![]() |
| Mke wa Mandela, Winnie akiwa amejishika tama kwa huzuni wakati wa msiba wa mumewe. Kulia ni Rais Jacob Zuma. |
Mkuu wa Shughuli za Mazishi ya Kitaifa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Collins Chabane alisema mpaka jana jioni, wakuu wa nchi 13 za Afrika, walikuwa wamethibitisha kushiriki.
Alisema wawakilishi kutoka Umoja wa Matiafa na Umoja wa Afrika, nao wamethibitisha kushiriki.
Rais wa Marekani, Barack Obama naye alithibitisha kwamba ataongozana na marais wastaafu wa nchi hiyo, Jimmy Carter, George W Bush na Bill Clinton na wake zao.
Waziri huyo alisema shughuli za mazishi ya Kitaifa, zitakazoanza kesho, zitaanza saa tano kamili asubuhi kwa saa za Afrika Kusini.
Kabla ya uthibitisho wa jana, juzi Jumamosi Ikulu ya Marekani ilithibitisha kuwa Rais Obama na mkewe Michelle pamoja na Bush na mkewe Laura, wangeshiriki kwenye mazishi hayo.
Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, ambaye alikuwa madarakani wakati Mandela alipochaguliwa kwa mara ya kwanza, yeye alitangaza kupitia mtandao wa jamii wa Twitter kwamba ataongozana na familia yake kushiri kwenye mazishi ya mwasisi huyo wa Taifa la Afrika Kusini.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duninai, Papa Francis na Malkia Elizabeth II wa Uingereza, wao wanatarajiwa kutuma wawakilishi. Vatican itawakilishwa na kiongozi mwandamizi wa kidini wakati Malkia atawakilishwa na Prince Charles.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon ambaye amemtangaza Mandela kama mwamba wa kupigania haki, pia mbali na wawakilishi wa UN, yeye binafsi pia atashiriki kwenye mazishi hayo.
Rafiki wa siku nyingi wa Mandelea ambaye pia ni kiongozi wa kiroho wa Tibet, Dalai Lama, haijafahamika kama atashiriki kwenye shughuli hiyo.
Migyur Dorjee ambaye ni Ofisa wa Serikali ya Afrika Kusini, alisema Dalai Lama bado hajapatiwa hati ya kuingilia nchini hapa.
“Dalai Lama ni mshirika wa karibu wa Mandela na kifo hiki kimemshitua," alisema.
Mwaka jana Serikali ya Afrika Kusini iliingia katika malumbano baada ya kuchelewesha kumpatia hati ya kuingilia nchini kiongozi huyo wa kidini, ambaye alikuwa anahudhuria sherehe ya siku ya kuzaliwa ya Askofu Desmond Tutu, aliyekuwa anatimiza miaka 80.

No comments:
Post a Comment