![]() |
| Vijana hao wameandamana kwa kile kinachodaiwa ni kupinga adhabu aliyopewa Kabwe Zitto (pichani) na uongozi wa Chadema. |
Wakati
Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa
akiendelea na ziara yake wilaya ya Kasulu mkoani hapa, wanachama na wapenzi wa
chama hicho, wamefanya maandamano makubwa ya kumtaka asikanyage wilaya ya
Kigoma.
Katika maandamano hayo, yaliyohusisha pikipiki za
bodaboda zaidi ya 100, magari, midundiko na magari yenye vipaza sauti jana,
wanachama hao walioanzia maandamano yao nyumbani kwa Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe eneo la Mwandiga walitembea umbali wa kilometa nane hadi
viwanja vya Mwanga Centre.
Wakati wote wakiwa katika maandamano hayo, waliongozwa na askari wa usalama barabarani
huku gari la Polisi lenye askari zaidi ya wanane, likiwafuatilia kulinda
usalama.
Wakitoa matamko baada ya kufika kwenye viwanja
hivyo, baadhi yao waliojitambulisha kuwa viongozi wa Baraza la Vijana la
Chadema (BAVICHA) wilaya za Kigoma Mjini na Vijijini, walimtaka Dk Slaa
asitishe ziara hiyo ili kuepusha walichokiita maafa makubwa.
Mtoro Jafari ambaye alijitambulisha kuwa kiongozi wa
BAVICHA Kigoma Kaskazini, alisema vijana hawakubaliani na uamuzi ya Kamati Kuu
ya Chadema ya kumvua Zitto uongozi na kisha Dk Slaa kufanya ziara Kigoma.
“Chadema walichofanya ni sawa na jambazi kuua mtoto
wako baadaye arudi kukupa pole wakati ukijua aliyemwua ni yeye, Dk Slaa anakuja
kutusanifu na hatukubaliani na hilo, tunamwomba akatize ziara yake, aende mikoa
mingine si Kigoma, kama ataendelea na ubishi basi ajue kitu kibaya kitamtokea,”
alisema Mtoro.
Samuel Mzigama ambaye ni kiongozi wa BAVICHA Kigoma
Mjini, alisema Zitto ndiye kila kitu kwao na ndani ya Chadema walimfuata yeye
na si chama, kwani kimejaa ukabila kwa watu wa Kaskazini na anapojitokeza mtu
wa mikoa mingine hufanyiwa fitna na kuondolewa kama alivyoondolewa Zitto.
Baadhi ya waandamanaji walibeba mabango yenye ujumbe
kwamba ‘Zitto kwanza, Chadema baadaye’;
‘Hatutaki chama cha Wachaga kituvuruge’; ‘Kigoma ni chuo cha siasa tunajua
kudai haki zetu’; ‘Zitto ni mkombozi wa Watanzania’ na ‘Wachaga mna radhi ya
Nyerere’.
Stumai Omari kiongozi wa Baraza la Wanawake la
Chadema (BAWACHA) Kigoma Kaskazini alisema
Zitto ataendelea kuwa mtetezi wa Watanzania na hila za Dk Slaa na
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kudhoofisha juhudi zake hazitafanikiwa.
Baada ya hotuba za viongozi hao, wanachama na
wapenzi walioshiriki maandamano walikusanya na kuchoma kadi na bendera za
Chadema huku wakiimba kuwa chama hicho kinawavuruga. Hatimaye msafara huo wa
bodaboda na mdundiko ulirudi Mwandiga nyumbani kwa Zitto.
Viongozi wa Chadema Kigoma ambao hawakushiriki ziara
ya Dk Slaa kwa kutoa udhuru hawakupatikana kuzungumzia hali hiyo na ziara
nzima.
Akizungumza na mwandishi, Kaimu Kamanda wa Polisi wa
Mkoa Kigoma, Zedekia Makunja alithibitisha kuruhusiwa kwa maandamano hayo
ambayo alisema yalikidhi vigezo vya ibara ya 18 (a) ya Katiba ya nchi.
Makunja alisema viongozi hao wa BAVICHA walikuwa na
nia ya kufikisha ujumbe kwa viongozi wao na Polisi kwa kutekeleza misingi ya
Katiba iliruhusu maandamano hayo na kuwapa ulinzi ili kuhakikisha maandamano
yanafanywa kwa amani bila vurugu.
Kamanda huyo alimshauri Dk Slaa aahirishe ziara yake
mkoani Kigoma ili kusubiri vuguvugu hilo la maandamano litulie na badala yake
wafanye mikutano ya ndani.
Hata hivyo, alisema Polisi imejipanga kuhakikisha
amani na utulivu vinadumu kama kiongozi huyo ataendelea na ziara yake.

No comments:
Post a Comment