![]() |
| Josephat Gwajima. |
Wakati viongozi
wa madhehebu ya dini ya Kikristo nchini, wakionekana kushindana kwa utajiri,
hali inayowafanya waishi `kifalme’ na kufungua miradi, Mchungaji Kiongozi wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema hana mpango wa kufungua
biashara, zaidi ya kujikita na mahubiri ya Injili.
Aidha, amesema
Mungu anaendelea kumbariki katika kazi yake, ndiyo maana mambo yake
yanamnyookea, akitolea mfano kuwa baada ya kumiliki nyumba, magari na fedha za
kutosha, sasa amembariki na kumpa helikopta atakayoitumia kufikia waumini wake
wa ndani na nje ya nchi.
Usafiri huo wa
angani, utaongeza idadi ya vyombo vya usafiri vya Mchungaji huyo, ambaye
anatajwa kuongoza kwa utajiri miongoni mwa viongozi wa madhehebu ya Kikristo
nchini, kwani anamiliki magari kadhaa, likiwamo la kifahari aina ya Hummer
lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 200.
Akizungumza na mwandishi
hivi karibuni kwa simu, Gwajima ambaye alikuwa anaendesha mikutano ya kueneza
Neno la Mungu katika mikoa mbalimbali ikiwamo Kilimanjaro na Tanga, alisema
helikopta imeshanunuliwa na matarajio
yake ni kwamba, baada ya kukamilika taratibu zote za kisheria nchini,
itawasili.
“Sipendi kusema
mambo yangu sana, lakini kwa kuwa umeuliza
naweza kugusia kidogo, ni kweli nina mpango wa kuanza kuhubiri Injili
kwa helikopta, na kama ilivyo kwa gari, nayo hii nimepewa na watu wa Mungu
walioguswa na huduma yangu Japan.
“Itafika nchini
wakati wowote mambo ya kisheria yakikamilika, huu si wakati wa kuizungumzia
sana maana bado haijafika,” alisema Gwajima ambaye gari lake aina ya Hummer
liliwahi kuzua gumzo, wengine wakimhusisha na biashara haramu ya dawa za
kulevya, ingawa anapuuza madai hayo.
Mchungaji
Gwajima, alieleza wazi kuwa utajiri wake unatokana na baraka anazopewa na
anaowahudumia ndani na nje ya nchi na pia kazi yake ya kufundisha anayoifanya
ughaibuni.
Aidha, kutokana
na utajiri anaosema unatokana na baraka za Mungu, Mchungaji Gwajima anamiliki
nyumba ya ghorofa nne eneo la Mbezi Beach katika Manispaa ya Kinondoni, ingawa
haijakamilika.
Pia,
amewanunulia wachungaji wake 40 magari ya kutembelea kwa bei tofauti, yakiwamo
ya chini ya Sh milioni 10 na mengine ya zaidi ya Sh milioni 20.
“Lakini nina
wachungaji wa ngazi mbalimbali, hawa ni wale wa juu, wengine wachungaji wadogo
wapo zaidi ya 670, hawa ni watenda kazi muhimu na wanatofautiana kwa ngazi zao,
ndiyo maana kazi ya Mungu inasonga mbele hata nisipokuwapo,” alisema.
Mbali na magari
ya wachungaji, pia amenunua mabasi 20 ya kubeba waumini kutoka na kwenda
kanisani, yakianzia maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam. Alithibitisha
kuwa, kila moja limegharimu kati ya Sh milioni 80 na 100.
Mbali ya
Mchungaji Gwajima, viongozi wengine wa makanisa wanaotajwa kuwa na utajiri
mkubwa wa mali na fedha ni Nabii na Mtume Josephat Mwingira
wa Kanisa la Efatha anayemiliki benki, mashamba makubwa na mali
nyingine, Mchungaji Gertrude Lwakatare wa Mikocheni B Assemblies of God
anayemiliki mtandao wa shule za St. Mary’s nchini.
Wengine ni Askofu Zachary Kakobe wa Kanisa la
Full Gospel Bible Fellowship, Anthony Lusekelo `Mzee wa Upako’ wa Kanisa la
Maombezi `GRC’ na Mtume Onesmo Ndegi wa Kanisa la Living Water Center ‘Makuti
Kawe’.
No comments:
Post a Comment