![]() |
| Gari maalumu likiwa limebeba mwili wa Mzee Nelson Mandela (kulia). |
Kwa Waxhosa wa Afrika Kusini, kifo kwa jadi si kitu
cha kuzungumzia au kupanga, hata kama kipo au kinakaribia.
Lakini walio karibu na Nelson Mandela hawakuwa na chaguo
wakati kiongozi mweusi wa kwanza wa Taifa hilo, akiwa amelazwa katika hospitali
ya Pretoria na kisha nyumbani kwake Johannesburg akisaidiwa na mashine.
Katika maisha yake ya mwisho, mipango iko hadharani
kati ya Serikali, Jeshi na familia yake wakati wakijiandaa kwa hafla ya kumuaga
shujaa huyo.
Ifuatayo ndiyo mipango iliyo katika siku 10 zijazo
za maandalizi ya maziko ya kitaifa ambayo
yatatangazwa moja kwa moja kwa mamilioni ya watu duniani lakini pia tukio la
faragha la kumuaga litakalofanywa na walio karibu naye.
Lakini kama ilivyo kwa matukio makubwa kama haya,
mipango inaweza kubadilika kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, usalama na
sababu zingine. Lakini kwa sasa, haya ndiyo ambayo Mamlaka husika na familia
wanatarajia kutokea.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, vinavyohusika
na mipango hiyo, siku hizo 10 za
maombolezo zitahusisha mila za kimagharibi na za kithembu za ukoo wa Mandela.
Mandela alifariki dunia Alhamisi saa 2.50 (saa 3.50
saa za Afrika Mashariki) usiku, akiwa amezingirwa na familia yake, Rais Jacob
Zuma alisema. CNN inaeleza kuwa wakati wa saa zake za mwisho, Mandela pia
alikuwa amezingirwa na wazee wa kithembu. La muhimu wakati fulani- ama nyumbani
kwake au mochari-wazee wa kimila wangekutana kufanya sherehe ya awali, kimila
inaitwa ‘kufumba macho’.
Katika sherehe hiyo, watakuwa wanazungumza na
Mandela, lakini pia na mizimu yake ya kimila, kuelezea kinachotokea kila hatua
ili kurahisisha safari ya kuachana na maisha ya kawaida na kuingia mengine. Baada ya sherehe hizo, mwili wa Mandela utawekwa dawa za kuuzuia kuharibika ndani ya
mochari.
Hakuna matukio yoyote kwa umma yatakayofanyika hadi
siku tano baada ya kifo hicho ambapo maelfu kwa maelfu ya waombolezaji watakusanyika
katika uwanja wa michezo wa FNB, unaojulikana kama Soccer City ulioko Soweto
kwa ajili ya kumbukumbu yake ya kitaifa. Ni katika uwanja huo, ndipo Julai
2010, Mandela alionekana kwa mara mwisho hadharani wakati wa fainali za soka za
Kombe la Dunia.
Watazamaji siku hiyo walisimama, wakashangilia huku
sauti zao pia zikimezwa na zile za vuvuzela ikiwa ni ishara ya kumpa heshima
kiongozi huyo wakati huo akiwa na umri wa miaka 92 ambapo baadhi ya watu
walidhani asingeweza kupata nguvu za kujitokeza hadharani.
Siku hii ya tano itaonekana kugubikwa na majonzi
makubwa wakati huo Taifa litakapokuwa
likiomboleza kuondoka kwa Madiba. Baadhi
ya viongozi wa kimataifa wanatarajiwa kuhudhuria tukio hilo.
Ofisa wa Ikulu ya Marekani (White House) aliiambia
CNN kwamba Utawala unashughulikia mipango ya Rais Barack Obama kwenda Afrika Kusini
kuhudhuria tukio hilo muhimu.
Kwa mujibu wa vyanzo, mwili wa Mandela utawekwa
katika majengo ya Serikali ya Union jijini Pretoria kwa siku tatu, mahali
yaliko makao makuu ya Serikali.
Siku ya kwanza itakuwa maalumu kwa wageni. Wananchi
wengine wataruhusiwa kupita pembeni mwa jeneza lake siku ya saba na ya nane.
Saa za kutoa heshima za mwisho zitakuwa mchana tu. Inatarajiwa foleni ndefu
kuanza mapema asubuhi.
Ni katika majengo hayo ya kihistoria ambako Mandela
aliapishwa kuwa Rais Mei 10, 1994. Siku hiyo adhimu, makundi ya watu
yatakusanyika katika majengo hayo kushuhudia historia ikijiandika. Siku hiyo,
mfungwa huyo wa zamani wa kisiasa, ambaye hakutarajiwa lakini akaja kuwa
kiongozi mweusi wa kwanza baada ya ubaguzi wa rangi kumalizika.
Siku tisa baada ya kifo cha Mandela, ndege ya
kijeshi yenye mwili wa Mandela itaondoka katika kituo cha anga cha Pretoria na
kwenda Kusini hadi Mthatha, mji mkuu wa jimbo la Eastern Cape. Wazee wa
kithembu na familia ya Mandela watafuatana na jeneza lenye mwili wa Mandela.
Maelfu ya waombolezaji wanatarajiwa kujipanga
pembeni mwa barabara kutoka uwanja wa ndege Mthatha kushuhudia Jeshi
likisafirisha mwili wa Mandela kwenye gari maalumu hadi kijijini Qunu.
Njiani msafara unatarajiwa kusimama kidogo kwa
maombi ili kuruhusu watu wa kawaida kutoa heshima zao.
Mwili ukifika nyumbani kwa Mandela, Jeshi
litakabidhi majukumu kwa familia yake. Bendera ya Afrika Kusini ambayo itakuwa
imefunika jeneza inatarajiwa kuondolewa na kufunikwa blanketi la jadi ya
Waxhosa, ikiwa ni ishara ya kurejea nyumbani kwa mmoja wao.
Jioni, viongozi wa ANC, machifu na familia ya
Mandela wanatarajiwa watakusanyika kwa ajili ya mkesha wa faragha kabla ya
kesho yake kufanyika maziko.
Maziko yatafanyika kwenye viwanja vya nyumbani kwa
Mandela. Inatarajiwa maelfu ya watu wakiwamo wakuu wa mataifa mbalimbali
duniani, watakusanyika kwa ajili ya maziko hayo ambayo yatafanywa chini ya hema
kubwa katika vilima ambako Mandela alikuwa akicheza enzi za utoto wake.
Ulinzi mkali wa kijeshi unatarajiwa kuwapo, kwa
lengo la kuondoa hofu ya usalama. Tukio lote litarushwa moja kwa moja kwa
mamilioni ya wasikilizaji na watazamaji duniani kote.
Mchana-wakati huu ambao jua la kiangazi linamulika
kutoka angani- Mandela atazikwa katika
ardhi hiyo yenye miamba. Eneo la makaburi limejengwa maalumu kwa ajili yake;
marehemu wengi wa familia ya Mandela wamezikwa hapo.
Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo alisema kiongozi huyo wa zamani mwenye umri
wa miaka 95, ambaye alirudishwa nyumbani kwa gari la wagonjwa Agosti kumalizia
siku zake hapo, “alifariki dunia kwa amani akiwa na familia yake.”
Mke wake wa tatu, Graca Machel (68), alikuwa pembeni,
sambamba na baadhi ya wanawe, wajukuu, watoto wa kambo, mchungaji na wazee wa
kabila lake la Wathembu.
Binti wa Mandela, Makaziwe Mandela-Amuah na mabinti
zake, Tukwini na Ndileka, nao walikuwa na babu yao huyo hadi mwisho wa pumzi
yake.
Lakini hakukuwa na dalili zozote za Winnie
Madikizela-Mandela, ambaye ni mkewe wa pili aliyemwoa mwaka 1958 na kudumu naye
kipindi chote cha miaka 27 aliyokuwa akitumikia kifungo gerezani kabla ndoa yao
ya miaka 38 kusambaratika kwa machungu mwaka 1996.
Hali ya kiongozi huyo wa zamani ilianza kudorora
tangu Juni, alipolazwa hospitalini akisumbuliwa na maambukizi na hali ilikuwa
ya wasiwasi kuwa alikaribia kifo.
Hali yake ilitengemaa hata kuruhusiwa kurudi
nyumbani, ambako chumba chake cha kulala kilionekana sawa na chumba cha
wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).
Mwezi jana, Winnie alisema mumewe huyo wa zamani
alishinda tatizo la baridi yabisi lililokuwa likimkabili, lakini alikuwa bado
mgonjwa na hakuwa anaweza kuzungumza kwa sababu ya mirija aliyowekwa kwenye
mapafu yake ili kutoa maji.
Alisema mumewe huyo wa zamani alikuwa akitumia
ishara kuwasiliana na kwamba nyumba alimokuwa ilikuwa ikisafishwa vizuri na
kupuliziwa dawa ili kuchelea maambukizi kurejea.
Wiki hii, hali ya Mandela ikabadilika tena na kuwekwa
mashine ya kumsaidia kupumua na wakati mwingine alipoteza fahamu.
Jumatano, siku moja kabla baba yake hajafariki
dunia, binti mkubwa Makaziwe (60) alisema: “Unaweza kumwona akipambana, lakini
roho yuko pamoja naye.”
Na mjukuu wake wa kiume kwa marehemu mwanawe wa
kiume, Makgatho Mandela, Ndaba Mandela (30), alisema: “Maendeleo yake hayatii
moyo pale kitandani.”
Haijulikani kama Winnie, ambaye aliolewa na kiongozi
huyo mwaka 1958 hadi 1996, alikuwapo wakati huo wa mwisho.
Kaka wa Ndaba, Mandla Mandela (39), anaaminika kuwa
na babu yake katika saa hizo za mwisho kama ilivyokuwa kwa watoto wa Graca,
Josina na Malenga Machel, ambao wana umri wa miaka 30. Mchungaji pia alikuwapo
baada ya kuitwa jioni kabla ya kifo.
Naye msaidizi wake, Zelda la Grange (43),
anafikiriwa naye alikuwa karibu na
familia wakati hali ya Mandela ikizidi kudorora.
Wakati wa saa za mwisho kabla ya kifo chake saa 2.50
(saa 3.50 saa za Afrika Mashariki) usiku, wazee wa kithembu waliungana na ndugu
zake pembeni mwa kitanda.
Juzi asubuhi mwili wa Mandela uliondolewa nyumbani
kwake ukiwa kwenye jeneza lililofunikwa bendera ya Taifa la Afrika Kusini na
kupelekwa kwenye mochari ya hospitali ya kijeshi jijini Pretoria, kabla ya
kuanza siku 10 za maombolezo.

No comments:
Post a Comment