Tuesday, December 10, 2013

MANDELA ALISAHAU VIATU DAR, AIACHIA ANC WOSIA MZITO KUHUSU TANZANIA...

Viatu maarufu vya Mzee Nelson Mandela.
Wakati dunia ikienda Afrika Kusini kumzika mpiganaji dhidi ya ubaguzi wa rangi duniani, Baba wa Taifa la Afrika Kusini, Nelson Mandela, Tanzania inaomboleza ikiwa na kumbukumbu za undugu wa tangu miaka ya 1960.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 52 ya Uhuru wa Tanganyika ambayo sasa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete ambaye anatarajiwa kushiriki maziko hayo, alisema Watanzania hatuna budi kuungana na wenzetu wa Afrika Kusini kuomboleza kifo cha ndugu yetu, mpenzi wetu na kiongozi wetu Mandela.
Uhuru wa Tanganyika, sasa Tanzania Bara, ulipatikana kutoka kwa wakoloni wa Kingereza Desemba 9,  1961 na maadhimisho yake yalifanyika jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam huku ngoma zikisitishwa kutoa burudani, ili kuungana na Afrika Kusini katika maombolezo ya kifo cha Mandela.
Rais Kikwete alisema mazungumzo yaliyofanywa kati ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Mandela miaka ya 1960, ndiyo aliyoibua mafunzo ya wapigania uhuru Kusini mwa Afrika na kuanzishwa kwa  kambi za mafunzo Kongwa, Mgagao, Msata, Nachingwea na Chunya.
“Bila kuficha Mandela amekuwa akizungumzia kuwa hatamsahau Nyerere kwa mchango wake, kwani wakati mataifa wakiona ukombozi ungekuwa mgumu, Nyerere ndiye aliyeamini kuwa tungefanikiwa.
“Mandela alisema siku zote anawakumbusha wenzake kutoisahau Tanzania, TANU na CCM.
“Wakati mwingine CCM ilifanya mazungumzo na vyama hivyo, ni kwa sababu hiyo, wenzetu ni watu wema na mara ya mwisho tulipokutana na vyama vilivyopigania uhuru, tulikubaliana kujenga chuo katika kukumbuka hili.
“Katika mazingira haya ya vyama vingi, watu wengine wangependa hata hilo tusilitaje, lakini hii ni historia haifutiki, kama chama chako kimeanzishwa sasa hiyo ni bahati mbaya,” alisema.
Rais Kikwete alisema katika uhusiano uliokuwapo kati ya Mandela na  Tanzania, mwaka 1964 kiongozi huyo akiwa njiani kwenda Algeria alifikia nyumbani kwa Asanterabi Nsilo Swai ambaye alikuwa Mwekahazina wa Tanu.
“Baada ya njia ya kudai uhuru kwa amani kukwama, Mandela na chama chake cha ANC walianzisha Jeshi la kupigania Uhuru. Akiwa kiongozi  katika harakati za kuimarisha Jeshi, alipita hapa mwaka 1964 akielekea Algeria.
“Kitu ambacho watu wengi hawajui, ni kuwa alipopita hapa alifikia nyumbani kwa Swai ambaye sasa ni marehemu, na alipoondoka aliacha viatu vyake kwa lengo la kuja kuvichukua atakaporudi kutoka Algeria.
Kikwete alisema kwa bahati mbaya Mandela  alipotoka Algeria, hakupita nchini akaenda moja kwa moja Afrika Kusini ambako alikamatwa na kufungwa miaka 27 jela.
Kikwete alisema baada ya kuachiwa huru, yeye akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alifuatwa na mke wa marehemu Swai, Vicky na kumweleza kuwa ana viatu vya Mandela.
“Nilimuuliza mama una uhakika? Akajibu ana uhakika maana yeye ndiye aliyempokea na kuomba tumrudishie Mandela viatu vyake kwani amekaa navyo tangu 1964.
“Baada ya kuwasiliana na Mandela alipokuwa Rais, alisema anavikumbuka sana na kuomba tumpelekee. Tulifanya msafara wa kurudisha pea moja ya buti. Hii inaonesha uhusiano wa karibu uliokuwapo kati ya Mandela na viongozi waasisi wa Taifa hili, kati ya  vyama vya TANU, ASP na baadaye CCM na ANC,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema Mandela alikuwa mwanamapinduzi wa dhati aliyechukia dhuluma, ubaguzi wa rangi na unyanyasaji dhidi ya mwanadamu bila kujali rangi, kabila na dini yake.
“Alipigania haki, usawa, maendeleo sawia ya watu wa nchi yake, alikuwa mpigania uhuru na mpigania haki za watu wa Afrika Kusini kwa ujasiri na ushupavu mkubwa.
Alisema Mandela hakukubali kutishwa, wala kutishika na ubabe na mabavu ya vyombo vya dola vya makaburu wakati ule, utawala ambao ulikuwa na ukatili ambao hauna mfano,  unaokaribiana na ule wa Adolf Hitler, aliyekuwa kiongozi wa kundi la Nazi la Ujerumani baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia.
“Mandela ni mtu wa aina yake, mtu ambaye kwa miaka mingi iliyopita hajawahi kuonekana hapa duniani na kwa miaka mingi ijayo, haitakuwa rahisi kumpata mtu wa aina yake,” ndivyo alivyomuelezea Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema Mandela alikuwa mtu jasiri aliyekuwa tayari kujitoa mhanga na kupoteza maisha yake kwa ajili ya kutetea haki za watu wake.
“Kwa mabavu ya makaburu, ilihitaji mtu mwenye moyo wa kupambana nao, yeye alisimamia alichokiamini, alikuwa tayari kufa lakini si kubadili msimamo wake wa kutetea haki za watu weusi. Mambo haya ndiyo yaliyomfanya Mandela awe mkubwa kuliko maisha yake,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema kinyume cha matarajio ya wengi ndani na nje ya Afrika Kusini, Mandela alionesha uungwana kwa kuwasamehe waliowatesa na kuimba wimbo wa umoja uliosaidia kujenga Taifa hilo.
“Ilikuwa kinyume na matarajio ya wengi na hofu kwa Wazungu ndani ya Afrika Kusini na mataifa yaliyokuwa yakiwaunga mkono Makaburu na kutupinga sisi, walidhani kwa mateso aliyofanyiwa Mzee Mandela na Waafrika baada ya kutoka gerezani, kitu cha kwanza kingekuwa kulipiza kisasi.
 “Lakini yule mzee aliwashangaza wengi, badala ya kulipiza kisasi, akawasamehe na akaanzisha Tume ya Maridhiano, ambayo mtu yeyote aliyefanya madhambi alienda huko na kutubu madhambi yake, ni kama huku kwetu tungesema ‘albadili bayana’.
“Mtu anakwenda kueleza alichofanya na yanaisha pale pale, na ukishakiri unakuwa umejikomboa na moyo wako na unaondoka kwenda kujiunga na wenzako katika kuleta maendeleo.
“Jambo kama hili ni gumu, kwani baadhi yetu hapa tunajiandaa kulipiza kisasi, mtu anasema nikipata tu mtanikoma,” alisema.
Alisema uungwana wa Mandela ndio uliofanya akajenga Taifa tulivu na kuendelea na kwa sifa hiyo ndio maana viongozi wa nchi kubwa duniani wanahudhuria mazishi yake.
“Nimebahatika kukutana naye nikiwa Waziri wa Nishati kwenye Mkutano wa Dunia wa Nishati, mkutano ulifungwa na Mandela, wakati ule   muda wote alikuwa ni mcheshi.
“Siku moja alikuja hapa nchini alipokuwa msuluhishi wa Burundi baada ya Mwalimu Nyerere, alinitania akisema mbona umekuwa mrefu zaidi ya mara ya mwisho nilipokuona.
“Nilimuuliza kwa umri wa miaka 45 naweza kukua tena? Alinijibu kuwa wewe unabahati wakati wenzako tumekoma kukua, wewe unakua,” alisema na kuongeza kuwa hayo yalikuwa maisha yake ya ucheshi.
Rais Kikwete alisema Mandela alikuwa rafiki mkubwa wa Tanzania na  uhusiano huo mpaka sasa unaendelezwa na nchi hizo mbili, kutokana na    mbegu na mizizi iliyopandwa na kiongozi huyo.
“Ni kiongozi aliyesogeza uhusiano mzuri wa nchi hizi, tunafanya kazi kwa karibu, pamoja na yeye kuondoka, akaja Mbeki (Thabo, Rais wa Pili wa Afrika Kusini huru) na baadaye Zuma (Jacob, Rais wa sasa) tumekuwa na uhusiano mzuri tuliojenga naye.
“Jambo kubwa la kukumbuka, Tanzania imekuwa na mchango wa ukombozi wao. Na hata nilipokwenda kumjulia hali na mke wangu alikuwa akisisitiza uhusiano wetu,” alisema Rais Kikwete.
Katika kuendelea kuonesha uhusiano wa Tanzania na Afrika Kusini, Rais Kikwete alizungumzia majeshi ya nchi hizo mbili yalivyosaidia kuondoa waasi wa M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
“Tuombe Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira wenzetu, baada ya kuondokewa na kiongozi wao na waendelee kuwa wamoja, na sisi tuungane na wananchi wa Afrika Kusini na dunia tumuombee Mandela kiongozi wetu mapumziko mema,” alisema.
Rais Kikwete pia waliwapongeza Watanzania kwa kusherehekea miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Katika maadhimisho hayo ambapo wananchi walisimama kwa dakika moja kuomboleza kifo cha Mandela, yalipambwa na gwaride la vikosi vya Ulinzi na Usalama waliopita kwa mwendo wa pole na haraka mbele ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Kikwete na halaiki ya vijana.

No comments: