdogo kama huyo wa miezi minne, kusababisha ulemavu wa kudumu kwa baadhi ya watu na uharibifu wa mali kutokana na makosa ya binadamu katika uendeshaji wa vyombo vya moto.
"Kutokana na ajali hiyo ya kusikitisha, ninakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Singida, salamu zangu za rambirambi kutokana na msiba huo, na kupitia kwako, naomba unifikishie salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo.
"Nawaomba wanafamilia wawe na moyo wa uvumilivu, subira na ujasiri hivi sasa wanapougulia machungu ya kupotelewa na ndugu zao," alisema Rais Kikwete kwa masikitiko.
Aidha, Rais alimwomba Mwenyezi Mungu, azipokee na kuzilaza mahali pema peponi roho za marehemu wote, na aliwahakikishia wafiwa kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huo mkubwa.
Vilevile alimtakia ahueni kijana majeruhi wa ajali hiyo aweze kupona haraka na kurejea katika hali ya kawaida na kuungana tena na ndugu na jamaa zake. 
Hizi ni ajali mbili kubwa za kwanza kutokea barabarani na kuua watu wengi tangu kuanza kwa mwaka huu.

No comments: