Jaji Joseph Warioba akihutubia wakati alipowasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba, Dar es Salaam, jana. |
Akikabidhi Rasimu hiyo jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba, alisema baada ya kukaa na kupitia malalamiko juu ya muundo wa sasa wa Muungano na takwimu za waliotoa maoni, imeona serikali tatu zinakidhi matakwa ya Watanzania wengi.
Uamuzi wa Tume umefanyika baada ya kupokea maoni kutoka kwa makundi ya watu zikiwamo taasisi za serikali, ambao asilimia kubwa ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu, walionesha kuhitaji muundo huo wa Muungano.
Akiwasilisha taarifa ya Tume kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais Ali Mohamed Shein, Jaji Warioba alisema katika maoni yaliyotolewa, takwimu zinaonesha upande wa Tanzania Bara, asilimia 61 walipendekeza serikali tatu; asilimia 24 mbili na asilimia 13 moja.
Kwa upande wa Zanzibar, asilimia 60 walipendekeza Muungano wa Mkataba, asilimia 34 serikali mbili na asilimia 0.1 serikali moja.
Aidha, taasisi nyingi kama vile vyama vya siasa, asasi za kiraia na jumuiya za kidini zilipendekeza muundo wa serikali tatu.
Miongoni mwa taasisi za serikali zilizopendekeza mfumo wa serikali tatu, ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo katika maoni yao, zilisema muundo huo utaondoa kero za Muungano.
Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, lilipendekeza kuwapo kwa Mamlaka huru ya Zanzibar, Mamlaka huru ya Tanganyika na Mamlaka ya Muungano kila moja ikiwa na mipaka yake.
Jaji Warioba akieleza namna Muungano ulivyoteka mjadala wa Rasimu ya Awali ya Katiba, alisema kwa Tanzania Bara, wananchi zaidi ya 39,000 walitoa maoni kuhusu eneo hilo.
“Wananchi karibu wote waliotoa maoni, walijikita kwenye suala la Muungano. Kati ya wananchi karibu 38,000 waliotoa maoni, 19,000 walitoa maoni kuhusu Muungano,” alisema.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, baada ya kuona takwimu za waliotoa maoni na kuzichanganua, Tume iliamua kufanya utafiti kuhusu muundo wa Muungano na kubaini malalamiko mengi kuhusu Muungano.
Akitaja malalamiko waliyobaini, Jaji Warioba alisema kwa upande wa Zanzibar, yapo malalamiko makubwa matatu ambayo ni Serikali ya Tanganyika kuvaa koti la Serikali ya Muungano linalosaidia Tanganyika zaidi kuliko Zanzibar. “Koti hilo limeifanya Tanganyika kuwa ndiyo Tanzania,” alisema.
Mengine ni kuongezeka kwa mambo ya Muungano na hivyo kuathiri madaraka ya Zanzibar na kufifisha hadhi yake hivyo kuendelea kumezwa.
Wazanzibari wanalalamikia pia kumwondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Kwa upande wa Bara, malalamiko makubwa yaliyobainishwa na Tume ni wananchi wa Bara kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa Zanzibar wana haki hiyo Bara.
Malalamiko mengine ni Zanzibar kuwa nchi huru, yenye bendera, wimbo wake, serikali na imebadili Katiba yake ili ijitambue kama nchi, wakati Tanzania Bara imepoteza utambulisho wake.
Vile vile wanalalamikia Zanzibar kwamba imebadili Katiba na kuchukua madaraka ya Jamhuri ya Muungano kama vile kuelekeza sheria za Muungano zilizopitishwa na Bunge zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi kujadiliwa.
Tume baada ya kufanya uchambuzi wa malalamiko hayo, ikaona ni vigumu kuyafanyia ukarabati hivyo ikaona ipendekeze muundo wa serikali tatu ili pande zote mbili ziwe na hadhi sawa.
“Kila upande utashughulikia mambo yasiyo ya Muungano na Serikali ya Muungano itabaki na mambo machache ya msingi na ambayo yanaunganisha Taifa,” alisema.
Hata hivyo, Jaji Warioba alisema Tume imetambua kuwa muundo huo una changamoto zake, hivyo ili kujikinga nazo, imependekeza mambo matatu likiwamo la uraia kubaki kuwa mmoja.
Imependekeza raia wote wa Jamhuri wawe huru na wawe na haki zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi nzima isipokuwa katika mazingira maalumu.
“Haki zao zikiingiliwa na upande wowote bila sababu maalumu, itasababisha kuibuka kwa utaifa, utanganyika au uzanzibari na uzalendo utayumba. Uzalendo ukiyumba, Muungano pia utayumba,” alisema.
Licha ya uraia, lingine ni Serikali ya Muungano kuwa na uhakika wa mapato kwa ajili ya kulipia gharama za Muungano ambapo Tume imependekeza ushuru wa bidhaa uwe ni kodi ya Muungano.
Kodi hiyo itakidhi sehemu kubwa ya matumizi ya Muungano na sehemu iliyobaki itapatikana kutokana na mapato yasiyo ya kodi yanayotokana na mambo ya Muungano, michango ya nchi washirika na mikopo.
Tatu ni kuundwa kwa Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais wa Muungano na ijumuishe viongozi wakuu wa nchi washirika.
Majukumu ya Tume ni kusimamia mashauriano na ushirikiano kati ya Serikali ya Muungano na za nchi washirika ili kuhakikisha sera zinawiana na pia kusimamia na kuimarisha masuala yenye maslahi kwa Taifa na pia kutatua migogoro.
Jaji Warioba ambaye alikiri suala la Muungano kuwa moja ya mambo yaliyojadiliwa kwa hisia kali tangu Rasimu ya awali ilipotolewa, alisema kazi ya kukusanya maoni na kuibuka na mapendekezo hayo katika Rasimu hii, haikuwa rahisi ikizingatiwa wajumbe wa Tume wametoka katika makundi tofauti.
Alisema, “kila mmoja wetu alikuwa na imani yake, maoni yake, itikadi yake, msimamo wake. Lakini tulikubaliana mapema kabisa, kwamba wajibu wetu ni kwa Taifa. Kwa hiyo tuliacha imani na misimamo yetu binafsi na kuamua kusikiliza wananchi kwa makini sana.”
Aliendelea: “Majadiliano yetu yalilenga kupata mwafaka wa kitaifa. Baadhi ya mapendekezo yetu kwa hakika yatapokewa kwa hamasa kubwa. Lakini la muhimu ni kupata mwafaka wa kitaifa badala ya kufikia uamuzi kwa kujipima katika makundi.”
Kulingana na taarifa ya Mwenyekiti huyo, kama ilivyokuwa katika Rasimu ya Awali, suala la muundo wa Muungano ndilo lililochukua muda mwingi wa Tume.
Akizungumzia Rasimu hiyo kwa niaba ya CCM, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Tawala, Nape Nnauye, alisema wanaipongeza Tume kwa kazi kubwa iliyoifanya kwa utulivu na umakini mkubwa na sasa sehemu iliyobaki ni ya Bunge Maalumu la Katiba na kura za wananchi.
“CCM inaitakia kila la heri sehemu muhimu iliyobaki katika mchakato ifanyiwe kazi kwa busara na umakini mkubwa kama ilivyotangulia kufanywa,” alisema Nape.
CCM ambayo inaamini katika Serikali mbili, ilisema imesikiliza kwa makini taarifa ya Tume hasa katika suala la Serikali tatu na sababu zilizotolewa na kwamba inazichukua na itaziingiza katika vikao vyake, itatafakari na kutoa uamuzi unaopasa.
Katika Rasimu hii ambayo ni ndefu kuliko ya awali, madaraka ya Rais hasa ya uteuzi yamepunguzwa kwa kuweka vyombo vya kupendekeza majina ya watu wa kuteuliwa na kwa baadhi ya vyeo kuhitaji kuthibitishwa na Bunge.
Rasimu hiyo yenye ibara 271 ikilinganishwa na ya awali yenye ibara 240, hata hivyo imesisitiza Rais ndiye mwenye hadhi na heshima ya Mkuu wa Nchi, Amiri Jeshi Mkuu na Kiongozi wa Serikali.
Vile vile imependekezwa wabunge wasiwe mawaziri, kuwe na ukomo wa uwakilishi katika Bunge na wapiga kura wawe na madaraka ya kumwajibisha mbunge hata kabla ya kumalizika kwa muhula wake.
Mengine ni Spika na Naibu Spika wasitokane na wabunge au kiongozi wa juu wa chama cha siasa.
Uraia ni mmoja wa Jamhuri ya Muungano ni mmoja. Rasimu inapendekeza kutambuliwa kwa uraia wa kuzaliwa na kujiandikisha ambao ni wa nchi moja. Aidha, inapendekeza kuwapa hadhi maalumu watu wenye asili au nasaba ya Tanzania ambao wameacha kuwa raia wa Tanzania kwa kuchukua uraia wa nchi nyingine.
Marufuku kiongozi wa umma kutumia wadhifa, nafasi au madaraka kwa manufaa yake binafsi, familia yake, ndugu, jamaa, marafiki au mtu aliye na uhusiano naye wa karibu.
Vile vile Tume kwa kuzingatia maoni ya wananchi, tofauti na ilivyokuwa katika Rasimu ya Awali, sasa inapendekeza Msajili wa Vyama vya Siasa iwe ni taasisi inayojitegemea na si kuwa sehemu ya Tume Huru ya Uchaguzi.
Imependekeza pia kuwepo Jeshi la Polisi moja na Idara ya Usalama wa Taifa moja katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rasimu inapendekeza muda wa mpito wa miaka minne, kuanzia tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba Mpya hadi Desemba 31, 2018; na kwamba sheria zilizopo sasa zitaendelea kutumika hadi zitakapobadilishwa.
Masuala yaliyopendekezwa yafanyiwe kazi katika kipindi cha mpito ni pamoja na kutungwa Katiba ya Tanganyika, mgawanyo wa rasilimali baina ya Serikali ya Muungano na serikali za nchi washirika.
Mengine ni kufanya maandalizi ya kuendesha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 2014. Kuundwa kwa tume na taasisi za kikatiba zilizoainishwa kwenye Katiba.
Akielezea mchakato wa maandalizi ya Rasimu hiyo, Jaji Warioba alisema tofauti na wasiwasi uliokuwapo kwa ushiriki wa wananchi wa kawaida, ungekuwa dhaifu, sura tano za mwanzo za Rasimu zinatokana na mchango mkubwa kutoka kwa wananchi.
“Tume ilipoanza kulikuwa na wasiwasi, kwamba ushiriki wa wananchi wa kawaida ungekuwa dhaifu kwa sababu iliaminika kwamba wananchi kwa ujumla wao hawana ujuzi wa Katiba,” alisema Jaji Warioba.
Aliendelea kusema: “Lakini Tume iligundua mapema kwamba wananchi wanajua mambo mengi ambayo ni msingi wa Katiba yoyote. Sura tano za mwanzo wa Rasimu ya Katiba zinatokana na mchango mkubwa kutoka kwa wananchi.”
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, maoni ya wananchi yalihusu misingi ya Taifa, tunu za Taifa, maadili na miiko ya viongozi, dira ya Taifa na haki za binadamu. Wananchi pia walitoa maoni mazito kuhusu uongozi na utawala wa nchi, ikiwa ni pamoja na nafasi ya wawakilishi wao bungeni.
Aprili 6 mwaka jana, Rais Kikwete aliteua wajumbe 34 wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Warioba na kuwaapisha Aprili 13 mwaka huo kabla ya kuanza kazi yao, Mei 2.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa miezi 18 kwa Tume kukamilisha kazi yake. Sheria pia ilitoa nafasi ya Tume kuongezwa muda usiozidi miezi miwili na iliomba muda huo ikakubaliwa kabla ya kukamilisha kazi yake jana na kuikabidhi kwa Rais.
No comments:
Post a Comment