![]() |
| Gari maalumu liliondoa mwili wa Mzee Nelson Mandela kutoka nyumbani kwake alipofariki dunia usiku wa kuamkia jana. |
![]() |
| Kama haamini kilichotokea. Mtu huyu akishika picha ya Mzee Mandela mara baada ya kutangazwa kufariki dunia. |
Rais Barack
Obama wa Marekani, mkewe Michelle na mabinti zao wawili Sasha na Malia, wataungana
na marais wastaafu wa Marekani akiwamo Bill Clinton, ambaye alimfahamu vilivyo
Mandela.
Maarufu wengi
ambao walikuwa na uhusiano wa binafsi na Mandela, kama vile Oprah Winfrey na
kiongozi wa kikundi cha U2 Bono, nao wanatarajiwa kushiriki mazishi ya kitaifa
yatakayofanyika keshokutwa katika uwanja wa michezo wa FNB jijini Johannesburg
wenye uwezo wa kuchukua watu 90,000.
Askofu Mkuu
mstaafu Desmond Tutu wa Cape Town, anatarajiwa kuongoza Ibada maalumu ya
mazishi hayo.
Hadi jana vitabu vya rambirambi vilikuwa
vimefunguliwa katika majengo ya Serikali nchini kote na katika ofisi za ubalozi
wa Afrika Kusini duniani kwa waombolezaji kusaini.
Maandalizi ya
maziko ambayo yanatarajiwa kuchukua kama wiki mbili yanatarajiwa ‘kuisimamisha’
nchi hiyo yenye watu milioni 53.
Makadirio ya
haraka haraka ya wageni watakaohudhuria mazishi wakiwamo wakuu kadhaa wa
serikali, yanaashiria kuongeza mzigo katika sekta ya usafiri na huduma kwa
Serikali ya Afrika Kusini, ambayo sasa italazimika kuimarisha ulinzi wa anga
wakati wote wa kipindi hicho.
Kwa mujibu wa
vyanzo kadhaa vya habari, vinavyoshiriki maandalizi ya mazishi, tukio hilo la
siku kama 10 litachanganya mila za kimagharibi na za jadi za ukoo wa Mandela wa
kabila la Wathembu.
Katika hatua
fulani kuanzia siku ya kwanza hadi ya nne, CNN iliripoti kuwa wazee wa Kithembu
watakusanyika kwa ajili ya sherehe ya kwanza inayoitwa ‘kufunga macho’ ama
nyumbani kwa marehemu au ndani ya mochari ulimohifadhiwa mwili.
Baada ya sherehe
hiyo, inaaminika mwili utatiwa dawa kuzuia kuharibika ndani ya mochari, katika
hospitali ya kijeshi jijini Pretoria.
Hakuna tukio
lolote rasmi linalotarajiwa kufanyika hadi siku tano ziishe pale ambapo
waombolezaji watapata fursa ya kumuaga baba yao kipenzi wakati wa Ibada maalumu
itakayofanyika katika uwanja huo ambao ulitumika kwa fainali za soka Kombe la
Dunia mwaka 2010.
Kwa siku tatu
baadaye, mwili wa shujaa huyo wa kupinga ubaguzi wa rangi unatarajiwa kuwekwa
katika majengo ya Serikali ya Union jijini Pretoria, ambako aliapishwa kushika
urais Mei 10, 1994.
Kwa mujibu wa
mila za Wathembu, atatakiwa kuzikwa mchana siku ya Jumamosi-kuna uwezekano
maziko yakafanyika Jumamosi ya Desemba 14.
Rais Obama
alitangaza rasmi kuhudhuria mazishi ya Mandela aliyefariki dunia juzi usiku
nyumbani kwake Johannesburg.
Baada ya
kuzungumza na waandishi wa habari Ikulu ya Washington, DC, ofisi ya Rais
ilitangaza kuwa Obama atasafiri kwenda Afrika Kusini kuhudhuria maziko hayo.
Akimzungumzia
Mandela, Rais Obama alisema: “Alipata mafanikio makubwa zaidi ya ilivyotarajiwa
kwa mtu yeyote na leo amerudi nyumbani. Madiba aliibadilisha Afrika Kusini na
alituvutia sote-safari yake kutoka jela hadi urais inajumuisha juhudi za
binadamu kubadilisha maisha yakawa bora zaidi.”
Obama alizuru
Afrika Kusini Juni na kukutana na familia ya Mandela na kushindwa kuonana na
kiongozi huyo aliyekuwa mahututi hospitalini. Akiwa Seneta, Obama mara nyingi
alikuwa akiwasiliana na Mandela.
“Hatutaweza
kuyaona tena ya mfano wa Mandela, hivyo tunapaswa kuishi kwa mfano wake na
kufanya uamuzi bila chuki ila upendo,” alisema Obama. Alisema mawazo na maombi ya familia yake na
watu wa Marekani yako na familia ya Mandela.
Rais Jakaya
Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais Jacob Zuma na kupitia kwake, kwa
mkewe Graca Machel, wanafamilia wote na
wananchi wa Afrika Kusini.
"Afrika
Kusini, Afrika na dunia wamepoteza mtu mashuhuri na shujaa mkubwa wa karne ya
20 na 21. Tunaelewa uchungu walionao wananchi wa Afrika Kusini kwa kupoteza
kiongozi shupavu, jasiri, mwanamapinduzi, mvumilivu na mstahimilivu,"
aliongeza Rais Kikwete.
Alimwelezea
Mandela kuwa kielelezo cha aina yake kwa wanadamu kwa moyo wake wa kusamehe,
kuhurumia na upendo uliomwezesha kuunganisha wananchi wa Afrika Kusini kuwa
Taifa moja baada ya kipindi kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
"Mandela
ni mfano bora kwa wanadamu wa jinsi binadamu mwungwana anavyopaswa kuwa. Ni
wajibu wa wana Afrika Kusini, Afrika na dunia kuiga mfano wake hasa moyo wake
wa uzalendo, kujitolea hata maisha yake kwa ajili yake na wananchi wenzake.
Tuzidi kumwombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi".
Kutokana
na kifo hicho Rais alitangaza siku tatu za maombolezo kuanzia jana Desemba 6
hadi keshokutwa na aliagiza bendera zote zipepee nusu mlingoti kwa siku hizo
tatu.
“Mungu
alikuwa mwema kwetu sisi Waafrika Kusini kwa kutupa Nelson Mandela kuwa Rais wetu katika kipindi kigumu sana
katika historia,” alisema mshirika wake wa siku nyingi, Askofu Mkuu mstaafu
Tutu.
Bibi wa miaka 70 aliwatia faraja waombolezaji nyumbani kwa zamani kwa
Mandela katika barabara ya Vilakazi mjini Soweto jana.
Ernestina Matshaka alionekana akicheza kama kijana akifuatisha wimbo wa uhuru ukimhusu Mandela. “Sisi Waafrika tunapofurahi, tunaposononeka au kuomboleza huimba. Kuimba kunatufariji,” alisema.
“Nimepunguziwa mzigo kwamba Madiba amefariki dunia. Haikuwa haki kumtarajia aruke kutoka kwenye kitanda cha ugonjwa na kukimbia huku na huko kama mtoto wa kiume.”
Matshaka alisema atakuwa na furaha sana kama Waafrika Kusini watatulia wakati huu na kuheshimu mema aliyoyaacha Mandela. Kundi la vijana na wazee lilitiwa nguvu na Matshaka, likicheza na kuimba.
Maofisa wa Polisi wakiwa katika magari yapatayo 10 walikuwapo wakifuatilia huku mishumaa ikiwa imewashwa mbele ya nyumba yake hiyo na barabara zikifungwa..
Walinzi wanaolinda nyumba hiyo walisimika ubao mkubwa mweupe kwa ajili ya watu kuandika ujumbe wao. Hata hivyo, ghafla nyimbo zilikatizwa na gari lililopita karibu likipiga wimbo wa Johnny Clegg wa ‘Asimbonanga isiZulu’ wenye maana ya “hatujamwona”.
Ingawa alidhoofu, Mandela alikuwa akikimbizwa na kutoka hospitalini katika miaka zaidi ya mitano, mara ya mwisho akipelekwa Juni 8. Awali alitibiwa tatizo la mapafu, lakini baada ya wiki tatu ilitangazwa hali yake kubadilika na kuwa mahututi.
Ingawa Serikali ya Afrika Kusini haikutangaza ukubwa wa tatizo lake kiafya, lakini vyanzo vya kuaminika vya habari vilisema ini na figo vilikuwa vikifanya kazi kwa asilimia 50 tu.
Vyombo vya habari Afrika Kusini viliripoti kwamba alikuwa akipumua kwa mashine huku figo zake zikisafishwa kila mara.
Baada ya kutangaziwa kifo hicho, wananchi waliingia mitaani huku wengine wakionesha wazi sura za majonzi huku wengine wakisherehekea wakiimba nyimbo kuonesha uzalendo.
Watu wa kada, rangi na dini tofauti waliimba kwa sauti kubwa pamoja, wakicheza na kupunga mishumaa karibu na nyumbani kwake alikofia.
Wengi waliimba: “Iko mikononi mwetu sasa,” wakimaanisha urithi aliouacha Mandela huku wengine wakijihisi kuwa sasa ni wajibu wao kuuendeleza.
Mamia wengine walipeperusha bendera za Afrika Kusini, wakipiga makofi na kutaja jina la Mandela kumkumbuka Rais huyo wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia.
Wakati wa kesi yake mwaka 1964 Mandela alikamilisha utetezi wake akiwa kizimbani akisema: “Nimepambana dhidi ya utawala wa weupe, nimepigana dhidi ya utawala wa weusi.
Ninavutiwa na wazo la jamii iliyo huru na ya kidemokrasia ambamo watu wote wanaishi pamoja kwa amani na fursa sawa. Ni wazo ambalo natumaini kulitetea na kulifanikisha. Lakini kama itawezekana, ni wazo ambalo niko tayari kulifia.”
Hakika Mandela aliishi kwa wazo hilo na kulifanikisha. Alifanikiwa zaidi ya matarajio ya mtu yeyote. Leo, amekwenda nyumbani. Na tumepoteza mmoja wa watu wenye ushawishi, jasiri na hakika binadamu wema ambao kila mmoja wetu atapenda kuwa nao duniani hapa. Si wetu tena – ni wa zama.
“Waafrika Kusini wenzangu, mpendwa wetu Nelson Rolihlahla Mandela, Baba wa Taifa letu la kidemokrasia, ameondoka. Alifariki dunia kwa amani akiwa na familia yake saa 2.50 (saa 3.50 saa za Afrika Mashariki) usiku wa Desemba 5 nyumbani kwake Houghton,” alitangaza Rais Zuma na kuongeza: “Hivi sasa amepumzika. Amepumzika kwa amani.”
Jijini London, Uingereza, familia ya kifalme, watu mashuhuri na wanafamilia ya Mandela –wakiwamo mabinti zake wawili-walikuwa wakihudhuria maonesho ya filamu ya maisha ya Mandela ndipo walipopokea taarifa hizo za kusikitisha. Akizungumza kutoka ukumbi wa sinema wa Odeon, mtoto wa Malkia Prince William alisema: “Nilitaka kusema kwa kweli ni habari za kusikitisha na kuhuzunisha. Tumekumbushwa kile mtu asiye wa kawaida Nelson Mandela alichokuwa. Tuko pamoja kwa mawazo na maombi na familia yake.”
Haikuweza kueleweka mara moja kilichompata binti wa Mandela, Zindzi, ambaye alionekana mwenye furaha na aliyetulia akiingia katika ukumbi wa sinema na akaonekana kuzidiwa alipoingia ndani.
“Ni kitu kinachonifanya nijisikie furaha kwamba kile familia yangu ilichopitia na mchango wa baba yangu vimetambuliwa,” alisema Zindzi kuhusu filamu hiyo na kukutana kwake na familia ya kifalme.
Mandela ameacha mjane Graca Machel, binti yake Makaziwe kwa mkewe wa kwanza na mabinti wawili Zindzi na Zenani.
Mara ya mwisho kuonekana hadharani ilikuwa katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 pale mkewe alipomsaidia kuinua mkono wake kupungia umati wa watu.
Pamoja na kupata matibabu ya saratani ya kibofu, maumivu ya tumbo na matatizo ya macho, tatizo kubwa la Mandela lilikuwa ni kupumua.
Aliharibika mapafu na kuugua kifua kikuu wakati akichimba chokaa akitumikia kifungo cha miaka 18 katika gereza la mateso la kisiwa cha Robben, nje ya Cape Town.
Hali hiyo ilimfanya alazwe mara nyingi hospitalini katika muongo uliopita-na mara tano tangu Desemba mwaka jana.
Alipata matibabu ya matatizo ya kupumua, maumivu ya tumbo, mawe kwenye figo na Aprili aliondolewa maji kwenye mapafu.
Alizaliwa katika familia ya kifalme, katika ufalme wa Wathembu, mjini Transkeiin mwaka 1918. Baba yake alikuwa na wake wanne, mama yake akiwa ni wa tatu. Alikuwa mtoto wa kwanza kwenye familia yao kwenda shule na alikuwa ni mwalimu wake aliyempa jina la Kiingereza la Nelson badala ya jina lake la awali la Rolihlahla.
Akiwa na miaka 19, alijiunga na Chuo Kikuu cha Fort Hare, ambako mara moja alianza kujihusisha na masuala ya siasa – au kuandaa migomo dhidi ya siasa.
Baada ya kukataa kufunga ndoa ambayo iliandaliwa kwa ajili yake na wazee wa kikabila, kwa kipindi kifupi alifanya kazi ya ulinzi mgodini na baadaye akajiunga na kampuni ya sheria ya Johannesburg.
Alianza kuishi katika mji wa weusi wa Alexandra na kuanza masomo ya sheria katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand, ambako alikutana na wanafunzi wenzake ambao walikuja kuwa wanaharakati wa kisiasa baadaye; Ruth First, Joe Slovo na Harry Schwarz.
Katika miaka ya awali ya hamsini, Mandela alijiingiza zaidi katika upinzani wa ubaguzi wa rangi, yeye na mwanaharakati mwenzake Oliver Tambo walianzisha kampuni ya uwakili, wakitoa ushauri wa bei nafuu kwa wakazi wa Alexandra.
Mandela alivutiwa sana na Mahatma Ghandhi wa India, kwa kujihusisha na upinzani usiotumia nguvu. Lakini mwaka 1956, akiwa na wenzake 150 walikamatwa na kufunguliwa mashitaka ya uhaini.
Katika hukumu dhidi yao, walinusurika adhabu ya kunyongwa lakini wakakumbwa na kifungo cha maisha jela. Alitumikia kifungo cha miaka 27, huku miaka 18 akitumika katika kisiwa cha Robben.
Ndoa yake na Winnie ilisambaratika baada ya kutoka jela na kuamua kumwoa Graca Machel, aliyekuwa mjane wa rais wa kwanza wa Msumbiji, Samora Machel.


No comments:
Post a Comment