Tuesday, December 10, 2013

MAAMUZI YA OMBI LA SHEKHE PONDA KUTOLEWA LEO...

Shekhe Ponda Issa Ponda.
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo itatoa uamuzi wa kusikiliza au kukataa ombi la Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Shekhe Issa Ponda.
Hatua hiyo inatokana na upande wa Jamhuri kuwasilisha pingamizi la awali wakiomba Mahakama hiyo itupilie mbali ombi hilo kwa kuwa lina kasoro za kisheria, ambazo haziwezi kurekebishika.
Jaji Rose Temba anayesikiliza ombi hilo, atatoa uamuzi huo leo baada ya kupitia hoja za pande zote mbili.
Katika ombi hilo, Shekhe Ponda anaiomba Mahakama ifanye marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, uliokataa kumfutia mashitaka ya kukiuka amri ya Mahakama.
Awali akiwasilisha hoja za kupinga kusikilizwa kwa ombi hilo Wakili Mkuu wa Serikali, Bernard Kongola alidai kuwa ombi hilo ni batili kwa kuwa kiapo kinachounga mkono kina mapungufu, kinyume na Kifungu cha 8 cha Sheria ya Viapo.
Alibainisha mapungufu hayo kuwa ni kutokuwepo kwa tarehe katika kiapo hicho, kilichoapwa na Wakili Hamidu Ubaidi. Pia, alidai kiapo hicho hakijaeleza kama aliyeapa, alifanya hivyo mbele ya wakili anayemfahamu.
Wakili wa Ponda, Nassoro Juma aliomba Mahakama itupilie mbali pingamizi hilo kwa kuwa halina msingi kisheria, bali ni maelezo, na kuangalia ombi hilo kwa jicho la haki na siyo kiufundi, alidai pingamizi hilo limewasilishwa kwa nia ya kuchelewesha kesi ili mshitakiwa aendelee kukaa rumande.
Ponda anadaiwa kukiuka amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyomtaka kutotenda kosa kwa mwaka mmoja, na kutotoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama.
Hata hivyo, Shekhe Ponda aliomba mashitaka hayo yafutwe katika Mahakama ya Morogoro au yahamishiwe katika Mahakama iliyotoa amri hiyo, kwa kuwa Mahakama hiyo ya Morogoro haina mamlaka ya kusikiliza.

No comments: