MENGI ATOA UFAFANUZI KUHUSU VITALU VYA UCHIMBAJI GESI...

Reginald Mengi.
Mwenyekiti wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Reginald Mengi, amesema sekta hiyo nchini haina nia ya kutaka vitalu vya gesi wapewe Watanzania binafsi, ila Serikali iwape Watanzania ambao wamejiunga kwenye makundi ili wapanue wigo wa umiliki.

"Sisi tunataka vitalu vimilikiwe sio na mtu mmoja mmoja mzawa, tunataka vimilikiwe na kampuni au vikundi vya Watanzania na hasa wazawa," alisema Mengi wakati akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake.
Alisema kampuni hizo, zitauza hisa zake kwa Watanzania ili wananchi wote wapate fursa ya kushiriki. "Hii ndio njia ambayo hata mtu mwenye hali ya chini ataweza kushiriki katika uchumi wa gesi," alisema.
"Mimi napinga kwa nguvu zangu zote mtu binafsi au mtu mmoja kumiliki kitalu cha gesi kwa sababu gesi asilia ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Watanzania wote na si kwa Watanzania wachache," alisema Mengi.
Alikuwa anazungumzia uamuzi wa sekta binafsi, kufanya mpango wa kuitisha vikao na viongozi wa dini ili kuwaelimisha msimamo wa sekta hiyo juu ya ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa gesi. Alisema wamechukua hatua hivyo kwa vile wizara ya nishati na madini tayari imeitisha mkutano na viongozi hao.
Mengi alisema hoja kwamba Watanzaia hawana mtaji sio sahihi kwani yeye binafsi anaamini kwamba gesi yenyewe ni mtaji tosha kwa Watanzania ambayo thamani yake ni zaidi ya mara tano ya fedha watakazoleta wageni.
Alisema cha kusikitisha zaidi ni kwamba fedha watakazoleta wageni watarudishiwa mara baada ya gesi kuanza kuzalishwa. Alisema kwa maana nyingine hizo fedha ni kama mkopo kwa Watanzania ambao itabidi izirudishe mara baada ya uzalishaji wa gesi kuanza.
Alisema wageni ambao wataleta fedha sio mtu mmoja mmoja ni watu ambao wamejiunga wengi wakiwa na hali ya zawaida kabisa kama ilivyo Watanzania wengi.
Alisema kitu kama hicho Watanzania wataweza kufanya na pale ambapo Watanzania watakosa uwezo Serikali inatakiwa kuwawezesha kama inavyoelekeza sera na sheria ya taifa ya uwezeshaji kiuchumi.

No comments: